
Sweden
Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Swahiba Mndeme, ameainisha vipaumbele vya utekelezaji wa majukumu yake katika kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na diaspora, kuvutia uwekezaji, kukuza biashara na kueneza lugha ya Kiswahili katika eneo lake la uwakilishi.
Amebainisha hayo tarehe 30 Mei 2026 alipokutana na Watanzania waishio Sweden katika Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania jijini Stockholm, ambapo pia aliwasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika mkutano huo, Balozi Swahiba amesema kuwa Diaspora ni rasilimali muhimu yenye ujuzi, maarifa na uzoefu inaweza kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania.
Aidha, aliwahimiza Watanzania hao kutumia nafasi na mitandao waliyonayo kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zilizopo nchini pamoja na vivutio vya utalii, hatua ambayo itasaidia kuongeza ushiriki wa diaspora katika kukuza uchumi wa Tanzania na kuitangaza nchi kimataifa.
Balozi Swahiba pia aliahidi kuendelea kukuza na kueneza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika eneo lake la uwakilishi kwa kuwezesha upatikanaji wa vitabu na vifaa vya kufundishia lugha hiyo. Alieleza kuwa Kiswahili ni sehemu muhimu ya utambulisho wa Taifa na nyenzo muhimu ya kuimarisha diplomasia ya utamaduni.
Katika majadiliano hayo, washiriki walijadili masuala mbalimbali yanayohusu diaspora ikiwemo Hadhi Maalum, sheria za mirathi na huduma za kikonseli. Balozi Swahiba aliwahimiza kuendelea kudumisha mshikamano na kuimarisha uratibu wao kupitia jukwaa la pamoja litakalowezesha ushiriki wenye tija zaidi katika shughuli za maendeleo ya Taifa.
Vilevile, Balozi Swahiba amewahimiza Diaspora kushiriki kikamilifu katika shughuli zitakazoratibiwa na Ubalozi, zikiwemo Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yatakayofanyika Julai 2026 na Serengeti Bonanza litakalofanyika Stockholm mwezi Agosti 2026.
Mbali na Sweden, Balozi Swahiba pia anaiwakilisha Tanzania katika nchi za Denmark, Norway, Finland, Iceland, Estonia, Latvia, Lithuania na Ukraine.












