0 0
Read Time:4 Minute, 54 Second

WUยฎ MEDIA

Na Abbas Mwalimu

(0719258484)

Jumamosi tarehe 08 Aprili 2023.

Ripoti ya CAG ndiyo jambo lililotawala vichwa vingi vya habari na mitandao ya kijamii kwa sasa.

Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba madudu yaliyoainishwa katika ripoti hiyo yanagusa maisha ya wananchi wengi Tanzania.

Aidha, ripoti ya CAG imeendelea kuonesha ubadhilifu mkubwa wa fedha za umma unaofanywa na watanzania wenzetu walioaminiwa kwenye nafasi mbalimbali za uongozi kwa miaka mingi sasa, jambo linalozidisha chuki na hasira miongoni mwa wananchi.

Kutokana na hali hiyo, madudu yaliyobainishwa katika ripoti ya CAG yanaakisi kitisho cha kiusalama (security threat) ambacho kinahitaji kufanyiwa kazi kwa haraka.

Kwa bahati mbaya, inaweza isieleweke sana miongoni mwa wengi kuhusanisha madudu yaliyoibuliwa na CAG na kitisho kwa usalama wa taifa.

Hivyo, ni vema kufahamu tafsiri ya maneno ‘usalama’ na ‘usalama wa taifa’ ili tuweze kuelewa athari za kufumbia macho madudu haya.

Usalama ni hali ya kujisikia kuwa huru kutoka kwenye madhara, hofu, wasiwasi, ukandamizaji, umasikini, njaa n.k (Afolabi, 2015).

Kimsingi, usalama ni uhai wa tunu za taifa (Bodunde na wenzake, 2014) hivyo, ni ulinzi wa misingi na miiko ya maadili ya nchi ambayo inaakisi utu, umoja, mshikamano, uzalendo, uwajibikaji na uadilifu.

Kwa mantiki hiyo, usalama wa taifa ni uwekaji wa nchi katika hali ya usalama kwa ujumla (Holmes, 2015:4).

Hivyo, uwajibikaji na uadilifu ni masuala yanayogusa usalama wa taifa moja kwa moja kutokana na matendo ya ubadhilifu yaliyoibuliwa na CAG.

Vilevile, ubadhilifu uliooneshwa katika ripoti ya CAG unatokana na mambo manne kati ya mengi; mambo haya ni, rushwa, kukosa uzalendo, uadilifu na uwajibikaji.

Sarah Chayes katika kitabu chake ‘Thieves of State: Why Corruption Threatens Global Security,’ cha mwaka 2015 anasema, suala la rushwa si kitisho cha usalama kwa nchi nyingine tu, bali hata kwa Marekani na dunia kwa ujumla.

Vivyo hivyo, kukosekana kwa uadilifu, uzalendo na uwajibikaji ni kitisho cha usalama kwa dunia nzima, na kipekee kwa Tanzania.

Kadhalika, von Soest na De Juan (2018) katika makala yao ‘Dealing with New Security Threats in Africa’, wamebainisha changamoto zinazolikumba bara la Afrika na kupelekea kuwepo kwa vitisho vya kiusalama vinavyosababisha ukosefu wa amani.

Von Soest na De Juan walieleza kwa kingereza; ‘The primary threats to peace and security in Africa are well known: poverty, weak state institutions, and weak governance (2018:4).

Pia, African Centre for Strategic Studies (2018) walikuwa na mtazamo huo huo katika chapisho lao lililopewa jina ‘Africaโ€™s Contemporary Security Challenges’.

Halikadhalika, The Nordic Africa Institute (2018) katika ripoti yao yenye kichwa cha habari ‘Peace and Security Challenges in Southern Africa: Governance Deficits and Lacklustre Regional Conflict Management,’ wamebainisha kuwa, katika kipindi cha miaka 10 iliyopita nchi za SADC zimekabiliwa na vitisho vya kiusalama vilivyotokana na mambo mbalimbali yakiwemo, kukosekana kwa uwajibikaji serikalini (government unaccountability) na utumiaji mbaya wa rasilimali za nchi (abuse of state resources). Rejea NAI (2018:4).

Hivyo, madudu yaliyoibuliwa na CAG yanatokana na kukosekana kwa uwajibikaji wa baadhi ya viongozi waliopewa dhamana na utumiaji mbaya wa rasilimali za nchi, kwa lengo la kujinufaisha wao na familia zao.

