

Na Abbas Mwalimu (0719258484).
Jumatano tarehe 28 Jumatano, 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Jumanne tarehe 27 Julai, 2021 aliwaapisha Mabalozi wapya 13 kati ya 23 aliowateua mwezi Mei mwaka huu 2021.
Baadhi ya mabalozi hao watahudumu nchi kutokea ndani na wengine kama Balozi Hoyce Temu aliyepelekwa Geneva kuwa Naibu Mkuu wa Kituo wakipelekwa katika vituo (nchi) mbalimbali kuhudumu na baadhi wakisubiri taratibu za vituo kama alivyobainisha Mheshimiwa Rais Samia.
Mara baada ya kuwaapisha mabalozi hao Rais Samia Suluhu Hassan alizungumza na watanzania kupitia mabalozi hao.
Miongoni mwa mambo aliyozungumza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika hotuba yake ni Diplomasia ya Dijitali (Digital Diplomacy) akitumia neno ‘Dunia ya sasa ni Dunia ya Mtandao’, alizungumzia pia Diplomasia ya Umma ama Public Diplomacy, Diplomasia ya Afya (Health/Medical Diplomacy), Waishio Nje (Diaspora), Uwekezaji kwa Watu (Human Assets Index) na Kujitegemea (Self Reliance).
Kwa bahati nzuri nilipata kuyaandikia masuala haya yote katika nyakati tofauti na hivyo leo ninapenda kugusia suala la Diplomasia ya Dijitali.
Ni wazi kuwa mapinduzi ya intaneti yameathiri utendaji kazi wa Wizara mbalimbali za Mambo ya Nje duniani ikiwemo Tanzania kwenye masuala mbalimbali kama vile uchumi, siasa, jamii na usalama.
Diplomasia kama nyenzo mojawapo ya kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje haijaachwa kuathiriwa na mapinduzi haya katika teknolojia na hivyo kupelekea mabadiliko katika mikutano, biashara kimataifa, majadiliano, huduma za kifedha, muingiliano wa wajumbe, usuluhishi, usimamizi, utatuzi wa migogoro na usalama.
Kwa mantiki hiyo hakuna namna ambayo Tanzania itakwepa athari za teknolojia kama alivyowahi kubainisha Hayati Julius Kambarage Nyerere katika andiko lake Argue Don’t Shout (Jenga Hoja Usibwate) la mwaka 1969.
Ni wazi kuwa teknolojia ni nguvu (power) ya kimya kimya au nguvu janja (soft power) kama alivyopata kubainisha Joseph Nye (1990: 176; 2004:5) kuwa ni nguvu janga ni uwezo wa kujenga ajenda katika siasa za dunia kupitia ushawishi na kuwavutia wengine kupitia imani ya mtu au jamii husika, misingi na mawazo na si kupitia mabavu au nguvu za kijeshi. Kwa maana nyingine ni uwezo wa kumfanya au kuwafanya wengine wafanye vile unavyotaka wewe pasina kutumia nguvu ya kijeshi au vikwazo.
Hapa ndipo unapokuja umuhimu wa kutumia teknolojia katika kutekeleza,kusimamia na kulinda maslahi ya taifa letu kupitia Diplomasia ya Dijitali.
Diplomasia ya Dijitali ni dhana mpya ya Diplomasia katika karne hii ya 21 ambayo imebadili mwenendo mzima wa utendaji kazi wa asili (traditional approach) wa Wizara za Mambo ya Nje na Utekelezaji wa Sera za Nchi husika kama walivyobainisha Stanzel (2018) na Summa (2020).
Kwa tafsiri, Diplomasia ya Dijitali ni kuongezeka kwa utumiaji wa mitandao ya kijamii (social media) katika utekelezaji wa Sera za Mambo ya Nje za Nchi ili kufikia malengo yake ya maslahi ya taifa na kulinda taswira ya Nchi na kusimamia mabadiliko kupitia vifaa vya kidijitali kama walivyobainisha Segev (2015) na Holmes (2015).
Ndiyo maana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alieleza sababu za kuteua mabalozi wengi walio chini ya miaka 45 kwamba hawa wanaweza kwenda sambamba na teknolojia kuliko wazee na hivyo wasisubiri kupata taarifa kutoka ‘Capital’ wanapotakiwa kulinda taswira (image) ya nchi katika majukumu yao ya ubalozi yaliyobainishwa katika Ibara ya 3 ya Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 unaohusu Mahusiano ya Kidiplomasia.
Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameona umuhimu wa Diplomasia ya Dijitali kutokana na ukweli kuwa jamii imekuwa na ufahamu mkubwa wa mambo yanayojiri duniani kwa haraka na kumekuwa na muingiliano mkubwa baina ya watu mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Instagram, Twitter na WhatsApp.