0 0
Read Time:7 Minute, 13 Second

Na Abbas Mwalimu (0719258484).

Jumamosi tarehe 28 Agosti, 2021.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesikitishwa na uamuzi wa Serikali ya Denmark kuamua kufunga shughuli za Ubalozi wake nchini Tanzania pindi ifikapo mwaka 2024.

Katika maelezo yake aliyoyatoa kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula wakati wa mazungumzo kwa njia ya mtandao Ijumaa tarehe 27 Agosti, 2021, Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Denmark Mhe. Flemming Moller Mortensen alieleza kuwa Denmark katika mkakati wake mpya nchi ya Denmark itajielekeza katika kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na nchi zenye machafuko na migogoro. Mheshimiwa Mortensen alisema:

“…We have decided to close our Embassy in Dar es Salaam during 2024…We look to fragility and we look where it seems like its most needed…and some regions are really fragile…”

Mheshimiwa Mortensen amegusia pia suala la mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula alieleza kusikitishwa kwake na uamuzi huo lakini anatarajia Denmark itaendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali. Mheshimiwa Balozi. Mulamula alisema:

“Tumesikitishwa sana na hatua hiyo iliyofikiwa na Denmark lakini tunaamini kwamba tutaendelea na majadiliano kuweza kujua kwamba tutaimarishaje uhusiano wetu pamoja na kwamba Waziri huyo wa Denmark amesisitiza kwamba wataendelea kushirikiana na sisi kupitia Umoja wa Europe na Umoja wa Mataifa…”

Waziri Balozi Mulamula alisisitiza kuwa Wizara itaenda kutafakari maana ya uamuzi huo katika mahusiano ya kimataifa.

Licha ya taarifa iliyotolewa na Serikali kupitia Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Bwana Emmanuel Buhohela lakini bado wadau wengi wamekuwa wakijiuliza, kweli Denmark haijavunja rasmi mahusiano na Tanzania?

Makala hii inajielekeza katika kulitazama hilo kwa mujibu wa Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 unaohusu Mahusiano ya Kidiplomasia kwa Kingereza, Vienna Convention on Diplomatic Relations of 1961 kwa kifupi VDCR1961.

Ibara ya 43 ya Mkataba huu inaeleza kama ifuatavyo:

The function of a diplomatic agent comes to an end, inter alia:

(a) On notification by the sending State to the receiving State that the function of the diplomatic agent has come to an end;

(b) On notification by the receiving State to the sending State that, in accordance with paragraph 2 of
article 9, it refuses to recognize the diplomatic agent as a member of the mission.

Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi ni kwamba kuna mazingira ya namna mbili ambayo huweza kupelekea shughuli za Ubalozi kufikia ukomo. Ibara imetaja namna mbili lakini kwa muktadha wa kujengeana uelewa nitaitazama namna ya kwanza ambayo kwa tafsiri yangu inatafsirika kama ifuatavyo:

‘Pindi Nchi iliyotuma Ubalozi/iliyomtuma Balozi itakapoijulisha Nchi iliyopokea Ubalozi/iliyompokea Balozi kwamba shughuli za uwakilishi wa kibalozi zimefika tamati.’

Hivyo Denmark imezingatia ibara hii ya 43 kuitaarifu Tanzania kuwa ifikapo mwaka 2024 itafunga Ubalozi wake uliopo Dar es Salaam.

Kimsingi shughuli hizi za uwakilishi wa kibalozi ambazo Denmark itaenda kuzifunga mwaka 2024 zimeelezwa katika ibara ya 3 ya Mkataba huo wa Vienna ambazo ni kuiwakilisha nchi iliyomtuma Balozi katika nchi iliyompokea, kulinda maslahi ya Nchi iliyomtuma Balozi ndani ya Nchi iliyompokea, sambamba na maslahi ya raia wake kwa kuzingatia wigo uliowekwa na sheria za Kimataifa, kuingia mazungumzo na Nchi iliyopokea Uwakilishi wa Kibalozi, kuenenda na mazingira ya kisheria yaliyomo katika nchi husika na kutoa taarifa ya kinachojiri kwa Serikali za nchi zao na kuimarisha mahusiano ya kirafiki baina ya Nchi iliyopokea Ubalozi/Balozi na ile iliyotuma na kukuza mahusiano yao ya kiuchumi, kiutamaduni na kisayansi.