Mbaya zaidi, inashangaza kuona kwamba hata baada ya kuambiwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan “watupishe,” watu hawa wameendelea kukalia viti vyao na hivyo kuzidisha chuki na hasira miongoni mwa watanzania.

Ukaidi huu unaashiria hali ya kukosa uadilifu na uwajibikaji kulikopitiliza kwa watumishi hao na hivyo kuzidisha changamoto ya kiusalama.

Kinachojitokeza hapa ni baadhi wananchi kuendelea kubeba chuki, hasira na manung’uniko mioyoni mwao wakiamini kuwa baadhi ya watu wameamua kujimilikisha rasilimali za nchi huku wao wakiteseka, kama alivyobainisha Paul Collier na mwenzake Hoeffler katika nadharia yao ya ‘greed versus grievance’ au ‘ulafi dhidi ya manung’uniko’ ya mwaka 2000.

Mtazamo huo wa wananchi ukiendelea kwa muda mrefu huweza kusababisha kuripuka kuwa vurugu na kuleta changamoto kubwa kwenye usalama wa taifa kwa ujumla.

Je nini kifanywe na Serikali?

(i) Ni muhimu kwa serikali kuwachukulia hatua wale wote waliobainishwa kwenye ripoti ya CAG.

(ii) Serikali iyafanyie kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na CAG. Kwa sababu, mapendekezo mengi ya CAG katika ripoti mbalimbali yamekuwa na changamoto za kufanyiwa kazi.

Kwa mfano ripoti ya CAG ya mwaka wa fedha 2020/2021 imebainisha wazi kwa kusema:

‘Mapitio zaidi yalibaini kuwa, kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30 2021, kulikuwa na jumla ya mapendekezo 17,179 ya miaka iliyopita yalikuwa bado kutekelezwa.Kati ya hayo mapendekezo 5,290(31%) yalitekelezwa
kikamilifu, 6,032 (35%) yapo katika hatua ya utekelezaji, 3,548 (21%) hayajatekelezwa na 1,143 (6%) yalifutwa kutokana na kupitwa na wakati na mapendekezo 1,166 (7%) yalirudiwa.’

Aidha, katika ripoti ya CAG ya mwaka wa fedha 2021/2022 inaonesha kuwa, katika mapendekezo 102 yaliyotolewa kwa Ofisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI, mapendekezo 45 hayajatekelezwa, 15 yamerudiwa wakati 27 yakiwa yamefutwa kutokana na kupitwa na wakati (Rejea ukurasa wa 10 hadi wa 15 wa ripoti kuona mapendekezo yaliyotolewa kwa taasisi nyingine).

Instaajabisha kuona kwamba mapendekezo yanatolewa mpaka muda wake unaisha yakiwa hayajatekelezwa, je kuna uzalendo hapo?

Hali hii inaonesha wazi kuwa bado kuna ombwe kubwa la uwajibikaji na uadilifu kwa baadhi ya watendaji wa serikali na hivyo kukwamisha juhudi za Serikali.

(iii) Kuongeza ukaribu wa Bunge na Ofisi ya CAG. Kwa mfano, kwa Marekani, Ofisi ya CAG ni sehemu ya Bunge la nchi hiyo kama ilivyo kwa Australia na New Zealand kiasi kwamba zina uwezo wa kumuomba Waziri husika atoe maelezo juu ya ubadhilifu wa fedha mbele ya Bunge.

(iv) Kuundwa kwa Ofisi ya Taifa ya Kufuatilia Uwajibikaji (Government Accountability Office). Hii ni kutokana na ukweli kuwa Sheria Namba 13 ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995 iliyopelekea kuundwa kwa ,Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kukosa nguvu ya kuleta matokeo chanya katika Utawala Bora nchini.

Hivyo, katika zile ‘R nne’ za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuna haja ya kuitazama hii ‘R’ ya ‘Reforms’ au ‘Marekebisho’ ili kupatikane taasisi itakayokuwa imara zaidi ya ilivyo sasa.

Abbas Mwalimu
(Facebook|Instagram|Twitter|Clubhouse)

+255 719 258 484

Uwanja wa Diplomasia
(Facebook|WhatsApp)

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %