
Dar Es Salaam TANZANIA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, ameshiriki katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya kuzaliwa kwa Mfalme Willem-Alexander wa Uholanzi, iliyofanyika katika makazi ya Balozi wa Uholanzi, jijini Dar es Salaam tarehe 24 Aprili,2025.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Kombo aliishukuru Uholanzi kwa mchango wake katika maendeleo ya Watanzania kupitia sekta za afya, kilimo, nishati, maji, elimu, mifumo ya kodi, ujasiriamali, utalii, na uwekezaji na alihaidi kukuza uhusiano na urafiki na nchi hiyo kwa manufaa ya wananchi wa pande zote.
“Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Uholanzi umejengwa kutokana na historia ya ushirikiano wa kirafiki uliojengwa na hayati Mfalme Bernhard wa Lippe-Biesterfeld na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Maadili waliyoamini pamoja yamekuwa msingi wa ushirikiano thabiti na wenye manufaa tunaouendeleza hadi leo,” alisisitiza Mheshimiwa Waziri Kombo.
Awali, Balozi wa Uholanzi nchini, Mhe. Wiebe de Boer, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa heshima ya ushiriki wake katika maadhimisho ya Siku ya Mfalme wa Uholanzi, na kuelezea dhamira ya Uholanzi ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania kwa lengo la kukuza ustawi wa wananchi wao na kujenga uchumi endelevu.
Uholanzi ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa wa kigeni nchini Tanzania, ikiwa na zaidi ya kampuni 100 za Kiholanzi zilizowekeza zaidi ya euro milioni 300 na kuunda ajira zipatazo 27,000, jambo linalothibitisha imani kubwa ya Uholanzi katika uchumi wa Tanzania.
Siku ya Mfalme” (King’s Day) huadhimishwa kuzaliwa kwa Mfalme wa Uholanzi, ambapo pia hutumia fursa hiyo kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Uholanzi na mataifa mengine ikiwemo Tanzania.









