0 0
Read Time:4 Minute, 21 Second

Na Abbas Mwalimu (0719258484).

Jumamosi tarehe 11 Septemba, 2021

Mwishoni mwa miaka ya 1970 na 80 Afrika ilitawaliwa na wimbi tawala za kijeshi (Rejea Huntington 1996: Diamond 1996: Jaggers na Curr, 1995 na Bratton, 2009:340) jambo ambalo lilizisukuma nchi Magharibi na Benki ya Dunia kuangalia namna ya kutafuta njia ya kurejesha tawala hizo mikononi mwa raia.

Ndipo, mwaka 1981 Benki ya Dunia ikaja na kile kilichojulikana kama, Ripoti ya Berg ya mwaka huo 1981. Ripoti hii ambayo ilidhaminiwa na Taasisi za Bretton (Benki ya Dunia na IMF) ilijulikana pia kama ‘Accelerated Development in Sub-Saharan Africa: An Agenda for Action.’

Kwa mujibu wa ripoti ya Berg, mojawapo ya changamoto za Afrika ni kuwepo kwa tawala zisizo za kidemokrasia ambazo zimesababisha chumi za nchi za Afrika kuwa na afya dhaifu (Fosu, 2018). Hivyo kulikuwa na umuhimu wa kuhakikisha kunakuwa na demokrasia na hasa demokrasia ya siasa ya vyama vingi.

Lengo mojawapo la kuanzishwa kwa taasisi za kidemokrasia kwa mujibu wa katiba (constitutional democratic) Afrika lilikuwa ni kulinda mamlaka ya taasisi za kiraia dhidi ya kuingiliwa na utawala wa kimabavu (Handy na Djiko, 2020).

Ni ukweli uliowazi kuwa masharti ya IMF na Benki ya dunia ulilazimisha tawala nyingi za kijeshi kurejesha madaraka mikononi mwa tawala za kiraia, lakini baadae miaka ya 1990 mwishoni mpaka miaka ya 2000 mwanzo pakaibuka wimbi la mapinduzi ya kijeshi hasa katika nchi za Afrika Magharibi kama vile Nigeria (1996) Burkina Faso, Niger, Guinea Bissau, Benin na hivi karibuni Mali (2018) na Guinea (2021).

Hali hii ya ubadilishanaji wa madaraka kwa njia isiyo ya Kikatiba (mapinduzi) inalitia doa bara la Afrika licha ya kwamba huenda kuna sababu zinazopelekea hali hiyo.

Azimio la Lome la mwaka 2000 na Mkataba wa Afrika unaohusu Demokrasia, Uchaguzi na Utawala la mwaka 2007 yote yanatafsiri ubadilishanaji wa madaraka usio wa kikatiba (unconstitutional change of government) kuwa ni ule unaotokana mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali iliyochaguliwa kidemokrasia, majeshi mamluki kuingilia nchi na kuiondoa serikali iliyochaguliwa kidemokrasia, kikundi cha waasi na harakati za uasi kuchukua madaraka ya serikali iliyochaguliwa kidemokrasia, au Rais au Serikali iliyopo madarakani kukataa kukabidhi madaraka kwa serikali mpya kufuatia kushindwa katika uchaguzu uliokuwa huru na haki.

Lakini kama tayari nchi za Afrika zina miongozo kama huu wa Lome na ACDEG, kwa nini mapinduzi yameendelea kutokea?

Jibu la swali hili kwa sehemu fulani limetolewa na Umoja wa Afrika (AU) wenyewe kupitia Baraza lake la Amani na Usalama (AUPSC) katika ripoti yake ya mwaka 2014 ambayo ilibainisha kuwa upungufu katika utawala (deficiency in governance) husababisha mapinduzi ya kijeshi katika nchi husika.

Mbali na PSC kubainisha sababu za mapinduzi katika nchi za Afrika, lakini Issa na David (2012) katika andiko lao wao ‘The Challenges of Leadership and Governance in Africa’, Amusa na wenzake katika andiko lao ‘The Challenges of Democratization in Africa: Evidence and Way Forward for Nigeria’ la mwaka 2017 sambamba Handy na Djilo (2020) katika andiko lao ‘What causes Africa’s Coups? That’s the question’ wameainisha vyanzo vya upungufu katika uongozi vikiwemo ulafi wa madaraka, ubinafsi, kushindwa kusimamia utofauti baina ya watu na watu, makundi na makundi au jamii na jamii, kushindwa kuzikamata fursa mbalimbali za maendeleo, kutengwa kwa baadhi ya makundi au jamii katika keki ya taifa, kuwepo kwa tofauti kubwa ya kipato kati ya walio nacho na wasio nacho, umasikini, ukiukwaji wa haki za binadamu, kutokukubali matokeo ya kushindwa uchaguzi, kufanya hila ama ujanja wa kubadili katiba kwa njia zisizo za kikatiba kwa maslahi ya watu wachache, rushwa, kukosekana uwazi, kukosekana uwajibikaji, kukosekana utawala wa sheria.

Kwa kuvitazama vyanzo hivyo vyote tunaona kuwa mizizi yake ipo katika upungufu katika utawala (deficiency in governance). Kwa kukazia hilo Crocker (2019) katika andiko lake ‘Africa Governance: Challenges and their Implications’, yeye alibainisha kwa kusema, ‘In Africa, as in every region, it is the quality and characteristics of governance that shape the level of peace and stability and prospects for economic development’, kwamba kiwango cha ubora wa utawala na tabia zake ndivyo vinavyotoa tafsiri ya amani na utulivu na mafanikio ya kiuchumi.

Kwa maana nyingine ni kuwa utawala dhaifu ni chanzo cha migogoro (Crocker ,2019) na kwa bahati mbaya zaidi, kutokana na hali hiyo, wananchi pia wamejikuta wakiona kuwa jeshi ndiyo chombo pekee kinachoweza kuwaokoa na hali hiyo kama tulivyoona Guinea wananchi wakiimba, ‘Liberte’ huku wakiimbiza gari iliyokuwa imembeba Alpha Conde.

Hili lilibainishwa pia na Tordoff aliposema ‘the military has supplemented civilian governments in Africa for several reasons; it has intervened to save, or has claimed to save the country from corrupt and inefficient politicians who had brought the
country to the verge of bankruptcy.’ Kwa lugha nyingine huu ndiyo mtazamo wa wananchi wa nchi zinazokumbwa na mapinduzi.

Je Afrika haikuongeza juhudi?

Mwaka 2011 Umoja wa Afrika ulikuja na Mpango wa Utawala wa Afrika ama Africa Governance Architecture kwa kifupi ‘AGA’ lakini bado inaonekana hali ya mapinduzi inaongezeka zaidi.

Hivyo basi ili kuondoa hali hiyo, kuna haja ya kuutazama upya mpango huu (AGA) kwa kuangalia namna ambayo wananchi wataweza kuziwajibisha serikali zao na kuongeza sauti ya maamuzi kuanzia kwa wawakilishi wao kama wabunge, madiwani n.k na zaidi utekelezaji wa sera uanzie ngazi ya wananchi wenyewe ili kuwepo na dhana ya umiliki na ushirikishwaji.

Asanteni.

Wenu:

Abbas Mwalimu (Facebook|Instagram|Twitter).

+255 719 258 484

Uwanja wa Diplomasia
(Facebook|WhatsApp).

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %