
Na Abbas Mwalimu (0719258484).
Jumapili tarehe 29 Ago nosti, 2021.
Miongoni mwa mambo yaliayoshika hatamu ya mijadala mitandaoni kwa sasa ni suala la tozo ya miamala ya simu kwa kutuma na kupokea pesa nchini.
Kodi ikiwemo tozo hizi za miamala hutumika kama njia ya uongezaji wa mapato ya ndani ya nchi lakini uwepo wake umekuwa ni tatizo kubwa sana kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kama alivyobainisha Drummond na wenzake mwaka 2012, licha ya kuwa ndiyo njia kubwa ya kupunguza utegemezi wa misaada ya kigeni na kuifanya Serikali iweze kutoa huduma muhimu kama vile maji, afya, shule na barabara kupitia makusanyo ya kodi.
Lakini wakati hali ya sintofahamu ikiendelea hivyo mitandaoni na mitaani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliweka bayana kuwa tozo zitaendelea kuwepo kwa kuwa watanzania wamezielewa isipokuwa tu serikali itazitazama upya tozo hizo.
Rais Samia Suluhu Hassan aliyasema hayo pindi alipowaapisha Mabalozi wateule Ikulu Dar Es Salaam mwezi Julai sambamba na alipofanya mahojiano na Mwandishi wa BBC Salim Kikeke. Katika hotuba yake kwa watanzania kupitia kwa mabalozi hao Mheshimiwa Rais alisema na hapa ninamnukuu:
“Ninachotaka kusema makato haya yaliwekwa kwa nia njema tu, nchi yetu sasa hivi wakulima wameamka na kilimo kikubwa lakini wakivuna wanashindwa kutoa mazao yaliko kuleta kwenye maeneo ya masoko, tatizo ni njia za vijijini hakuna, kwa hiyo sehemu ya fedha hii au sehemu kubwa itakwenda kujenga njia za vijijini tuwafanye wakulima watoe mazao walete kwenye masoko wafaidi jasho lao lakini na bidhaa zile zisiwaharibikie mikononi ziende kwenye masoko.”
Na katika kusisitiza hili la tozo, akijibu swali la Salim Kikeke kuhusu malalamiko ya wananchi juu ya tozo Mheshimiwa Rais Samia alisema:
“Nadhani lalamiko kubwa la wananchi lilikuwa kuangalia zile, kiasi kilichowekwa cha mkato, lakini hawakulalamikia tozo, wamelalamikia kiasi au namna ya makato.” Mwisho wa kunukuu.
Na katika kukumbushia kile alichosisitiza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Jumamosi tarehe 28 Agosti, 2021 Msemaji wa Serikali ndugu Gerson Msigwa alikutana na waandishi wa habari katika Ofisi ya Idara ya Habari-Maelezo jijini Dodoma ambapo licha ya kufafanua mambo mengine mbalimbali alieleza pia kuwa uamuzi juu ya tozo ya miamala utatolewa Jumanne tarehe 31 Agosti, 2021. Ndugu Msigwa alisema na hapa ninamnukuu:
“Kauli, uamuzi na msimamo rasmi wa serikali kuhusu suala la sintofahamu ya tozo ya miamala ya simu itatolewa Agosti 31, 2021 baada ya taratibu za ndani kukamilika baada ya ripoti ya ukusanyaji maoni kutoka kwa wananchi kupokelewa kwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa.” Mwisho wa kunukuu.
Ni kwa kiasi gani wananchi wameelewa tozo hizi na umuhimu wake kwa maendeleo ya nchi na mtu mmoja mmoja? Nadhani hili ndilo swali la msingi ambalo linapaswa kujengewa hoja.
Kwa mtazamo wangu mimi naona shida haipo kwenye tozo yenyewe tu bali ipo kwenye elimu juu ya namna gani tozo hizi zinatumika, kwangu hili ndiyo suala la msingi ambalo naamini wananchi wanataka kuona matokeo yake. Hivyo bado ninaamini kuwa hata kama serikali ikiamua kupunguza tozo za miamala lakini bado malalamiko bado yataendelea kuwepo kutoka kwa baadhi ya watu.
