Na Dr Yahya Msangi
Kuna wengi hawakuwepo enzi ya Mwalimu. Hawakuona alivyoweza kudhibiti majizi. Mwalimu aliwapa wafanyakazi na vyama vyao nguvu ya kuingilia wanapoona wakubwa wao wanafakamia mali ya umma. Ilikuwa kupitia mabaraza ya wafanyakazi. Kupitia mabaraza haya wafanyakazi walifanikiwa kuzima majaribio mengi ya wizi wa mali za umma. Hawakuweza kuzuia 100% lakini walifanikiwa sana.
Hakuna kitu wakubwa walikichukia kama yale mabaraza ya wafanyakazi! Na Nyerere aliyaweka mpaka kwenye mashirika binafsi! Waliyachukia sana maana yalizuia utoroshwaji fedha kwenda nje. Mabaraza yale yalipewa nguvu ya kisheria kupitia sheria iliyoitwa SHERIA YA USALAMA KAZINI YA MWAKA 1962 (Security of Employment Act of 1962). Sheria hii iliigwa toka China. Mabeberu waliichukia mno. Ukaundwa mikakati kuua huu utaratibu. Mwanya ukapatikana lilipovunjwa Azimio la Arusha na kuletwa Azimio la Zanzibar. Moja ya maazimio kule Zanzibar ilikuwa kuvunja mabaraza ya wafanyakazi kwa kisingizio kuwa yanaenda kinyume na utandawazi (utandawizi) aka globalization.
Haraka ikaundwa tume ya kurekebisha sheria! Wakaanza na sheria za kazi! Wala hawakugusa sheria zote za kazi isipokuwa île ya Usalama Kazini! Wakahakikisha mabaraza ya wafanyakazi hayana tena nguvu ya kisheria! Viongozi wakapewa mamlaka kamili kuamua mapato na matumizi ya taasisi wanazoziongoza. Wizi ukaanza na ukapanda daraja kuwa ufisadi!
Mpaka kuja kuingia marehemu JPM ikamlazimu yéyé mwenyewe ndio akamate mafisadi na kuyatumbua! Baada ya yéyé kufariki hâta hajazikwa ufisadi ukaanza upyaaa (shahidi Mama SAMIA). Hili ni tatizo la kumuachia mtu mmoja peke yake ndio awe mkamata mafisadi!
Akiondoka au asipokuwepo ni balaa! Hivi sasa ni kama Waziri Mkuu katwaa jukumu la kukamata mafisadi na wazembe. Watu wanashangiliaaaa!
Ukiwa hufikiri utadhani dawa ya ufisadi imepatikana. Hebu jiulize hivi mpaka DART iko hoi vile Mkuu wa Mkoa na MA DC au mameya ambao DART iko eneo lao la kazi walikuwa wapi? Siku île RC alikuwepo lakini utadhani naye ni mgeni! Waziri Mkuu kabla ya kutumbua wale jamaa angemuuliza RC au DC “nyie kazi yenu nini kama hamkuweza kuona kuwa DART inakufa”?
Wakati tukifurahia Waziri Mkuu kutumbua tujiulize je tutaendelea kutegemea mtu hadi lini? Majaliwa atafika kote? Hivi kina DC na RC wao hawatakiwi kufuatilia? Wanasubiri raisi au waziri mkuu aje? Raisi au Waziri Mkuu ni nyongeza tu. Wanaopaswa kukagua ni waliopewa eneo kuliongoza!
Hivi kama tunashindwa kurejesha mabaraza ya wafanyakazi kama zamani hatuwezi hâta kulipa Jeshi jukumu la kufuatilia hii miradi mikubwa ya kimkakati? Hii si vita ya kiuchumi? Hivi kweli kama Jeshi lingefuatilia DART lile bus lingejaa tope kama jaruba la mpunga?
Hivi kwa nini walau ule utaratibu wa Mwalimu wa raisi, wakuu wa mikoa na wilaya kukutana na wananchi kila Alhamisi tusiurudishe na kusimamia vizuri? Ili mwenye shida yake au taarifa za mradi kuhujumiwa apate fursa ya kueleza? Enzi zile wakubwa hawakuupenda huu utaratibu! Lakini utaratibu huu una nguvu na faida kuliko wa kuvizia mpaka raisi apite kwenu!
Ufisadi na uzembe hautaisha kama tutaendelea kutegemea mtu au watu wawili wazunguke nchi yenye karibu 1 million square kilometers !
Je kutuambua pekee inatosha? Hebu fikiri jamaa wa DART. Kwa maelezo ya waziri mkuu walikuwa na tiketi zao! Je ni héla kiasi gani ameingiza mfukoni kwa miaka 5? Ukimtumbua bila kutaifisha mali zake atasikitika au ndio atafurahi? Utafurahisha wanaoshabikia kutumbuliwa lakini hukomeshi ufisadi!
Tutafakari njia sahihi. Viongozi waendelee kutumbua ila wenye maeneo ya kazi wasikae pembeni kama hawahusiki! Hatutafika!









