
Yerevan ARMENIA
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amependekeza Tanzania na Armenia kushirikiana kuanzisha kituo cha mafunzo ya teknolojia nchini Tanzania, ili kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kisasa na kukuza ubunifu.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 15 Oktoba 2026, alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Armenia, Mhe. Vahagn Khachaturyan, katika Ikulu ya Yerevan, nchini Armenia, ambako yupo kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa Viongozi wa Dunia kuhusu Bioanuai (COP17).
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamejadili fursa za kuimarisha ushirikiano katika elimu, teknolojia, utalii na uhusiano wa kidiplomasia, ikiwemo kubadilishana wanafunzi na kuanzisha kituo cha mafunzo ya teknolojia kwa kutumia uzoefu wa Armenia.
Rais Khachaturyan amesema Armenia iko tayari kuimarisha ushirikiano na Tanzania, akieleza kuwa nchi hiyo imetenga nafasi 50 za masomo katika vyuo vyake vya elimu ya juu kwa wanafunzi kutoka nchi za Afrika, huku akitaja pia teknolojia ya kisasa, hususan akili mnemba (AI), kuwa eneo lenye fursa za ushirikiano.
Kuhusu COP17, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika uhifadhi wa bioanuai na mazingira, akieleza kuwa Tanzania imetenga karibu theluthi moja ya eneo lake kwa shughuli za uhifadhi.
Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi amewasilisha mwaliko wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Rais Khachaturyan kutembelea Tanzania katika wakati utakaomfaa.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Kinyasi Millya, Balozi wa Tanzania nchini Urusi anayewakilisha pia Tanzania nchini Armenia, Mhe. Fredrick Ibrahim Kibuta, pamoja na viongozi wengine wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


