Kimsingi, shida kubwa ya nchi za Afrika ni ukwepaji wa kodi, hili lilibainishwa katika ripoti ya IMF ya mwaka 2011. Lakini pia si Afrika tu bali ni duniani kote ukwepaji wa kodi ni mkubwa kama walivyobainisha McKerchar na Evans mwaka 2009, isipokuwa tu nchini za Afrika ndizo zinazongoza kwa tatizo hili la ukwepaji kodi, haya yalibainishwa na Cobham (2005) na Fuest na Riedel (2009).
Kwa kuangalia tafiti hizo tunaona kuwa shida kubwa ya nchi zinazoendelea kiuchumi duniani na hasa hizi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ni wananchi kutoona matokeo ya kodi wanazolipa na hivyo kukwepa kodi, hili ndiyo tatizo kuu kwa maoni yangu.
Tafiti mbalimbali zilizofanywa na Kamasa na wenzake (2019), Merima na wenzake na Abdu na wenzake (2020) zote zimeonesha kuwa wananchi wamekuwa wakikwepa kodi au kuwa na tabia ya kutolipa kodi kwa sababu hawaoni matokeo ya moja kwa moja ya kodi wanazolipa.
Licha ya mtazamo huo, kwa mtazamo wangu mimi naona kwamba si kuwa hawaoni matokeo ya kodi wanazolipa bali Serikali za nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara hazifanyi juhudi za dhati kuwafikia wananchi hasa wa vijijini na kuwaelimisha juu ya uhusiano uliopo kati ya kodi wanazotozwa na kile wanachoona kinafanywa na serikali katika maeneo yao ikiwemo ujenzi wa shule, hospitali, vituo vya afya, maji na barabara.
Kwa mfano, hatua inayochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sasa kupitia kwa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwingulu Nchemba na Mhe. Ummy Mwalimu kutangaza makusanyo yaliyopatikana kupitia tozo za miamala na mgawanyo mgawanyo wake katika ujenzi wa vituo vya afya na shule ni hatua kubwa sana lakini hatua hii isiishie kwa Dkt. Mwingulu Nchemba na dada yangu Ummy Mwalimu tu bali iende kwa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, madiwani, wenyeviti wa serikali za mitaa na wenyeviti wa vijiji. Nafahamu kuwa baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya wameanza kufuata mkondo huo lakini bado mikoa mingine na wilaya ambako pesa hizo zimepelekwa wana wajibu wa kufanya hivyo.
Madiwani wa Kata husika ambao Kata zao zimepatiwa fedha za ujenzi wa majengo ya shule au vituo vya afya wana wajibu wa kuitisha vikao na kuwaeleza wananchi wao kuwa fedha hizo walizopokea zimetokana na tozo za miamala ya simu na endapo kuna fedha nyingine wanatarajia kupokea mwezi au miezi inayokuja wawaeleze wananchi. Ifanyike hivyo pia kwa wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji ambavyo miradi hiyo inafanyika.
Tatizo lingine la nchi zetu Afrika si kukosa sera nzuri, tuna sera nzuri mno, shida yetu ni utekelezaji wa sera hizo, na utekelezaji huu wa sera hupata changamoto zaidi kwa sababu hakuna uelewa wa pamoja baina ya wananchi na serikali juu ya nini Serikali imekipanga au inafanya kwa wananchi wake.
Kwa kifupi ni kwamba serikali inajua nini inataka kufanya kwa wananchi wake lakini kutokana na kukosekana kwa ufikishwaji au ufikishwaji sahihi wa kile ambacho serikali inakipanga au inakifanya wananchi wanakuwa hawaelewi dhamira ya Serikali zao. Hili liliwahi kubainishwa pia katika utafiti wa OECD na SIDA.
