WU® Media PRODUCTION
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza matumaini yake makubwa kwamba zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka huu 2022 litakwenda vizuri kutokana na matayarisho mazuri yaliyofanyika ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kwa Sensa ya Majaribio.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipokutana na Kamisaa wa Sensa Zanzibar, Balozi Mohamed Haji Hamza akiwa na ujumbe wake Ikulu Jijini Zanzibar, wakati alipofika kwa ajili ya kutoa taarifa juu ya Sensa ya Majaribio iliyofanyika pamoja na muendelezo wa matayarisho ya zoezi hilo linalotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu 2022.
Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuendelea kuunga mkono jitihada hizo na kusisitiza kwamba zoezi hilo kwa vile linamaslahi mapana ya Taifa na wananchi wake Serikali itaendelea kuliunga mkono wakati wote.
Rais Dk. Mwinyi alipongeza utaratibu uliwekwa wa ajira kwa watendaji wa zoezi hilo kwani mfumo huo utaondosha malalamiko yaliyowahi kutokea hapo siku za nyuma sambamba na kuweza kupata ufanisi mkubwa kutokana na watendaji ambao watatoka katika maeneo husika.
Alisema kwamba kutokana na utaratibu huo ana matumaini makubwa kuwa hakutokuwa na eneo ambalo watapatikana watu ambao hawatokuwa na sifa za kufanya kazi hiyo ambayo ina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi.