0 0
Read Time:2 Minute, 40 Second

NA Zain Kachumbari

Diaspora USA

Elimu ni ufunguo wa maisha!

1. Kulipa kodi mara mbili; nchi zilizoendelea hukamata kodi raia wake popote pale duniani. Tanzania nayo inatakiwa ifanye hivyo sasa hivi, hata kama haitatoa uraia pacha wala hadhi maalumu. Mwenye hadhi maalumu akifanya kazi nje ya Tanzania, kodi hii haitamuhusu.

2. Kuhudumia paspoti mbili; serikali madhubuti ikiwemo ya Marekani hulazimisha raia wake kutumia paspoti yao. Na Tanzania inatakiwa ifanye hivyo. Kuna uwezekano wa paspoti zote mbili kuonyeshwa airport. Mwenye hadhi maalumu hana tatizo hili.

3. Kugonganisha paspoti; kosa lolote kwenye paspoti, iwe ni la makusudi au bahati mbaya kama ni jina, tarehe ya kuzaliwa, mahali pa kuzaliwa nk. litasababisha adhabu ndogo kama kuzuiwa kusafiri au adhabu kubwa kama jela na kufutiwa uraia wa nchi moja hasa ya nje. Teh teh! waliojilipua kuwa ni wasomali na waburundi. Mahali pa kuzaliwa pataonyesha nchi tofauti kwenye paspoti ya Tanzania na paspoti za nje. Mwenye hadhi maalumu hahusiki kwa sababu ana paspoti moja tu.

4. Kunyimwa kazi muhimu; kazi muhimu za serikali na zinazohitaji kuaminiwa hasa kwa Marekani (clearance) hapewi mtu mwenye uraia pacha. Mwenye hadhi maalumu, atapata clearance hata ya kufanya kazi NASA.

5. Sheria za nchi mbili; kwa hapa mfano mzuri ni vijana kulazimika kujiunga na jeshi kwa lazima wakifikia umri fulani. Chukulia JKT nayo ni lazima. Na hii inaweza kusababisha mtu afutiwe uraia wa nje. Mwenye hadhi maalumu anavuta sigara yake tu, hayamuhusu haya.

6. Michezo na sanaa; hivi Mwakinyo angekuwa na uraia wa Marekani na Tanzania angepigana kwa bendera ya Tanzania? Ukitaka jibu itizame timu ya taifa ya Ufaransa.

7. Kupoteza uraia wa nje; kwa wenye asili ya Tanzania walio na uraia wa nje kwa nchi kama au Oman wakichukua uraia pacha Tanzania watapoteza uraia wao wa nje kwa sababu nchi hizo haziruhusu uraia pacha. Hadhi maalumu ndio kimbilio pekee la watu hawa kama wangejua.

8. Kupoteza mafao ya serikali; kwa serikali zinazotoa mafao ya kijamii. Katika mazingira fulani wenye uraia pacha huweza kujikuta matatani na serikali zote mbili, hasa ikiwa watachukua mafao kote kote. Chukulia uko Tanzania na unavuta mafao ya nyumba Marekani. Ukikinukisha ni mwendo wa jela au utakuwa hurudi tena Marekani. Mwenye hadhi maalumu, anakunywa soda na bisi hayamuhusu haya.

9. Kutopata uongozi wa siasa; mwenye uraia pacha haaminiki kushika uongozi katika nchi zote mbili. Mgombea urais Ted Cruz wa Marekani alilazimika kuutema uraia wake wa Canada. Mwenye hadhi maalumu hana tatizo hili katika nchi aliyo na uraia nayo.

Yote tisa kumi; ni kuwa uraia pacha hautolewi kwa wazawa wa Tanzania peke yake. Ni kwa mtu wa taifa lolote duniani mwenye kutimiza vigezo vya kuuomba. Hii ni hasara kwa wazawa wa Tanzania kwa sababu kwanza hawako wengi kama wageni watakaoomba uraia Tanzania. Pili hawana uwezo wa kushindana nao kiuchumi hasa katika uwekezaji. Kutakuwa na uhaba wa ardhi kwa sababu zitanunuliwa na wageni wataochukua uraia Tanzania. Vilevile hata biashara na kazi muhimu zitachukuliwa na wageni hasa kutokana na ubora wao wa elimu.

Ukiona wanalalamika utolewe uraia pacha kwa wazawa wa Tanzania tu, ujue dawa imekolea. Hapo sasa wanachozungumzia ni hadhi maalumu kwa jina tofauti.

Acha kufuata mkumbo. Elimika, jifunze, epukana na ujinga. Hadhi maalumu ndio chaguo lenye manufaa kwa wanadiaspora, serikali na taifa kwa ujumla.

Mungu Ibariki Tanzania!

Ni Zain wa Kachumbari!

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %