
WAZIRI KOMBO AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KUSHIRIKI KATIKA MKUTANO WA PILI WA JUKWAA LA MAWAZIRI WA MAMBO YA NJE WA AFRIKA NA RUSSIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb) ameongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Russia uliofanyika Desemba 19 na 20, 2025, jijini Cairo, Misri.
Mkutano huo uliofanyika chini ya Wenyeviti Wenza ambao ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Mhe. Dkt. Badr Abdelatty na Waziri wa Mambo ya Nje wa Shirikisho la Urusi Mhe. Sergey Lavrov umetoa nafasi kwa nchi za Afrika na Russia kujadiliana na kukubaliana masuala muhimu yanayogusa maslahi ya pamoja katika nchi zao na katika Umoja wa Mataifa, na Mashirika yake.
Mawaziri wa Afrika na Russia wamesisitiza umuhimu wa Umoja wa Mataifa na Mashirika yaliyo chini yake, ikiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufanyiwa marekebisho ili kuongeza uwakilishi wa Afrika, kuimarisha uwajibikaji na ufanisi, kuwa na mfumo wa biashara duniani unaozingatia usawa, na kutoa nafasi sawa kwa kila nchi kushiriki kwa uhuru katika majadiliano na maamuzi muhimu yanayoigusa dunia.
Katika Mkutano huo Mhe. Waziri Kombo alizungumzia uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo, na maeneo ya kimkakati ya ushirikiano yanayoendelea kutekelezwa kati ya Tanzania na Russia.
Alisisitiza kuwa ushirikiano wa muda mrefu kati ya Russia na mataifa ya Afrika, ulioanza kabla na wakati wa mapambano dhidi ya ukoloni, hauna budi kuendelezwa na upewe kipaumbele zaidi katika kuongeza ushirikiano wa kiuchumi, hususan katika sekta za kimkakati za miundombinu na usafirishaji, nishati na nishati mbadala, teknolojia, TEHAMA, na afya.
Aidha aliongeza kuwa ushirikiano ulioimarishwa katika sekta hizi utasaidia juhudi za Afrika za kupanua Uchumi wake.















