Na Mwandishi wetu 10/02/2024
Rome Italy
Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alikutana kwa chakula cha jioni na Wanafunzi wanaosomea dini Vatican pamoja na jumuiya za Watanzania nchini Italy zilizowakilishwa na viongozi wao. Pamoja nao pia walikuwepo wajumbe wa kamati kuu ya diaspora Italy na uongozi mzima.
Pamoja nae Mh. Rais aliongozana na Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika mashariki, Mh. January Yusuf Makamba. Kabla ya chakula cha jioni , hafla ilianza kwa sala na dua na baadae kupata neno la ufunguzi lilitolewa na balozi wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mahmoud Thabit Kombo.
Vilevile Balozi wa Tanzania Vatican My. Hassani Iddi Mwamweta alitoa salaam. Balozi alimpongeza MH Rais kwa kupata mwaliko na Papa Francesco kwani mara ya mwisho alikuwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete mwaka 2007
Ratiba iliendelea kwa hotuba fupi ya Mh January Yusuf Makamba. Kwa kuwa ilikuwa ni hafla ya Mh Rais kukutana na Wanafunzi na Diaspora kwa ujumla, kulikuwa na risala ya wanafunzi ilisomwa na mwenyekiti wa jumuiya ya wanafunzi wa Vatican Fr. Emmmanuel Tumaini Karia
Baada ya risala ya wanafunzi ilifuata risala ya Diaspora ambayo ilisomwa na Mwenyekiti wa Kamati kuu ya diaspora nchini Italy ndugu Nsangu M. Kagutta.
Katika risala ya diaspora , Kwa niaba ya diaspora Mwenyekiti alimshukuru Rais kwa mualiko wa chakula cha jioni ili kusalimiana nao na kusikiliza machache kutoka kwao. Diaspora wamempongeza rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoiofanya tangu kuingia madarakani, kwa kuendeleza kazi kubwa walizozianzisha yeye na mtangulizi wake Hayati Dkt John Pombe Magufuli. Diaspora pia walieleza changamoto walizonazo na kumuomba Mh Rais kuzitafutia majawabu kupitia wizara husika na wasaidizi wake.
Pamoja na kujibu maswali ya Diaspora , Rais Samia Suluhu Hassan aliwataka diaspora kuwa wazalendo na kuisemea mazuri nchi yao bila kujali tofauti za itikadi zao. Kuwa mabalozi wazuri wanapoishi ugenini na kujiepusha na vitendo ambavyo vinaiharibia sifa nchi yao. Pia Rais aliwataka watanzania wote kujiandisha kwenye mtandao wa diaspora Hub. Rais Samia ameahidi kuyafanyia kazi maombi ya diaspora yanayohusu changamoto zao.
Diaspora katika picha