Kuthibitisha haya, utafiti uliofanywa na Kamasa na wenzake (2019) wenye kichwa *’Tax Compliance in Sub-Saharan Africa: How Important are Non-Pecuniary Factors? kwa kutumia matokeo ya Mzunguko wa 5 wa utafiti kutoka taasisi ya utafiti ya Afrobarometer uliofanywa katika nchi 29 za Afrika ulibainisha kuwa tatizo la ufahamu juu ya kodi na umuhimu wake kwa maendeleo, kutokuwa na imani na usimamizi wa kodi, na kwamba utoaji wa huduma za afya elimu na mahitaji ya barabara yanatoa uwezekano mkubwa kwa wananchi kupenda kulipa kodi katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kwa kuonesha umuhimu wa serikali kutoa mrejesho kwa wananchi mpaka vijijini juu ya uhusiano wa huduma za afya, elimu, barabara na kodi wanazotozwa wananchi Merima Ali na wenzake nao walitumia utafiti wa Mzunguko wa 5 wa Afrobarometer kueleza sababu zinazofanya wananchi wasipende kulipa kodi katika chapisho lao, ‘Factored affecting tax compliant attitude in Africa: Evidence from Kenya, Tanzania, Uganda and South Africa’
Lakini zaidi Abdu na wenzake (2020) waliongeza kwa kuitazama rushwa kama chanzo cha ukwepaji kodi katika utafiti wao ‘Analysis of Tax Compliance in Sub-Saharan Africa: Evidence from Firm-Level Study.’ Hivyo basi kodi ya tozo za miamala kwa kiasi fulani itasaidia kupunguza nakisi ya kutofikia malengo ya ukusanyaji kodi kila mwaka wa fedha wa serikali inayosababishwa na ukwepaji kodi kutokana na rushwa licha ya uwepo wa sababu nyingine.
Ninaamini kuwa kama elimu hii ya uhusiano uliopo baina ya tozo za miamala na fedha zinazogawanywa kwa maeneo husika nchini ukielezwa kwa kina mpaka vijijini, wananchi wataongeza uelewa na kupenda kulipa kodi, si tu kupitia miamala bali hata zile kodi nyingine.
Ninaamini hata kama serikali ikipunguza tozo, bado kuna watu watalalamikia tozo hizo, kwangu nadhani jambo muhimu ni watu kushuhudia kwa macho matunda ya kile wanachotozwa, kwa mfano mwananchi akiona kijijini kwake kuna barabara ya lami sidhani kama hatoelewa uhusiano uliopo baina ya kile alichotozwa na hiyo barabara, kwa nini? Kwa sababu nchi inavyojengwa ni kama nyumba pia, mtu ukitaka kujenga nyumba utadunduliza ukijinyima mpaka utajenga, ni sawa na tozo.
Sababu nyingine inayonifanya niamini kuwa kunahitajika elimu ya kina juu ya uhusiano wa tozo za miamala na huduma kama shule, vituo vya afya na barabara ni kwamba nchi 11 duniani ndizo zinazoongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha kutoza kodi lakini ndizo zenye huduma bora kwa wananchi wao.
Ripoti ya OECD ya mwaka 2013 na 2016 inazitaja nchi za Denmark, Norway, Marekani ,Canada, Switzerland, Iceland, Uingereza, Luxembourg, Sweden, Belgium, na Finland kuwa ndizo zenye kiwango kikubwa cha kodi duniani. Lakini tujiulize nchi hizi si ndiyo zinakamuana kodi mpaka kufikia kutupa sisi misaada? Sisi hatuwezi kujihudumia kwa kodi zetu?
Kwa mfano, nchi ya Finland ina makato ya kodi mbalimbali kati ya asilimia 25 mpaka 40 katika kodi yao ya Mapato ya Taifa ama National Income Tax, rejea ripoti ya Taxation in Finland.
Kwa msingi huo naamini kabisa tatizo halisi la tozo za miamala ni sisi wananchi kuelewa uhusiano uliopo kati ya tozo na huduma zinazotolewa. Muhimu zaidi ni serikali kutoa huduma bora za afya, elimu, maji na barabara ili wananchi waone uhusiano wa kodi na matokeo ya kodi kwa macho yao kwani Merima Ali na wenzake walibainisha katika ukurasa wa 7 wa utafiti wao kwa kusema: ‘In Tanzania as many as 16% of the respondents consider poor public services to be the main reason why some people evade taxes.’
Kwa mantiki hiyo kuna umuhimu wa serikali kuendelea kutoa huduma bora za afya, elimu, maji na barabara lakini pia serikali iwajengee wananchi uelewa juu ya tozo za miamala ya simu na uhusiano wake katika utoaji wa huduma hizo muhimu hasa kuanzia ngazi ya vijiji, mtaa, kata, wilaya mpaka mkoa.

Asanteni kwa kusoma:
Abbas Mwalimu (Facebook|Instagram|Twitter).
+255 719 258 484
Uwanja wa Diplomasia (Facebook|WhatsApp).








