Maaskofu Wakatoliki wa Tanzania wakiwa kwenye ziara maalumu Vatican wafanya mazungumzo na Balozi MAHMOUD THABIT KOMBO
Rome, Italy 17/05/2023
Na Mwandishi wetu ROME ITALY
WU®MEDIA
Maaskofu wa Kanisa la katoliki wa Tanzania wapo Vatican kwa ziara ya kuhiji inayofanyika kila baada ya miaka mitano.
Ziara hiyo ya baraza la maaskofu imekuwa ya kipekee Sana mwaka huu baada ya kuahirishwa kwa Kipindi kirefu kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Uviko19.
Pamoja na ratiba yao ndefu tangu wafike na ikiwa bado ratiba yao inaendelea lakini waliona ni umuhimu pia kukutana na Balozi wa Tanzania nchini Italy Mh. Mahmoud Thabit Kombo, kumsalimia lakini pia kubadilishana nae mawazo katika nyanja mbalimbali hasa kwenye huduma za kijamii ambazo wao kama kanisa Katoliki wamekuwa wakizifanya kwa muda mrefu. Mh Balozi aliwapokea wageni wake kwa hotuba ya utambulisho na historia fupi ya mahusiano mazuri ya miaka mingi baina ya Tanzania na Vatican ambapo ndiko makao makuu ya Wakatoliki. Balozi pia alikumbusha tuzo iliyotolewa na Vatican kwa Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na mzee Thabit Kombo Jecha wakati huo wa Papa John Paul II.
Mh Balozi alimtambulisha Waziri wa maji Mh. Aweso ambaye nae yupo nchini Italy kwa ziara ya kikazi. hivyo nae aliitumia nafasi hiyo kukutana na Maaskofu hao.
Kabla ya Mh.Balozi kumkaribisha Rais wa Maaskofu Tanzania Mhashamu Gervas Nyaisonga, Balozi alimpa nafasi Waziri Aweso kusalimia Maaskofu na kusema machache.
Mh. Waziri alizungumzia miradi ya kimkakati ambayo serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaitekeleza ili kuhakikisha Watanzania wanapata maji safi na salama. Mh Waziri amesema safari hii ni moja ya Kazi za miradi mikubwa ya kimkakati. Waziri aliwaomba Maaskofu kwa nafasi yao washiriki kutoa elimu kwa waumini kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira hasa kwenye vyanzo vya maji. Waziri amesema inasikitisha Sana kuona vyanzo vingi vya maji vimepotea kutokana na uharibifu wa mazingira. Waziri Aweso amewaomba maaskofu na viongozi wa Dini waendelee kuliombea Taifa la Tanzania amani Pamoja na kusisitiza umuhimu wa maadili kwa jamii kama afanyavyo Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Mh waziri pia awaomba Maaskofu kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Afya njema ili aweze kuendelea kuliongoza Taifa letu.
Balozi pia alimpa nafasi katibu mkuu wizara ya maji Eng. Nadhifa Kemikimba ambae ameongozana na Mhe. Waziri Juma Aweso nchini Italy kwa ziara ya kikazi wakiambatana na wataalamu wa sekta hiyo.
Baada ya maombi Balozi Mahmoud Thabit Kombo alipata picha za pamoja na wageni wake akiwemo Mkuu wa majeshi mstaafu (CDF) Meja generali Venance Salvatory Mabeyo ambae nae alikuwa mmoja wa walioongoza na maaskofu kutoka Parokia yake akiwakilisha familia zote kwa ujumla.
Picha na H.Jiwe
contact: WU® MEDIA
tel. +39 3898573370
Email: info@tzabroad.com