Kwa kutazama shughuli hizo tano zilizoainishwa na Mkataba wa Vienna tunaona kwamba shughuli nne kati ya hizo tano zilizoelezwa kwa mujibu wa Mkataba ndizo zitakazoathirika na kufungwa kwa shughuli za ubalozi wa Denmark hapa nchini lakini suala la kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizi na kukuza maendeleo ya kiuchumi, kiutamaduni na kisayansi bado zitaendelea kufanyika kutokana na kwamba shughuli hizo hazihitaji uwakilishi wa moja kwa moja ama physical representation wa Denmark nchini.

Ndiyo maana Waziri Mortensen aliitoa hofu Tanzania kuwa Denmark itaendelea kushirikiana na Tanzania kupitia Uwakilishi wa Umoja wa Ulaya uliopo hapa nchini.

Zipo sababu zinazopelekea Ubalozi kufungwa au kusitisha shughuli zake, sababu hizi ni kama vile, kukamilika kwa malengo yaliyopelekea kufunguliwa kwa ubalozi husika kwa mfano Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) hufunga balozi zake pindi shughuli ya kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi inapokamilika, lakini pia kutokea kwa mgogoro au vita baina ya nchi husika navyo huweza kusababisha kufungwa kwa ubalozi.

Sasa tujiulize, kuna mgogoro au vita baina ya Tanzania na Denmark? Jibu ni hapana!

Lakini tukingalia kukamilika kwa malengo ya Denmark kuanzisha mahusiano na Tanzania mwaka 1963 tunaona kuwa kuna mantiki kwa sababu tayari Tanzania imeshaingia uchumi wa kipato cha kati hivyo huenda Denmark inaona kuna haja ya kuzisaidia nchi nyingine zenye uhitaji zaidi.

Na katika kudhirisha hilo Waziri Mortensen amemhakikishia Waziri Mulamula kuwa Denmark itaendelea kutekeleza makubaliano ya ufadhili yaliyokwishafanyika kwa Tanzania na pia Denmark itaendelea kuunga mkono jitihada za kuimarisha biashara, ukuaji wa uchumi, demokrasia na sekta binafsi.

Kwa kutazama majukumu ya Balozi yaliyoainishwa kwenye Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 tunaona kuwa majukumu haya yote yanaweza kutekelezwa pasipo kuwa na uwakilishi wa moja kwa moja nchini Tanzania.

Lakini kubwa pia hapa ni kujiuliza, ni kwa kiasi gani kauli za Waziri Mortensen zina uhalisia?

Waziri Mortensen alieleza kuwa Denmark itajielekeza zaidi katika kutekeleza Mkakati wake unaokwenda kwa jina la “The World We Share”-Denmark’s Strategy for Development Cooperation. Mkakati huu unalenga kuhakikisha kuwa Denmark itaendana na Malengo 17 Endelevu ya Umoja wa Mataifa (UNSDGs) yaliyofikiwa mwaka 2015 ambayo yanaelekeza Dunia kuwa na Kesho Endelevu kwa Wote kufikia mwaka 2030.

Sambamba na hilo, katika Mkakati huo Denmark inajielekeza pia kutekeleza kikamilifu Mkataba wa Kupambana na Mabadiliko ya Tabianchi uliofikiwa na nchi 196 jijini Paris, Ufaransa mwaka 2015 katika mkutano wa 21 (COP21) wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC).

