0 0
Read Time:2 Minute, 18 Second

Na Madaraka Nyerere

Dalili za upumbavu hizi hapa

Nimemaliza kusoma kitabu cha Mfaransa Jean-Francois Marmion, “The Psychology of Stupidity” (Saikolojia ya Upumbavu) ambaye anafafanua maana ya upumbavu akitumia tafiti na mahojiano aliyofanya na baadhi ya wanasaikolojia mashuhuri duniani.

Kwenye kitabu chake, baadhi ya maswali anayojibu ni:
• Kwanini watu wenye akili wakati mwingine huamini masuala ya kipumbavu
• Kwanini akili zetu za kivivu zinatuongoza kuchukua maamuzi yasiyo sahihi
• Kwanini kubishana na wapumbavu ni mtego
• Kwanini waliyobobea kwenye upumbavu hawatambui kuwa ni wapumbavu
• Ni jinsi gani vyombo vya habari na mitandao vinatuongezea upumbavu

Kuna changamoto kubwa za kukabiliana na upumbavu kwa sababu, aghalabu, mpumbavu ni vigumu sana kujitambua kuwa ni mpumbavu.

Zipo aina nyingi za upumbavu, kuanzia yule ambaye kila mtu anafahamu hana uwezo wa kufanya tathmini ya aina yeyote, mpaka yule mpumbavu ambaye ni msomi ambaye usomi wake unamziba macho na kufifisha uwezo wa kuchambua tofauti ya mihemuko yake na hali halisi. Anaweza akaropoka chochote, bila kujali kama ni kweli au uongo. Ni mpumbavu mwenye digrii lakini hajali umuhimu wa kulinda na kutetea ukweli. Kiuhalisia, ni hatari kuliko mpumbavu asiye msomi kwa sababu ana ushawishi mkubwa zaidi ndani ya jamii.

Sababu kubwa inayofanya vita dhidi ya upumbavu kuwa ngumu ni maendeleo makubwa ya teknolojia ya habari na mawasiliano. Wakati zamani upumbavu ulibaki na kujificha ndani ya mipaka ya kijiji, sasa hivi dunia yenyewe imekuwa kijiji. Upumbavu unaibuka Washington na ndani ya saa moja kwa kupitia mawasiliano bora tuliyonayo unatapakaa duniani kote, ukisaka wale ambao hawana chanjo dhidi yake.

Sababu nyingine ni kuwa kuchambua kila hoja inayojitokeza kunahitaji akili ya kichambuzi kila wakati, jambo ambalo si rahisi kutekeleza. Unapofika kituo cha basi unamuomba muuza tiketi kukushauri basi lipi la uhakika kutoka Mwanza hadi Dar na unaamini kuwa atakwambia ukweli; hutajaribu kupanda kila basi lililopo stendi ili ufikie uamuzi wako mwenyewe. Kitabu hiki kinakumbusha kuwa muuza tiketi hapaswi kuaminika wakati wote; anaweza kuwa ana hisa kwenye kampuni ya basi. Ni upumbavu kung’ang’ania na kurudia ushauri wa muuza tiketi kuwa ndiyo ukweli, lakini kubaini ukweli si jambo rahisi.

Hatari kubwa ya kukithiri kwa upumbavu wa aina hii ni kuwa wapo wajanja ambao wameanza kuutumia kwa propaganda, pamoja na manufaa ya kisiasa. Kama mwanasiasa anashinda uchaguzi kwa kusema ukweli hilo si tatizo; kama anafanikiwa kuchochea uongo na kuaminika na wapiga kura na kushinda uchaguzi hilo ni tatizo kubwa. Upumbavu wa wengi una athari kubwa ndani ya jamii.

Mwandishi anasema: “Ujinga si upumbavu. Ujinga ni chombo muhimu cha kuchochea ufahamu; ili mradi unafahamu kuwa hujui, na unafahamu usichokijua.”

Somo muhimu hapa ni kuwa hata kupambana na upumbavu kunahitaji msingi mdogo wa uelewa.

Ni kitabu chenye kufungua upeo. Nashauri kisomwe na yeyote anayetaka kutambua upumbavu wake na wa binadamu wenzake kwa sababu ni kwa kutambua upumbavu tu ndiyo tunaweza kuukabili.

T: @MadarakaN
I: @madarakanyerere

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %