
Berlin Germany
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshiriki kwa mafanikio maonyesho makubwa ya Utalii duniani (ITB-Berlin) yanayoendelea kwenye jiji la Berlin nchini Ujerumani.

Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye maonesho hayo umeongozwa na Mawaziri wawili ambao ni Mheshimiwa Mudrick Soragha(Mb), Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale kwa upande wa Zanzibar na Mheshimiwa Dunstan Kitandula (Mb), Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii kutoka Tanzania Bara.
Aidha, Bw. Arif Abbas Manji, Katibu Mtendaji wa Tume ya Utalii Zanzibar na Mheshimiwa Hassani Iddi Mwamweta, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani nao walishiriki maonesho hayo.

Zaidi ya makampuni 100 kutoka Tanzania bara na Zanzibar yameshiriki maonyesho hayo ambayo yamehudhuriwa na Makampuni ya Utalii zaidi ya 5800 kutoka mataifa zaidi ya 170 duniani kote.
Ujerumani ni soko muhimu kwa utalii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa mwaka 2024 zaidi ya watalii 95,000( elfu tisini na tano) wametembelea Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujionea vivutio mbalimbali.


















