
WU®Media
Antwerp Belgium
Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora na Fursa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Salvator Mbilinyi, ametoa wito kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi kuendeleza mshikamano na kuishi kwa upendo na waendelee kuitangaza vyema Tanzania kama taifa la amani.

Bw. Mbilinyi alitoa rai hiyo alipokutana na Watanzania waishio nchi mbalimbali za Ulaya waliojumuika jijini Antwerp, nchini Ubelgiji, katika Tamasha la Moira wa miguu la Serengeti (Serengeti Football Bonanza) lililofanyika tarehe 15–16 Agosti 2025.
Tamasha hilo liliandaliwa na Diaspora kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania Ubelgiji na kujumuisha timu 14 za mpira wa miguu kutoka mataifa mbalimbali, ambapo timu ya Kilimanjaro ya Sweden iliibuka mshindi.
Tamasha hilo pia lilitumika kama jukwaa la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwasilisha kwa diaspora taarifa kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana nyumbani, sambamba na kuwakutanisha na taasisi za huduma muhimu kama benki, uhamiaji, NIDA, na UTT-AMIS.
Aidha, Bw. Mbilinyi aliwashukuru Watanzania waishio nje ya nchi kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa kupitia sekta za afya, elimu, makazi, utalii pamoja na utumaji wa fedha nyumbani.
Alisisitiza pia umuhimu wa Watanzania waishio nje kujiandikisha katika Mfumo wa Usajiri wa Diaspora wa Tanzania (DDH), akieleza kuwa ukusanyaji wa takwimu sahihi ni nyenzo muhimu kwa Serikali katika kupanga mikakati ya maendeleo, ikiwemo maandalizi ya kuanzisha mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa diaspora.
Kadhalika, alihimiza diaspora kuendelea kuzingatia sheria za nchi wanazoishi, huku wakiendelea kulinda na kutetea maslahi ya Taifa lao la Tanzania.
















