
Na Abbas Mwalimu (0719258484).

Alhamisi tarehe 27 Mei, 2021.
Tanzania ina nafasi kubwa sana ya kuwa dola/nchi kiranja/kiongozi Afrika endapo tutaamua kutumia nafasi ya lugha ya Kiswahili kama nyenzo ya ushawishi. Mtu anaweza kushangaa hili lakini tujiulize, tuliwezaje miaka ile ya 1960-1980 ambapo hata katika vikao vya Umoja wa Mataifa nchi nyingine zote za Afrika zilikuwa zikisubiri kusikia nini kitasemwa kutoka Tanzania kabla hazijazungumza? Huu ulikuwa ushawishi wa hali ya juu.
Tarehe 25 Mei, 2021 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, aliongoza kikao cha mabalozi wa Afrika katika kusheherekea siku ya Umoja wa Afrika na katika siku hii Waziri Mulamula alieleza kuwa lugha ya Kiswahili imepitishwa rasmi kutumika kama lugha ya mawasiliano katika mikutano rasmi ya Umoja wa Afrika.
Tukumbuke pia kuwa mwezi Machi mwaka huu 2021 Tanzania iliomba Kiswahili kitumike pia katika kuendeshea mikutano ya Mawaziri na Wakuu wa Nchi za SADC ili kukifanya kuwa lugha rasmi ya kuendeshea mikutano ya SADC. Hili lilifuatia mapendekezo ya Kamati Maalumu iliyopitisha mapendekezo hayo mwezi Agosti, 2019 katika mkutano wa Kilele wa SADC uliofanyika Dar es Salaam.
Kiswahili ni fursa adhimu kwa serikali, wafanyabiashara,wajasiriamali na wananchi wa kawaida katika kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika kiuchumi, kisiasa na kijamii Afrika na duniani kwa ujumla.
Kwa nini naamini hivi?
Kwa sababu mwaka 2013 wakati Umoja wa Afrika ukitimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1963 nchi za Afrika zilikuja na mpango wa maendeleo wa Afrika ujulikanao kama Ajenda 2063 ambayo inalenga kuliunganisha bara la Afrika katika nyanja zote: kijamii, kisiasa, kisayansi, kiuchumi, kibiashara na kiutamaduni.
Kutokana na mpango huu mkakati wa Afrika 2063 na utumikaji wa Kiswahili kama lugha ya mawasiliano utainufaisha sana Tanzania kuweza kuyafikia malengo yake ya kisera.
Ni wazi kuwa Kingereza ambacho bado kinaonekana kama lugha ya kikoloni hakiwezi kuinufaisha Tanzania kufikia malengo yake ya kisera. Na wala si kifaransa ambacho nchi pekee zinazongumza ni zile za kaskazini na Magharibi sambamba na DRC, Burundi na Rwanda. Kichina ambacho ndiyo kwanza kinaanza kufundishwa Afrika hakiwezi kabisa.
Kwa kutazama changamoto ya lugha nyingine tunaona kuwa ni wazi kuwa Kiswahili pekee ambacho kinaweza kutumika kuziunganisha nchi za Afrika na hili litainufaisha sana Tanzania kuongeza ushawishi katika maamuzi ya kisera na ya kimkakati ya Umoja wa Afrika. Na haya ndiyo yalikuwa mawazo, fikra na maono ya viongozi wetu waliotuachia Tanzania hii,Hayati Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Katika kuthibitsha hilo, Adebayo na wenzake katika kitabu chao Marginality and Crisis cha mwaka 2010 (2010:62) waliandika:
Kiswahili kimetambuliwa na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) kama lugha yenye kuleta umoja katika nyanja za maendeleo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kielimu, kisayansi na kiteknolojia.
Lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa lugha kubwa na kongwe duniani ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika uhusiano wa kidiplomasia kabla na baada ya Uhuru wa bara letu la Afrika.
Haya yamewekwa wazi na Adebayo na wenzake walipoeleza kuhusu mchango wa Kiswahili katika mahusiano, na ninawanukuu:
“Kihistoria, Kiswahili imekuwa lugha ya mawasiliano kwa jamii ya mwambao wa Pwani ya Afrika Mashariki tangu karne ya Kumi na nne. Ni lugha ambayo inazungumzwa na zaidi ya watu milioni mia moja ishirini katika eneo la Afrika Mashariki na Kati. (Adebayo na wenzake, 2010:64)
Ni lugha hii inayozungumzwa katika mataifa ya Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Kongo, Somalia, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Msumbiji, Zambia, Malawi, Zimbabwe na Afrika ya Kusini.
