
Dar Es Salaam TANZANIA
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa saalam za pongezi kwa kwa Jamhuri ya Watu wa China (PRC) kwa kuadhimisha miaka 76 tangu kuanzishwa kwa taifa hilo la pili kiuchumi duniani.

Salaam hizo kwa niaba ya serikali, zimewasilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo kwenye sherehe za kumbukizi zilizoandaliwa na Ubalozi wa China hapa nchini zilizofanyika tarehe 29 Septemba 2025 katika makazi ya Balozi wa nchi hiyo, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Waziri Kombo ameipongeza China kwa hatua ilizopiga katika maendeleo ya kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia ndani ya kipindi cha miaka 76, akibainisha kuwa taifa hilo limekuwa mfano wa kuigwa na mshirika muhimu wa maendeleo kwa bara la Afrika, hususan Tanzania.
“Uhusiano wa Tanzania na China ni wa kihistoria, uliojengwa katika misingi ya urafiki, uwazi, usawa na uheshimiana. Tunayo furaha kuona kuwa uhusiano huu unaendelea kukua na kuimarika kila siku, kupitia ushirikiano katika masuala ya kimataifa na maeneo mbalimbali kati ya pande mbili ikiwemo; utalii, biashara na uwekezaji, uchumi, elimu, kilimo, afya na miundombinu ya usafirishaji” alisema Waziri Kombo.
Vilevile Waziri Kombo alielezea kuhusu dhamira ya Tanzania ya kuendelea kushirikiana kwa karibu na China katika kutafuta fursa mpya za uwekezaji na biashara, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda misingi inayojenga mshikamano wa mataifa hayo mawili, ambayo imekuwa dira ya uhusiano imara uliodumu kwa kipindi cha takribani miongo sita.
Kwa upande wake Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian ameeleza kuwa licha ya changamoto za kisiasa na kiuchumi zinazo ikabaili dunia kwa sasa Taifa hilo limeendelea kuwa imara katika kusimamia ustawi wa kiuchumi na kisiasa wa wananchi wake na dunia kwa ujumla.
Mhe. Balozi Chen Mingjian pia alieleza kuhusu mikakati ya China ya kuendelea kukuza na kuimarisha ushirikiano na jumuiya ya kimataifa ikiwemo kuendelea kusimamia agenda za msingi zinazolenga kutela usawa na haki kwa watu wote ikiwemo suala la mabadiliko ya tabia nchi, usuluhishi wa migogoro na kupitia program na majukwa mbalimbali kama vile belt and road initiative na Jukuwaa la Ushirikiano wa China na Afrika (FOCAC).
Kadhalika, Mhe. Balozi Chen ameishukuru Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano na nchi yake, akieleza kwamba ushirikiano huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 60 baina ya nchi hizi mbili umejikita katika misingi ya kuheshimiana na maendeleo.
Hafla ya maadhimisho hayo imehudhuriwa na viongozi na watendaji wa ngazi mbalimbali kutoka serikalini na kisiasa, jumuiya ya wanadiplomasia na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa.









