

George Michael Uledi.
Kyela, Mbeya.
June 18, 2021.
Mambo yanayoendelea kufanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Samia Suluhu Hassan kupitia makundi mbalimbali kwenye jamii yanatupa funzo kubwa vijana Nchini kwamba kamwe usimchukulie poa mtu yoyote bali muda ndio utaongea!Mpaka sasa kila makundi mitaani na kila kona ni kama wameamua kumvulia kofia Mh Rais Samia Suluhu Hassan kabla hata hajatimiza siku mia moja Ofisini.
“…Mama anaupiga mwingi sana,..mama mtu hatari sana,ukizingua ntaku mzingua,…Mama anakuja na mkeka…….”haya ni baadhi ya misemo inayotamba kwa sasa kila kona ya Tanzania yote yakilenga kuukubali muziki wa Mama na hivyo Samia Suluhu Hassan kuweza kubadilishana upepo ndani ya siku chache za utawala wake.
Hakuna ubishi kuwa ile “style” yake ya kukutana na kila kundi katika jamii”Wazee,Wamama na Vijana” imefanikiwa sana kutoa picha ya nini anataka kitokee kwa kila kundi kwa kuhakikisha Serikali yake inaandaa mipango kabambe na wa kimkakati kwa kila kundi kwa lengo wa kuwapatia fursa makundi husika ya kuweza kubadilisha maisha yao!Hakuna “strategy” iliyompa pointi Mama kama hii,hongera mingi mingi kwa wachora ramani wake.
JE MH. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN NI JOHN MAGUFULI WA JM KIKWETE?
Wala usitumie nguvu kupata tafsiri kuhusu kichwa cha makala haya hapo juu kwani ninachotaka kusema ni falsafa rahisi sana kueleweka kwako na kwa wasomaji wengine.Nataka kusema nini?
1.Wote tunajua kuwa hayati John Magufuli Rais wa awamu ya tano alikuwa ni mhudumu katika Serikali ya awamu ya nne ya Jakaya Kikwete katika nafasi za Uwaziri na ni wazi kuwa alikuwa mmoja wa Mawaziri tegemeo sana mpaka JK aliwahi kumsifia.
Pamoja na uchapakazi wake lakini pia JPM alikuwa na maono yake moyoni siku akija kupewa nafasi ya kuiongoza Tanzania na maono haya uwenda angeyatamka wakati wa uwaziri wake ndani ya Serikali ya JK labda angeshatumbuliwa na bosi wake, Mzee Jakaya Kikwete.
2.Cha kujifunza hapa kwa sisi viongozi vijana ndani ya Taifa ni kwamba,kwanza unapopewa lifti kamwe usipige honi!Wajibu wako unapopata uteuzi ni kutumikia lengo la mamlaka ya uteuzi kwa akili na nguvu zako zote hata kama unadhani lengo la mkuu wako sio sahihi sana!Unapaswa akili na maono yako uyaweke kabatini kwako kwanza mpaka siku na wewe ukapata nafasi ya kuendesha jahazi.
3.Hayati John Pombe Magufuli baada ya Mwaka Desemba 2015 kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,hakuwa yule mfuasi wa Jakaya tena kwani sura,dira na maono yake yalikuwa wazi zaidi na tukaanza kusikia maneno ambayo hapo kabla yasingeweza kutoka katika mdomo wake hapo kabla..”Nchi imeliwa sana hii,…Tanzania sio masikini,…Nani atafanya haya nisipofanya mimi?,si walikuwepo,mbona hawakufanya…..?”.haya yalikuwa ni baadhi ya maneno magumu lakini yenye kuleta hali mpya na kujiamini kwa Watanzania.
Haya sio matusi kwa mwanasiasa muelewa bali ni ishara kwamba zama za kale tayari zimebadilika”regime change”hivyo kwa kiongozi mzuri kijana lazima ujiandae kisaikolojia kucheza muziki wenye korasi mpya tena kwa nguvu zaidi kuliko hapo kabla!
4.Mmoja wa wacheza korasi hiyo ya muziki mpya wa awamu ya tano alikuwa Rais wa sasa wa JMT Mh. Samia Suluhu Hassan!Sina uhakika saana kwamba alicheza kwa kuipenda au alicheza sababu ilikuwa ndio korasi inayopaswa kuchezwa kwa wakati husika.
6.Nani ambaye anaweza kusimama leo na kusema JPM hajafanya makubwa katika Nchi hii kwa miaka yake mitano?Ni katika muktadha huo huo wa mawazo mapya katika Taifa JPM na msaidizi wake Mama Samia walikuja kufanya mambo ambayo itakuwa ngumu kufutika katika Taifa!JPM alipewa nafasi akafanya hivyo tuwaache wengine pia wapewe nafasi waweze kutekeleza maono na ndoto zao kwa Taifa lao Tanzania.
HATA MH RAIS SAMIA SULUHU HASSAN HAWEZI AKAWA YULE SAMIA WA JPM.
Ni wazi kuwa Mh. Samia Hassan huyu “anaupiga mwingi” sana kwani kabla hata hajatimiza siku mia moja za kukaa Ikulu tayari watu hasa vijana wanasema wameanza kuona mwanga katika maisha yao ya kila siku!Sio rahisi sana kushawishi vijana ndani ya siku chache tu za utawala wako,sio kawaida sana!
1.Mwanzoni labda hakueleweka pale aliposema sitaki kodi za dhuluma na vijana wengi wakadhani labda kutakuwa na ulegevu katika makusanyo lakini ikawa tofauti kabisa kwani makusanyo ya TRA ya mwezi March,April na May 2021 yameweza kupaa zaidi.
2.Kale kakikundi kamtandaoni ambako mwanzo kalidhani Mama Samia anapoteza “direction” ni kama kakundi kale kenyewe ndio kimeanza kupoteza”direction” sasa kwani hotuba ya Mama pale uwanja wa Nyamagana imebadili akili za vijana katika Taifa!
Vijana wa Tanzania wanaona labda Leo na kesho yao itakuwa nzuri zaidi katika awamu ya sita kuliko huko nyuma kwani angalau Serikali ya Samia Suluhu Hassan inasema wazi ni aina gani ya vijana Taifa lina taka kuwanao.
3.Mh.Rais Samia huyu sio yule wa awamu ya tano,huyu ana maono makubwa kwa vijana na anasema wazi kuwa wakati wa vijana kuendesha Taifa ni sasa!”….kuna mkeka wa MDC unakuja na wote ni vijana,japo tukiwapa nafasi mnatuangusha…..”.
Itoshe kusema kwamba Samia huyu alikuwa Magufuli wa Jakaya Mrisho Kikwete lakini kwa sasa huyu ndio Samia Suluhu Hassan mwenyewe,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Hesabu za kwamba Mama huyu atafanya “wonders” kubwa zaidi zipo wazi na zinaonekana kwani wenzetu wazungu wanasema”namba hazidanganyi”.
Kazi Iendelee!
+255784159968.