0 0
Read Time:3 Minute, 15 Second

Na Abbas Mwalimu (0719258484).

Alhamisi tarehe 10 Juni, 2021.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (MB) amewasilisha mapendekezo ya Serikali ya Shilingi Trilioni 36.33 kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Katiba hotuba yake, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba aliainisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria kadhaa ikiwemo Sheria ya Petroli, SURA 392

Kwa mujibu wa Waziri Dkt. Nchemba ameomba kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Petroli ili kuongeza tozo ya
Mafuta ya Taa kutoka shillingi 150 hadi shillingi 250. Lengo la hatua hiyo likiwa ni kupunguza uchakachuaji wa mafuta kufuatia ongezeko la ushuru wa mafuta kwenye dizeli na petroli.

Kufuatia hotuba hiyo ya Waziri wa Fesha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba, Mbunge wa jimbo la Sengerema Mheshimiwa Hamis Mwagao almaarufu kama Tabasamu alifanya mahojiano na TBC1 na kueleza kuwa ongezeko la shilingi 100 litasaidia katika ujenzi wa barabara za vijijini kwani fedha zitakazopatikana kutokana na ongezeko hilo zitaelekezwa Mamlaka ya Barabara Vijijini yaani TARURA ili ziweze kusaidia ujenzi wa miundombinu ya barabara na hivyo kuokoa maisha ya kina mama wanaojifungua njiani kutokana na kukosa huduma ya barabara kama alivyoeleza Waziri Dkt. Mwigulu Nchemba katika hotuba yake.

Mbali na hayo Mheshimiwa Tabasamu ameeleza kuwa wao kama wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wataishauri Serikali ijielekeze katika kuagiza mafuta kwa wingi kutoka kwa wazalishaji moja kwa moja kutoka nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi kama vile Qatar, Kuwait na Saudi Arabia.

Hili ni wazo jema sana na lenye kutia matumaini ya kupungua kwa gharama za mafuta ya dizeli na petroli nchini na hivyo kupunguza gharama za maisha kwa wananchi wengi wa kipato cha chini.

Mbali na ushauri huu wa Mheshimiwa Tabasamu nadhani kuna haja kwa Serikali kuangalia namna gani inaweza kukifufua kiwanda cha kuchakata mafuta cha TIPER yaani Tanzania International Petroleum Reserves Limited ambacho kwa sasa kinaendeshwa kwa ubia baina wa 50 kwa 50 ya Serikali ya Tanzania kupitia TPDC na kampuni ya mafuta ya Oryx Energies SA ya Switzerland.

Miaka ya 1970-1980 kabla ya mabadiliko ya kimfumo na kimuundo yaliyopendekezwa na Benki ya Dunia (World Bank) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) TIPER iliyokuwa ikiendeshwa kwa ubia baina ya kampuni ya mafuta ya Italia Agip na serikali ya Tanzania ilikuwa na uwezo wa kusafisha mafuta ghafi yanayoagizwa kutoka nje na hivyo kufanya bei ya mafuta kuwa yenye unafuu kwa watumiaji wake.

Ni imani yangu kuwa kuirejesha TIPER iliyokuwa miaka ile ya 1970 ambayo ilikuwa na uwezo wa kusafisha mafuta (refinery) kwa sasa itasaidia si tu kupunguza bei ya mafuta lakini pia kusaidia kuendeleza viwanda (kupitia mafuta ya HFO) na kupunguza kama si kuondoa kabisa matumizi ya mkaa na hivyo kulinda mazingira kutokana na kupatikana kwa mazao mengine ya mafuta ghafi kama vile gesi za LPG ambazo butane na propane n.k ambazo utumikaji wake umeongezeka sana kwa sasa kama takwimu za EWURA za mwaka 2020 ambapo metriki tani 189,509 ziliagizwa kutoka nje.

Ni vipi kama gesi hizi zikiwa zinachakatwa hapa hapa nchini?

Si hayo tu uchakataji wa mafuta ghafi (petroleum) unatoa mazao mengi kuanzia lami, mafuta ya meli, oil za magari, dizeli, petroli, mafuta ya taa, mafuta ya ndege, mafuta ya kutengeneza kemikali sambamba na gesi za butane na propane ambazo nimezitaja awali.

Kwa maoni yangu ushauri wa Mheshimiwa Tabasamu kwa Serikali ni mzuri sana lakini naamini utaleta tija zaidi endapo ataishauri Serikali kuangalia namna bora ya kufufua kiwanda cha TIPER ili kiweze kuchakata mafuta ambayo ameweka bayana kuwa ataishauri serikali iagize kwa wingi lakini badala ya kutaka Serikali iagize kwa wingi ni vema pia akashauri kuagizwa kwa mafuta ghafi ambayo yatasafishwa hapa nchini kama ilivyokuwa zamani tofauti na ilivyo sasa ambapo matanki ya TIPER yanatumika kama ghala za kuhifadhia mafuta ya kampuni ya Oryx iliyo katika mkataba na Serikali ya Tanzania.

Nawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wenu:

Abbas Mwalimu (Facebook|Instagram|Twitter).

+255 719 258 484

Uwanja wa Diplomasia (Facebook|WhatsApp).

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %