0 0
Read Time:4 Minute, 18 Second

WU® MediaPRODUCTION LIMITED

KULIKUWA NA HAJA GANI KWA SERIKALI KUTANGAZA SIKU TANO ZA MAOMBOLEZO YA KIFO CHA MALKIA ELIZABETH II?

Na Abbas Mwalimu
(0719258484).

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Jumamosi tarehe 10 Septemba, 2022 alitangaza siku tano za maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha Malkia wa Uingereza, Elizabeth II kilichotokea Alhamisi tarehe 8 Septemba, 2022 huko Balmoral, Uskochi.

Malkia Elizabeth II

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu maombolezo hayo ya kitaifa yatadumu kuanzia tarehe 10 Septemba, 2022 mpaka tarehe 14 Septemba, 2022 ambapo katika kipindi hicho bendera zote zitapepea nusu mlingoti ikiwemo balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali duniani.

Kumekuwa na mijadala mingi ikihoji kwa nini Tanzania iomboleze msiba huu ikiwa Uingereza inalalamikiwa na baadhi ya nchi kwa madhira ya ukoloni hasa Afrika.

Katika kutazama hilo makala hii itajielekeza katika utamaduni wa kidiplomasia ili kufahamu sababu za Tanzania kuomboleza msiba huu kwa siku tano.

Kimsingi diplomasia inazingatia sana historia, kanuni na utamaduni wa jamii husika.

Kihistoria Tanzania ina uhusiano mkubwa na Ungereza. Uhusiano huu unatoka na;

Mosi, Uingereza kuwa nchi iliyotawala pande zote mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maana ya Tanganyika na Zanzibar wakati huo zikiwa kama himaya ya Uingereza (British Protectorate) kwa nyakati tofauti.

Lakini pili, mara baada ya kupata uhuru na hatimaye kuungana kwa pande zote mbili, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa mwanachama wa Jumuiya ya Madola ambayo ina wanachama 56 duniani huku Mkuu wa Jumuiya hiyo akiwa Malkia Elizabeth II.

Kufuatia kufariki kwa Malkia Elizabeth II Mkuu wa Jumuiya hiyo sasa atakuwa Mfalme Charles III.

Jumuiya ya Madola ina utaratibu wake wa kufanya mahusiano na miongoni mwa hayo ni utaratibu wa misiba.

Ndiyo maana tumeona kuwa taarifa ya kufariki kwa Malkia Elizabeth II ilianzia kwa Waziri Mkuu wa Uingereza Liz Truss kupokea taarifa ya siri (London Bridge is Down) kutoka Balmoral kuwa kisha taarifa ile ikasambazwa kwa nchi 15 ambazo zipo chini ya milki Uingereza kisha taarifa ile ikasambazwa kwa nchi 56 wanachama wa Jumuiya ya Madola na baadae taarifa ikaenda BBC na kusambazwa kwa nchi nyingine zilizobaki.

Hivyo basi, kwa mujibu wa utaratibu wa Uingereza nchi za Jumuiya ya Madola zina nafasi ya pekee katika kupokea taarifa kuliko nchi nyingine kama vile Marekani, China, Ufaransa, Ujerumani na Italy licha ya ukubwa wao wa kiuchumi ambazo si wanachama.

Na katika kuonesha hilo, nafasi ya kwanza ya kutoa salamu za rambirambi iliwekwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambapo alifika kwenye makazi ya Balozi wa Uingereza na kutoa salamu zake za rambirambi kufuatia msiba huo mkubwa kwa waingereza.

Huu ni utaratibu wa Waingereza na pia ni sehemu ya utaratibu wa nchi za Jumuiya ya Madola.

Diplomasia ina utamaduni wa ‘reciprocity’ na hapa ndipo panapoanzia pia sababu za maombolezo ya siku tano.

Reciprocity kwa Kiswahili kisicho rasmi ni kurejesha ama kurudishia kile alichokufanyia mwenzako kwa kumfanyia kama vile au zaidi ya vile alivyokufanyia kwa nia njema.

Kufanya kwa nia mbaya huitwa retaliation.

Kwa muktadha huo, Serikali ya Tanzania kutoa siku tano za maombolezo ya kitaifa ni kurejesha au kulipa (reciprocate) kile ambacho Uingereza imekifanya kwa mwanachama wake wa Jumuiya ya Madola (Tanzania) kwa kupitia taarifa ya kifo cha Malkia Elizabeth II kama ulivyoeleza utaratibu wa utoaji taarifa za kifo ulivyofanyika.

Jambo jengine ambalo nalo ni muhimu kufahamu ni kuwa Tanzania inatekeleza sera ya Diplomasia ya Uchumi ambayo inaelekeza kwamba chochote ambacho serikali itakifanya kwenye uhusiano wa kimataifa kinapaswa kizingatie maslahi ya kiuchumi ya Tanzania.

Mkakati huu unalenga kuifanya diplomasia ya uchumi kipaumbele (prioritizing economic diplomacy) cha nchi ambapo inaweka bayana kwamba Tanzania itafungamanisha masuala ya uchumi katika kila jambo kiasi kwamba ahadi za kisiasa kama vile usuluhishi wa migogoro, kukuza haki za binadamu na mengineyo (ikiwemo msiba kama huu wa Malkia Elizabeth II) yatatazamwa kama mazingira wezeshi (ya kuvutia) wawekezaji kwa ushirikiano wa uchumi na maendeleo.

Hivyo basi, maombolezo ya siku tano ni sehemu ya mkakati wa utekelezaji wa sera ya Diplomasia ya Uchumi yakiwa yanalenga kuonesha mshikamano na nchi ya Uingereza. Labda hapa swali lingekuwa kwa nini Uingereza?

Jawabu ni kwamba Uingereza ni moja kati ya nchi zinazoongoza kwa uwekezaji mkubwa nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa ripoti za uwekezaji, nchi zinazoongoza kwa uwekezaji Tanzania ni China, India, Kenya, Uingereza, Mauritius, Oman, Umoja wa Falme za Kiarabu, Canada, Marekani, Uholanzi, Afrika Kusini na Ujerumani.

Soma: https://www.tanzaniainvest.com/fdi au www.twitter.com/tanzaniainvest

Kwa maana nyingine ni kwamba Uingereza ni mbia wa mkubwa wa maendeleo ya Tanzania kutokana na uwekezaji mkubwa iliyofanya nchini Tanzania.

Kwa kuzingatia sera ya Diplomasia ya Uchumi ambayo inaelekeza serikali kuweka mazingira wezeshi ya kuwavutia wawekezaji kitendo cha serikali kuweka siku tano za maombolezo ni sehemu ya kutambua mchango wa Uingereza katika maendeleo ya Tanzania na hivyo Waingereza waliopo Tanzania wanaihisi thamani waliyopewa mioyoni mwao.

Tukumbuke chochote kinachofanywa katika diplomasia hulenga kuathiri mioyo na fikra za wananchi wa nchi husika hivyo hili nalo kwa namna moja ama nyingine limeathiri mioyo ya Waingereza kwa kuzingatia thamani waliyopewa huku Tanzania ikilitazama hilo kama sehemu ya kuimarisha diplomasia ya uchumi na kuvutia wawekezaji zaidi.

Kwa hayo machache nadhani tumeelewa sababu za serikali kutangaza siku tano za maombolezo.

Abbas Mwalimu
(Facebook|Instagram|Twitter|Clubhouse).

+255 719 258 484

Uwanja wa Diplomasia

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %