Na mwandishi wetu
Wabongo Ughaibuni Media
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Italy, Mh Mahamoud Thabit Kombo leo tarehe 18/08/2022 ameshiriki sala na dua wakati wa kuaga mwili wa marehemu Mustafa Munawar Karim, Mtanzania aliyefariki tangu tarehe 27/07/2022.
Mustafa Munawar Karim alikuwa akiishi Castel Volturno Caserta nchi Italy, alifariki tangu tarehe 27/07/2022 akiwa nyumabni kwake.
Umati mkubwa wa Watanzania uliogubikwa na huzuni na majonzi,ulikusanyika kutoa salama zao za mwisho kwa mwenzao na kati ya waombolezaji pia alikuwepo ndugu yake aliyekuja kwenye msiba akitokea nchi Greece ambako anaishi. Pamoja na Balozi Mahmoud Thabit Kombo , pia aliongozana na Mkewe Bi Zakia Kombo na Afisa wa ubalozi Bi Eva Kilua. Baada ya taratibu zote zilizokuwa zikisimamiwa na viongozi wa Jumuiya ya Watanzania, Watanzania walikusanyika katika chumba kilichotengwa kwa ajili ya kusalia mwili wa marehemu. Balozi Mahmoud Thabit Kombo nae alikluwa mmoja wa waliosalia mwili wa marehemu Mustafa Munawar Karim na baada ya sala Mh Balozi yeye mwenyewe aliongoza dua kumuombea marehemu.
Baada ya sala na dua, Watanzania walipita kutoa salam zao za mwisho kama ishara ya kumuaga mpendwa wao. Ratiba iliendelea kwenye ukumbi kwa ajili ya chakula cha pamoja kama sadaka kwa jili ya marehemu.
Baada ya Chakula Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania Italia (IN CAMPANIA) Bi Judith Joseph alizungumza kabla ya kumkaribisha Mh Balozi ili kutoa neno kama mwakilishi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwenye dhamana na raia wa Tanzania wanaoishi katika nchi ya Italy na mlezi wa diaspora.
Mwenyekiti wa Jumuiya Bi Judith Joseph alimshukuru sana Mh Balozi na staff wake wote kwa ushirikiano mkubwa waliotoa kwa viongozi wa Jumuiya ili kuhakikisha mahakama inatoa kibali na kukabidhiwa mwili wa marehemu ili uweze kusafirishwa nyumbani kwa mazishi. Mwenyekiti alisema haikuwa kazi ndogo kwani utata mkubwa ulikuwa kwenye vibali au vitambulisho vya marehemu ambavyo vilikuwa vinakinzana na ukweli wake.
Mwenyekiti alitumia nafasi hiyo kuwasii Watanzania wote wanaoishi katika mkoa wa Campania kujiandikisha na kujisajili kama wanajumuiya ili waweze kutambulika na kuhakikisha kila mmoja anakuwa na vibali sahihi. Mwenyekiti pia aliwashukuru sana Watanzania wote wanaoishi Napoli , Caserta na mkoa mzima wa Campania, kwa mchango wao wa hali na mali uliosaidia na kuwawezesha viongozi kutimiza wajibu wao. Vile vile Mwenyekiti aliwashukuru Watanzania wote wanaoishi mikoa mingine kwa michango yao na rambirambi kupitia jumuiya zao.
Mwenyekiti kabla kumkaribisha Mh. Balozi, alimaliza kwa kumshukuru balozi kwa kutenga muda wake kuja kushiriki pamoja na watanzania katika sala na dua ambayo aliongoza yeye mwenyewe Mh. Balozi.
Balozi Mahmoud Thabit Kombo aliwapongeza sana Viongozi na wanajumuiya wa Campania, kwa kuonyesha ushirikiano mkubwa katika suala zima la msiba, na kusema kuwa wamekuwa ni mfano wa kuigwa na jumuiya zote. Balozi pia alisisitiza kwa watanzania wote wanaoishi Italy kuwa lazima wahakikishe kuwa wanakuwa na vitambulisho na vibali na hata wale ambao hawana passport kwa sababu moja ama nyingine, wahakishe wanafuata taratibu ambazo tayari ubalozi umetoa muongozo kwa kila jumuiya. Mh Balozi pia alitoa salaam za pole na rambirambi kwa familia ya marehemu kupitia ndugu yake ambae nae mwisho alipta nafasi ya kutoa shukrani zake kwa Watanzania wote.