Na Mwandishi wetu
Napoli, Italy
Serikali ya awamu ya sita yaendelea kutoa majawabu ya changamoto za Diaspora
Moja ya Changamoto kubwa kwa Watanzania wanaoishi nje ni hati za safari yaani Passport. Kutokana na wengi kuwa ughaibuni kwa miaka mingi kumekuwa na tatizo la kutokutimia kwa vigezo vilivyowekwa kwa ajili ya kuomba pasi mpya za KIELEKTRONIKI.
Baada ya kilio Cha Muda mrefu, Cha Watanzania waliopo kwenye eneo la nchi takriban SITA zinazowakilishwa na Ubalozi wa Tanzania uliopo Rome Italy, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mjini Rome Mh Mahamoud Thabit Kombo ameweza kukata kiu ya Watanzania hao kwa kufanikiwa Kupitia serikali, kuletwa kwa Maofisa wa vitengo maalumu kutoka makao makuu ya uhamiaji Zanzibar na Tanzania Bara.
Zoezi hilo la mchakato wa kusikiliza na kupokea maombi ya Watanzania waliojitokeza kuomba pasi ya KIELEKTRONIKI yalienda sambamba na uchukuaji picha na Alama za vidole kwa waombaji. Maofisa wa Uhamiaji wakiongozana na ofisa wa kitengo hicho kutoka Ubalozi wa Tanzania Ndugu Nenmbuka, walianza zoezi hilo mjini Athens Greece ambapo waliweza kupokea Maombi zaudi ya mia moja wakiwemo watoto wa kitanzania waliozaliwa ughaibuni. Nchini Ugiriki zoezi lilifanyika kwa siku mbili mfululizo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania nchini Ugiriki Ndugu Kayu Ligopora alitoa shukran nyingi kwa maofisa wa uhamiaji Pamoja na Ubalozi kwa kuweza kumalizia kero hiyo ilikuwepo kwa miaka mingi. Mwenyekiti kwa kipekee alimshukuru Balozi Mahamoud Thabit Kombo kwa kuweza kupatia majawabu ya changamoto za Diaspora.
Baada ya kuhitimisha huko Ugiriki zoezi lilihamia mjini Napoli Italy siku ya jumatatu ya tarehe 23/01/2023 ambapo ndipo kuna idadi kubwa ya Watanzania wanaoishi nchini Italy.
Zoezi lilianza rasmi mjini Napoli kwa kufunguliwa Rasmi na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Italy.
Mh Mahamoud Thabit Kombo, alianza kwa kuwashukuru maofisa wa uhamiaji Pamoja na Ndugu Nenmbuka kwa Kazi nzuri waliyofanya nchini Ugiriki na wanayoendelea nayo mjini Napoli. Katika pongezi na shukran Mh Balozi pia alimpongeza Ndugu Erasmus Pindu Luhoyo mfanyakazi wa Ubalozi kitengo Cha Visa na Passport kwa Kazi nzuri anayofanya .
Balozi aliwashukuru viongozi wa Jumuiya ya Watanzania Napoli Kupitia Mwenyekiti wake Dada Judith Joseph, kwa kushirikiana vyema na Ubalozi kuandaa zoezi hilo na hasa kwa msaada Mkubwa kwa Watanzania waliokuwa na changamoto mbalimbali .
Mwenyekiti wa Jumuiya Ndugu Judith Joseph alitumia nafasi ya uwepo wa Mh Balozi kwa Kumshukuru kwa jitihada kubwa alizozifanya kufanikisha ujio wa maofisa wa uhamiaji, lakini pia Mwenyekiti kwa niaba ya Watanzania wanaoishi Napoli alituma salaamu za shukran kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr Samia Saluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali Diaspora na kupatia ufumbuzi wa changamoto zao ikiwemo suala la uraia pacha na Hadhi Maalumu na hili la hati mpya za safari. Katika shukran hizo mwenyekiti pia alichomekea suala la vitambulisho vya Nida, kuwa lipewe umuhimu Mkubwa kwa Diaspora maana kwa sasa imekuwa ni kikwazo kikubwa kwa Watanzania wanaoishi nje wanapotaka huduma mbalimbali ikiwemo ya uwekezaji nyumbani.
Zoezi lilikamilika siku ya jana tarehe 24/01/2023 usiku, sambamba na kukamilika huko Watanzania mbalimbali walitoa ya moyoni kwa Kumshukuru Balozi wao, maofisa wa uhamiaji na kwa umuhimu wa kipekee Watanzania hao walituma salamu za shukran na pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Maofisa wa Uhamiaji wataendelea na zoezi hilo siku ya Alhamisi Mjini Rome ambapo itakuwa ndio wanahitimisha ziara Yao hiyo ya Kazi.