
WU® MEDIA PRODUCTION LIMITED
Na Mwandishi wetu
Siku ya Jumamosi ya tarehe 11/06/2022 Jumuiya ya Watanzania Napoli walitambulisha uongozi mpya baada ya uchaguzi wa kihistoria uliofanyika siku ya tarehe 4/06/2022.
Sherehe zilifana Sana na kupata muitikio Mkubwa hasa ukizingatia ni muda mrefu Diaspora wa NAPOLI hawakuwa na mkusanyiko Mkubwa wa namna yake tangu uingie mlipuko wa Uviko 19.
Sherehe zilianza kwa Sala ikiongozwa na Katibu wa Jumuiya Bi Cecilia Lemmah , Baadae aliwashukuru wote kwa mahudhurio makubwa na kuwataka kuendelea kuunga mkono uongozi. Baada ya hotuba fupi Katibu alimkaribisha rasmi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania Napoli in Campania, Bi Judith Joseph ambae alipokelewa kwa makofi mengi ambayo ni ishara ya kukubalika na pongezi.
Mwenyekiti nae aliungana na Katibu kuwashukuru Watanzania wote kwa imani kubwa waliyompa.”Nawashukuruni Sana wote waliojitokeza kupiga kura na kuitumia haki yenu ya msingi,na sasa uchaguzi umeisha twendeni Pamoja tukiacha tofauti zetu zote ,sisi ni Watanzania na asili yetu ni umoja” alisema mwenyekiti.

Mwenyekiti alitangaza rasmi kamati za Jumuiya zitakazo kuwepo na kufanya Kazi na uongozi. Kamati ziliundwa kwenye kikao Cha Viongozi mara Baada ya uchaguzi.
Pia Mwenyekiti wa kamati ya Diaspora alipewa nafasi ya kusalimia nae aliwashukuru wote kwa kuhudhuria na aliwataka waendelee kuunga mkono uongozi mpya. Vile vile mwenyekiti wa kamati ya Diaspora alitoa ujumbe na salaam za Mh Balozi Mahamoud Thabit Kombo kwa Watanzania Napoli. “Mh Balozi anawasalimu Sana, amefurahi Sana kwa hatua tulizopiga, anawapongeza viongozi wote na anawatakia mafanikio. Vile vile Mh Balozi amesisitiza umoja, upendo na ushirikiano,zaidi amesema tuendelee kuwa mabalozi wazuri wa Taifa letu kwa kufuata Sheria za Nchi na kuitangaza nchi yetu vizuri.Mh Balozi ameahidi kukutana na uongozi mara atakapo pata nafasi.” Alimaliza hivyo Mwenyekiti wa kamati ya Diaspora Ndugu Kagutta Maulidi kuwasilisha salaam za Balozi.
Mwisho alikaribishwa msaidizi wa Sindaca kutoka Napoli Bi Francesca nae alipata nafasi ya kutoa shukrani zake na kuutaka uongozi kufanya nao kazi kwa karibu.
Sherehe zilinoga zaidi kwa ushiriki wa Msanii wa kizazi kipya kutoka Tanzania “Ge2 Kay” @Getukisome ambaye yupo kikazi kwa Muda nchini Ufaransa na Italy. Ge2 atashiriki kwenye show kubwa mjini Paris siku ya tarehe 26/06/2022 , atakuwa stage moja na wasanii wakubwa wa Africa Magharibi na Ulaya.












