
WU®Media
Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Sweden umeratibu na kuwa mwenyeji wa Serengeti Bonanza 2026. Bonanza hili la mpira wa miguu lililoanza tarehe 7 Agosti 2026 na linatimishwa tarehe 8 Agosti 2026 jijini Stockholm, Sweden.
Bonanza hilo limewakutanisha Watanzania waishio nje ya nchi, marafiki wa Tanzania na wadau mbalimbali kutoka mataifa tofauti kwa lengo la kuimarisha umoja na mshikamano kupitia michezo, kujenga mitandao na kuitangaza Tanzania kimataifa.
Mgeni Rasmi katika bonanza hilo ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Diaspora na Fursa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Salvator Mbilinyi
Akifungua Bonanza hilo, Bw. Mbilinyi amesema Serikali inatambua nafasi na mchango mkubwa wa Diaspora katika maendeleo ya Taifa, na inaendelea kuweka msisitizo katika kuwawezesha Watanzania wanaoishi nje ya nchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, kiuchumi na maendeleo ya Taifa.
Akitoa neno la ukaribisho, Balozi wa Tanzania nchini Sweden Mhe. Swahiba H. Mndeme, alisema Serengeti Bonanza limeendelea kukua na kuwa zaidi ya mashindano ya michezo, na sasa ni jukwaa muhimu la kuwaunganisha Watanzania waishio nje ya nchi, kuwafikishia huduma mbalimbali, kukuza utamaduni wa Kitanzania, kujenga mitandao na kutangaza fursa za biashara, uwekezaji na utalii zilizopo Tanzania.
Balozi Mndeme pia ameeleza umuhimu wa Diplomasia ya Michezo, akibainisha kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kuunganisha jamii, kujenga na kuimarisha mahusiano pamoja na kuitangaza Tanzania na fursa zake kimataifa.
Serengeti Bonanza 2026 limekutanisha timu 14 kutoka nchi tisa ambazo ni Uingereza, Ubelgiji, Uholanzi, Finland, Sweden, Kenya, Uganda, Sudan na Tanzania. Ushiriki huo unaonesha namna Bonanza linavyoendelea kukua na kuwa jukwaa la kuwakutanisha Watanzania na marafiki wa Tanzania kutoka mataifa mbalimbali.
Mbali na michezo, Bonanza hilo limetoa fursa kwa Watanzania waishio nje ya nchi kupata huduma kutoka Uhamiaji, UTT AMIS na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).



















