
Belgrade
Tanzania na Serbia zimekubaliana kuanzisha Tume ya Pamoja ya Uchumi kwa lengo la kukuza biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), na Waziri wa Mambo ya Nje wa Serbia, Mhe. Marko Đurić, pembezoni mwa Mkutano wa Kumbukizi wa Ngazi ya Juu wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowore (NAM), unaofanyika jijini Belgrade, Serbia.
Katika kikao hicho cha Mawaziri hao wa Mambo ya Nje, Tanzania imeainisha fursa katika kilimo, madini, nishati, miundombinu, usafirishaji, utalii, uvuvi na uchumi wa buluu, huku Serbia ikieleza utayari wa kuwa lango kwa wafanyabiashara wa Tanzania wanaolenga masoko ya Ulaya.
Viongozi hao pia wamejadili kuimarisha ushirikiano kati ya Shirika la Ndege Tanzania ( ATCL) na Shirika la Ndege la Serbia (Air Serbia) pamoja na kuongeza muunganiko wa usafiri wa anga kati ya Tanzania na Serbia.
Katika hatua nyingine, Tanzania imepongeza uamuzi wa Serbia wa kuanzisha Ubalozi wa Kudumu jijini Dodoma, na kueleza utayari wake wa kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia, biashara na uwekezaji.
Mhe. Kombo amesema Tanzania iko tayari kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na Serbia, huku Serikali za nchi hizo zikiendelea na mchakato wa kuanzisha Tume ya Pamoja ya Uchumi.
Mazungumzo ya viongozi hao yalihusisha pia sekta binafsi, ambapo ujumbe wa Tanzania wenye takribani washiriki 20 upo nchini Serbia, huku zaidi ya kampuni 40 za Serbia zikitarajiwa kushiriki katika mazungumzo ya kibiashara ya pande mbili