Kwa mujibu wa Mkakati huo uliotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Denmark mwezi Agosti, 2021 unaeleza zaidi kuwa:

Denmark itatumia Mkakati huo kuzuia na kupambana na umasikini, kukosekana kwa usawa, migogoro na watu kulazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita sambamba na kutatua uhamiaji usio rasmi.

Mbali na hayo Mkakati huo wa Denmark unaeleza kuwa nchi hiyo itaongoza mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, kukuza misingi ya demokrasia na haki za binadamu, kupigania usawa wa kijinsia, kulinda haki za kinamama na wasichana pamoja na kulinda makundi yaliyotengwa (marginalised).

Denmark imesisitiza katika Mkakati huo kwa kuwa itaelekeza juhudi zake kule ambapo kuna mahitaji makubwa na kwamba nchi hiyo ingependa kufanya mahusiano na nchi ambazo itazichagua kwa umakini sana ambapo mahitaji na changamoto ni kubwa mno. Lakini pia itaendeleza mahusiano na nchi nyingine kupitia Umoja wa Ulaya.

‘Our efforts will focus on where the needs are greatest…We wish to form partnerships with carefully selected partner countries where the needs and challenges are greatest. A focused engagement through the EU will equally widen Denmark’s reach across developing countries’ (MFAD, 2021).

Kwa kuzingatia Mkakati huo wa Denmark tunaona kuwa bado Denmark itaendeleza mahusiano na Tanzania hasa kupitia Umoja wa Ulaya kama ambavyo Waziri Mortensen alieleza.

Lakini pia dunia ya sasa imebadilika, nchi nyingi zilizoendelea zinajielekeza kwenye Diplomasia ya Dijitali (Digital Diplomacy) ambapo kuna baadhi ya nchi sasa zinajielekeza kuwa na mahusiano ya kidijitali na nchi nyingine pasina kuwa na mahusiano ya moja kwa moja (physical representation).

Nchi ya Marekani ilifungua Ubalozi wa Kimtandao (Virtual Embassy) jijini Tehran, Iran mwezi Desemba mwaka 2011 ambao inautumia kufanya mahusiano na watu wa nchi hiyo licha ya kwamba mahusiano ya moja kwa moja kati ya nchi hizo yalivunjika mwaka 1979 kufuatia kuibuka kwa mgogoro baina ya Marekani na Iran mara baada ya Mapinduzi yaliyoutoa madarakani kwa utawala wa Shah.

Lakini pia tangu nchi ya Uingereza ilipoanzisha Ofisi ya Diplomasia Dijitali katika Serikali yake nchi nyingine kama Sweden, Ufaransa na Poland zimejielekeza katika kutumia diplomasia ya dijitali. Haya yamebainishwa na Bjola na Holmes katika andiko lao la mwaka 2015.

Denmark ni sehemu ya nchi za Nordic kama ilivyo Sweden ambayo imejielekeza katika diplomasia ya dijitali, je hatuoni kuwa huu ni mwelekeo wa nchi za Nordic kupunguza gharama za kuweka Ubalozi wa moja kwa moja (physical representation) na hivyo kujielekeza kwenye diplomasia ya dijitali?

Nadhani ndiyo maana Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula alimalizia kwa kusema:

“Wizara itaenda kutafakari maana ya uamuzi huo katika mahusiano ya Kimataifa.” Mwisho wa kunukuu.

Hivyo kimsingi mahusiano baina ya Tanzania na Sweden hayajavunjika kwa sababu hakuna hata sababu moja miongoni mwa sababu zinazopelekea kuvunjika kwa mahusiano inayothitisha hilo lakini tunaona kuna sababu maalumu za Denmark kufunga shughuli za ubalozi kwa kuzingatia utekelezaji wa Mkakati wa nchi hiyo uliotolewa mwezi Agosti, 2021.

Wenu:

Abbas Mwalimu (Facebook|Instagram|Twitter).

+255 719 258 484

Uwanja wa Diplomasia (Facebook|WhatsApp).

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %