Na Mwandishi wetu, Napoli
Watanzania wanaoishi mkoa wa Campania katika miji ya Caserta na Napoli walikusanyika katika kanisa la Madonna Del Carmine jijini Napoli ambako kulifanyika sala na maombi kwa ajili ya marehemu Mashaka Salehe Omari.
Marehemu alifariki tarehe 20/04/2023 wakati akiwa hospitalini akipatiwa matibabu. Marehemu alibatizwa katika kanisa hilo mwaka 2012 na kuwa rasmi muumini wa Kristo.
Sala hiyo iliongozwa na Padre Paul ambae ni Mtanzania, hivyo sala na maombi yalifanyika katika lugha zote mbili. Padre Paul wakati akimzungumzia Marehemu ambae alitambulika kwa jina la Ubatizo kama Carmelo, alisema marehemu alikuwa mtu mkarimu na muaminifu sana kiasi alikuwa akipendwa na kila mtu kwenye maeneo aliyokuwa akiishi , Padre alieeleza hayo, mbele ya Mwakilishi wa balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini ambae alikuja kutoa salamu za ubalozi. “Carmelo alipeperusha bendera ya Tanzania kiasi cha kufundisha nidhamu nzuri kwa jamii ambayo ni utamaduni wetu watanzania, alikuwa hampiti mtu njiani bila kumsalimia,alisaidia wazee akutanapo nao njiani wakiwa na mizigo hasa watokapo kufanya manunuzi” alisema Padre.
Baada ya sala Padre alimkaribisha Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania in Campania PRESIDENTE Judith Joseph kutoa salamu za Watanzania walioshiriki kwa njia moja au nyingine kufanikisha na kukamilisha safari ya mwisho ya mwenzi wao. Mwenyekiti aliwashukuru wote kwa kuwa pamoja katika kipindi kigumu cha msiba, pia alimshukuru balozi wa Tanzania Mh. Mahmoud Thabit Kombo kwa kuendelea kuwajali watanzania na kutoa ushurikiano kwa viongozi wa jumuiya pindi wanapo hitaji, Mwenyekiti alitoa shukurani kwa ubalozi kwa ujumla pamoja na wawakilishi waliokuja kuhudhuria sala na maombi kanisani hapo. Kwa namna ya kipekee alimshukuru Padre Paul kwa kushirikiana na viongozi tangu wakati marehemu amelazwa kwa matibabu, sambamba nae pia alishukuru uonngozi wa Kanisa pamoja na jamaa wa karibu wa Carmelo ambao nao walitoa michango yao ya hali na mali.
Mwisho Kabla ya kufunga Maombi , Padre alimkaribisha Mh. Sigfred Nnembuka aliyebeba ujumbe mzito wa balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Pamoja na shukrani nyingi kwa watu wote walioshiriki pale kanisani , Mh. Balozi ametuma salamu ya kusisitiza umoja , ushirikiano na upendo baina ya watanzania na kuepuka kuweka makundi yasiyo na tija kwenye jamii. Balozi amewataka Watanzania kuwa mfano wa kuigwa kwani wanabeba bendera ya taifa huku nje. “alisema Mh. Nnembuka wakati akitoa salamu hizo kwa niaba ya Balozi”
Padre Paul nae alisisitiza kudumisha umoja baina ya Watanzania na kuacha fikra potofu zinazozua sintofahamu, aliwataka viongozi kuendelea kuweka kila jambo linalohusu jumuiya wazi kwa wanajumuiya. Amesema alipokea dhamana za marehemu wakati akiwa hospitalinu , hivyo pamoja na vitu vingine vya marehemu ataviweka katika maandishi ili viongozi waweze kubaki na kumbukumbu, na kuahidi kuwa pindi atakapopata safari Kwenda Tanzania atawakilisha dhamana hizo kwa familia yake. Padre alieleza kuwa alipokea kiasi cha michango kutoka kwa jamaa wa karibu wa marehemu hivyo atakabidhi kwa viongozi ili kuchangia taratibu na gharama za usafirishaji wa mwili wa marehemu Carmelo ( Mashaka Salehe Omari).
Padre alifunga sala kwa maombi na kuwatakia wote waende kwa amani.
Jumuiya ya Watanzania Rome iliwakilishwa na Mwenyekiti wake Ndugu Leonce Uwandameno ambaye aliongozana na Ujumbe wa Ubalozi
Mwili wa marehemu utaondoka Rome Italy kupitia Istanbul siku ya jumamosi 13/05/2023 na ndege ya shirika la Turkish na utafika Dar Es Salaam Tanzania tarehe 14/05/2023.