Kidiplomasia ukuaji wa ushirikiano kati ya ukanda wa Afrika Mashariki na Mashariki ya Mbali pamoja na Mashariki ya Kati ulitegemea ukuaji wa Kiswahili.
Hivyo basi, Kiswahili kimetumika kama kiungo kati ya wafanyabiashara wa nje na wa ndani.
Kwa upande mwingine lugha ya Kiswahili ilitumika kama lugha ya ukombozi wa bara la Afrika.
Kiswahili ndiyo lugha iliyotumiwa na chama cha TANU kuwaunganisha na kufanikisha ukombozi na uhuru wa Tanganyika. Lakini ilikuwa pia lugha ya ukombozi na mapinduzi Zanzibar. Na ndiyo lugha iliyoziunganisha Tanganyika na Zanzibar kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili, 1964.
Lugha ya Kiswahili ilitumika kama lugha ya ukombozi wa nchi za Kusini na Kaskazini mwa Afrika. Mashujaa wa FRELIMO,PAC,ANC,MPLA, POLISARIO na ZANU-PF walipokea mafunzo yao na msaada wa ukombozi kwa mchango wa Kiswahili kama lugha iliyowaunganisha.
Hivyo basi hatua za awali za utekelezaji wa sera ya kwanza ya mambo ya nje lugha ya Kiswahili ilikuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wake, hususan kwenye eneo la ukombozi.
Mbali na hayo Kiswahili kilitumika pia kama lugha ya Ukombozi wa bara zima la Afrika huku Tanzania ikiwa ndiyo kitovu cha harakati hizo chini ya Kamati ya Ukombozi iliyoongozwa na Hatayi Brigedia Jenerali Hashim Mbita.
Hili lilielezwa kwa kina na Khatib (2004) akielezea uwezo wa lugha ya Kiswahili kama lugha ya ukombozi wa waafrika.
Khatib alieleza kwa mawanda mapana namna nasaba ya Abushiri ilivyoweza kutumia Kiswahili kupambana na uvamizi wa waarabu katika karne ya Kumi na Saba.
Kwa umuhimu wa kipekee, Kiswahili kilitumika pia kama lugha ya ukombozi katika nchi za Msumbiji, Zimbabwe na Afrika ya Kusini (wakati wa ubaguzi wa rangi), Uganda, Rwanda, Burundi, Afrika ya Kati na Kongo.
Kiswahili pia kinatumika kama lugha ya utafiti katika vyuo vikuu mbalimbali vya Afrika, Ulaya, Asia, na Marekani.
Kutokana na kazi hizo za Kiswahili taasisi mbalimbali za kimataifa husaidia tafiti katika elimu ya Kiswahili.
Hizi ni miongoni mwa sababu zilizofanya Sekretarieti ya Umoja wa Afrika (AU) kukichagua Kiswahili kama lugha yake rasmi ya kazi (Adebayo na wenzake, 2010:65).
Tunapozungumzia utaifa na demokrasia leo hii katika Afrika tunapaswa kufahamu kuwa msingi wake ni lugha ya Kiswahili.
Katika kuthibitisha hili Muthwii na Kioko (2004) wameandika:
Lugha ni chombo muhimu katika kuhanikiza utaifa. Kwa msingi huo ina umuhimu katika kuanzishwa kwa demokrasia ya kweli na usawa.
Harakati mbalimbali zilifanyika na zinaendelea kufanyika ili kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya mawasiliano barani Afrika kama ambavyo Muthwili na Kioko (2004) walivyobainisha:
Mwaka 1958 Baraza la Pili la Waandishi na Wachoraji Weusi lilipitisha Azimio la kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya mawasiliano kwa bara zima la Afrika. Nina hakika jambo hili litatimia siku fulani lakini kunahitajika juhudi za dhati na utashi.









Uchambuzi umenigusa sana na endapo ushauri ulioutoa humu ndani kama mamlaka husika utalifanyia kazi utaleta tija kwa nchi.
1. Kuitambulisha Tanzania zaidi duniani
2. Kuongeza kasi ya sekta ya utalii na watalii
3. Itafungua ajira za moja kwa moja.
Kwa mfano
I. Uwepo wa tamasha maalum la kitaifa litaleta wageni wengi kama wenzetu Zanzibar na lile tamasha lao la sauti za busara
2. Vituo vya kufundisha Kiswahili duniani vitachochea ajira nyingi.
Tukichelewa kama Taifa kuyaona haya mapema wenzetu majirani wataitumia fursa hii.
Kongole kwako Abas Mwalimu kwa uchambuzi na maoni yako