
WU® Media PRODUCTION
Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar ipo tayari kushirikiana na wadau mbali mbali wa kimataifa katika kupata Teknolojia za kisasa katika shughuli zote za bahari Ili kuendana na mabadiliko ya Dunia katika matumizi endelevu ya bahari.
Waziri wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Mheshimiwa Suleiman Masoud Makame akizungumza na wataalamu kutoka kampuni ya NAVTEK ya nchini Uturuki wanaotaka kuwekeza katika shughuli hizo hapa Zanzibar amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka utaratibu mzuri kwa wawekezaji katika sekta hii kwa manufaa ya taifa.
Amesema sekta ya Uchumi wa Buluu ndio dira ya Serikali, hivyo Serikali inatumia Teknolojia za kisasa ili wananchi wafaidike na rasilimali za bahari.
Wataalamu kutoka Kampuni hiyo ya NAVTEK ya Uturuki wakiongozwa na Captain Eugene Yalin wamesema kampuni hiyo imebobea katika uwekezaji wa baharini kwa zaidi ya miaka 40 Sasa katika nchi mbalimbali duniani.
Wamesema tayari wanaendesha miradi zaidi ya miradi 250 kwa Teknolojia za kisasa.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Dkt. Aboud Suleiman Jumbe alizungumzia umuhimu wa uwekezaji katika masuala ya miundombinu ya bandari, usimamizi na udhibiti wa taka za baharini, maendeleo ya mafuta na gesi asilia baharini, usalama na uokozi baharini.
Vile vile, Mkurugenzi Idara ya Maendeleo na Uratibu wa Uchumi wa Buluu Captain Hamad Bakar Hamad amesema watajadili zaidi na wataalamu hao katika uwekezaji wa kutengeneza mashine na boti za kutumia umeme.
Pia amewaelezea wawekezaji hao mandhari ya Zanzibar na shughuli ambazo wanaendelea nazo .Amesema Utalii unachangia pato kubwa kwa taifa lakini kutokana na ugonjwa wa COVID19 shughuli za utalii zilipungua hadi karibuni ambapo zimeanza kushika kasi.











