0 0
Read Time:3 Minute, 34 Second

Na mwandishi wetu

AVERSA, ITALIA โ€“ Novemba 28, 2026 

Mkutano wa kibiashara na fursa za uwekezaji uliopewa jina la “Lango la Kuingia Masoko ya Afrika: Tanzania” (Porta d’accesso ai mercati africani: Tanzania) umefanyika leo kwa mafanikio makubwa katika mji wa Aversa (Caserta), nchini Italia. 

Mkutano huo ulioandaliwa na taasisi ya Italia-Africa Cooperazione Internazionale (IACI) kwa ushirikiano na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Italia, umevutia wadau mbalimbali wa kibiashara na wawekezaji 

Ingawa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk, hakuweza kuhudhuria kutokana na majukumu mengine alituma ujumbe kumwakilisha. Ujumbe huo uliongozwa na Waziri Mshauri (Minister Plenipotentiary), Bw. Songelaeli W. Shilla, aliyeambatana na Mwambata wa Kilimo (Agricultural Attachรฉ) na Mwakilishi wa mashirika ya FAO, IFAD na WFP jijini Roma, Bi Jacqueline Mbuya. 

Ufunguzi Rasmi wa IACI na Mazingira ya Uwekezaji 

Mkutano huo ulifunguliwa rasmi na Rais wa taasisi ya COINS, Prof. Vincenzo Palumbo, ambaye alitoa muhtasari mfupi wa malengo ya mkutano kabla ya kumkaribisha mwenyeji wa shughuli hiyo, Rais wa Italia-Africa Cooperazione Internazionale (IACI), Wakili (Avv.) Angela Felicia Senese. 

Katika hotuba yake, Wakili Senese alieleza kuwa siku ya leo ni ya kihistoria na muhimu sana kwa taasisi ya IACI, kwani pia ni siku uzinduzi rasmi wa shughuli za taasisi hiyo. Hatua hii inakuja mara baada ya yeye binafsi pamoja na Katibu wa IACI, Ndugu Kagutta N. Maulidi, kuteuliwa rasmi na Balozi wa Tanzania nchini Italia kuwa Wawezeshaji wa Biashara na Uwekezaji (Trade and Investment Facilitators). 

Aidha, Wakili Senese alitoa muhtasari mpana kuhusu Tanzania, akirejea uzoefu wake binafsi alipotembelea nchi hiyo mwaka 2010. Alibainisha faida za kijiografia za Tanzania kama lango muhimu la kibiashara katika ukanda wa Afrika, pamoja na kusisitiza kuwa amani, utulivu wa kisiasa, na usalama uliopo nchini humo ni msingi imara unaomhakikishia mwekezaji usalama wa mtaji wake. 

Kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Wakili Senese alitoa shukrani za dhati kwa Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, kwa kutuma wawakilishi wabobezi katika masuala ya Diplomasia na uchumi. 

Sababu za Kuwekeza Tanzania, Maandalizi ya Forum ya Napoli na Kipaumbele cha Kilimo 

Akizungumza kwa niaba ya Balozi wa Tanzania, Bw.ย Songelaeli W. Shilla aliwaeleza wadau waliohudhuria kuhusu fursa lukuki zilizopo nchini Tanzania katika sekta za kimkakati ikiwemo kilimo biashara, nishati, miundombinu, madini muhimu, na teknolojia ya kidijitali. Bw.Shilla alifafanua kwa kina kwa nini wawekezaji wa Italia wanapaswa kuichagua Tanzania na si sehemu nyingine, akianisha sababu mbalimbali za msingi ikiwemo kuwepo kwa amani na utulivu wa kisiasa (peace and political stability), sera rafiki za uwekezaji, na mazingira wezeshi ya kufanya biashara.ย 

Aidha, Bw. Shilla aliwasilisha ujumbe maalum wa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk kuwa mkutano wa leo ni mwanzo wa matayarisho na maandalizi makubwa ya jukwaa (forum) la kibiashara na uwekezaji. Kwa mujibu wa Balozi Mbarouk, jukwaa hilo litaandaliwa na Ubalozi kwa kushirikiana na Italia-Africa Cooperazione Internazionale (IACI) na linatarajiwa kufanyika katika jiji la Napoli. 

Kwa upande wake, Mwambata wa Kilimo, Bi Jacqueline Boniface Mbuya, alipata nafasi ya kuzungumza na wawekezaji hao na kufafanua maeneo ya kipaumbele katika sekta ya kilimo na ufugaji. Alieleza fursa zilizopo katika uongezaji wa thamani wa mazao, kilimo cha kisasa, na ushirikiano wa kiteknolojia ambao unaweza kuleta tija kwa pande zote mbili za Tanzania na Italia. 

Msimamo wa Diaspora katika Diplomasi ya Uchumi na Kufungwa kwa Mkutano 

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na viongozi wa Jumuiya ya Watanzania Mkoa wa Campania, wakiwemo Mwenyekiti Bi. Judith Joseph, Makamu Mwenyekiti Ndugu Hussein Msawira, na Katibu wa Jumuiya Bi. Cecilia Lemmah. Viongozi hao walitambulishwa rasmi mbele ya hadhira na Mwenyekiti wa Kamati ya Diaspora ya Tanzania nchini Italia, Ndugu Kagutta N. Maulidi, ambaye pia ni Katibu wa Italia-Africa Cooperazione Internazionale (IACI). 

Katika hotuba yake, Mwenyekiti wa Diaspora, Ndugu Kagutta N. Maulidi, alieleza kuwa anapenda kumhakikishia Balozi  kupitia Waziri Mshauri Bw. Shilla  kuwa Diaspora wa Tanzania nchini Italia wanaitikia kwa vitendo wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyewataka Watanzania wanaoishi nje ya nchi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa sera ya Diplomasi ya Uchumi. 

Akihitimisha ratiba ya mkutano huo, Wakili Angela Felicia Senese, alitoa neno la shukrani kwa washiriki wote waliohudhuria na kufunga rasmi mkutano huo uliomalizika kwa mafanikio makubwa na matumaini mapya ya ushirikiano wa kibiashara kati ya Italia na Tanzania. 

AVERSA CE.
Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %