

mkali@live.co.uk
23/07/2021.
Mh. Spika Ndugai,
Watanzania walio wengi wanafahamu vizuri tu umuhimu wa wananchi kulipa kodi katika taifa.
Lakini hizi kodi zisiwe kandamizi au za kukomoa maskini, hizi kodi ziwe ni za haki na ni vizuri matajiri walipe kodi kubwa zaidi katika jamii kuliko maskini.
Nchi ambazo zina ubora wa hali ya maisha kwa wananchi ( broad-based development) kama nchi za Scandinavia hivyo ndivyo wanavyofanya. Na matokeo kwenye nchi hizo huwezi kukuta upeo wa umaskini ambao ni kawaida kukutana nao katika nchi kama Uingereza au Marekani (USA).
Mwalimu Nyerere aliwahi kusema dalili ya vinchi “corrupt” ni vile vinavyoacha kukusanya kodi kutoka kwa matajiri na kuanza kufukuzana na maskini.
Hii nafikiri ni moja ya sababu za kufuta kodi ya kichwa (1968); kodi ambazo zilikuwa zinakusanywa na matarishi wa “Native Authorities.” Hizi tozi ni kurudisha nchi zama za native authorities kwa mlango wa nyuma.
Kweli inaleta mantiki kwa Serikali kulazimisha hizi tozo kandamizi, wakati:
1: Mathalani, tumeanza kusafirisha tena makinikia yetu nje kwa maelezo kuwa kodi imekwisha lipiwa kule kwenye machimbo ambako hakuna vifaa vyenye kuchenjua na kutathimini kiwango cha madini zaidi ya 12 ambayo yanakuwepo kwenye hayo makinikia? Huku si kuendeleza kuibiwa kwa raslimali zetu ambako kulikomeshwa na Serikali iliyopita?
2: Serikali inafungua maduka ambayo yaliyofungiwa baada ya kuthibitika kuwa hayo maduka yalikuwa yanafanya utakatishaji fedha. (Money laundering). Hapa ni nani anaenufaika?
3: Serikali hiyo hiyo inatoa misamaha ya kulipa kodi kwa Makampuni ya nje pamoja na Wabunge wake wakati wote hawa wakiwa na vipato wakubwa mno kulinganisha na maskini ambao wanabambizwa hizi tozo kandamizi.
Katika miaka mitano na miezi mitano ya Uongozi wa Awamu ya Tano chini ya JPM Tanzania ilishuhudia utekelezwaji wa miradi mikubwa na yenye tija kwa wananchi kuliko muhula mwingine wowote tangu uhuru wetu. Je, kulikuwa na hizi tozo kandamizi? Jibu: Hazikuwepo. Huu ulazima wa hizi tozo leo unatoka wapi?
Kadri Serikali yetu inavyojaribu kupigia chapuo hizi tozo ndivyo inavyojionyesha kwa wananchi kuwa hii Serikali haipo upande wa wananchi wanyonge; yaani Serikali haipo kwa ajili yao.
Kwenye hili suala la tozo, kuna umuhimu tena mkubwa, wa Serikali yetu kulifikiria upya.

mkali@live.co.uk
23/07/2021.