WU®Media PRODUCTION LIMITED
Watanzania wanaoishi nje ya nchi maarufu kama diaspora, wamekuwa na mijadala mikubwa kuhusu uraia pacha, mara baada ya wabunge kuanza kuchangia hotuba ya waziri wa mambo ya nje Mh Mulamula. Wakati wa kuchangia hotuba hiyo wabunge walijikita kwenye kipengele cha diaspora ambacho kila mmoja alijaribu kutoa maoni yake kuhusu faida za uraia pacha. Wamemtaka waziri pia kutoa maelezo na ufafanuzi kuhusu dhamira ya serikali kutoa hadhi maalumu kwa diaspora badala ya uraia pacha.
Pamoja na diaspora wengine kuunga mkono hoja za wabunge , lakini bado lipo kundi kubwa la hao diaspora linalopinga hoja ya uraia pacha . diaspora hao wameonyesha hofu yao ikiwa bunge litafanya marekebisho ya katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuruhusu uraia pacha.
Maoni na mijadala inayoendelea kwa takriban siku ya tatu sasa ni mingi ila hapa tutakuletea maoni ya nguli na mchambuzi wa masuala ya kimataifa ndugu Harid Mkali. Ndugu Mkali ni Diaspora anaeishi Uingereza (UK).
Wakati akijibu hoja aliandika haya..:-
TATIZO LETU KUBWA NI ARIDHI.
Nilichotaka kukisema hapo ni kwamba hayati JPM alianzisha ujenzi wa miradi mikubwa kama vile: Bwawa la Mwalimu Nyerere kule Rufiji, Reli ya kisasa almaarufu kama SGR, Ufufuaji wa Shirika letu la Ndege, Reli na Usafiri wa majini nk nk. Kwenye miradi hii yote hakukuwa na mchango wa moja kwa moja wa kutoka Diaspora.
Ni kweli kuwa Banki Kuu ina takwimu za fedha shilingi takribani bilioni 648 ambazo Wanadiaspora wamepeleka nyumbani. Lakini fedha hizo hazikwenda kwenye miradi ya Taifa kama niliyoigusia hapo juu. Fedha hizi zilipelekwa aidha kwa ndugu na jamaa au kwenye miradi binafsi ya Wanadiaspora wenyewe.
Je, Uraia Pacha usipotolewa Wanadiaspora wa Tanzania tutaacha kusaidia ndugu na jamaa zetu nyumbani?
Mimi ninasadiki kuwa ujenzi wa Taifa utaendelea hata bila ya michango ya kutoka Diaspora. Sisemi kuwa michango ya Diaspora si muhumu. La hasha.
TATIZO NI ARIDHI
Hofu yangu kubwa ipo kwenye suala la ardhi.
Napenda kutolea mfano wa jirani ya Kenya.
Kenya hivi sasa ni watu takribani milioni 53.7.(UN estimate 2020).
(1) Katika hawa, watu asilimia 13 (13%) yaani watu wapatao milioni 6.9 hawana ardhi kabisa. (absolutely landless).
(2) Asilimia 67, yaani watu karibu milionj 35.9 wana wastani wa pungufu ya hekta moja (ambayo karibu ni sawa na hakuna).
(3) Zaidi ya nusu ya ardhi yenye rutuba nchini Kenya imehatamiwa na asilimia 20 ya watu.
(4) Kenya haina “full employment or welfare state), yaani Serikali haitowi ruzuku ya kuwakimu watu ambao hawana aridhi ya kulima au hawana ajira.
Hii ndio hali iliyosabisha walichokiita (post election violence) ya 2007/2008. Uchaguzi ulikuwa ni symptom; ugonjwa wenyewe ulikuwa ni uhaba wa aridhi ulikithiri.
Na kwenye makubaliano yaliyoleta usuluhisho wa ile vita ya wao wao; ibara ya nne ilisema: Utaifishaji na ugawaji mpya wa ardhi ni muhimu.
Lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika. Katiba yao Mpya ya 2010 ilichofanya ni kuhalalisha hii hali ambayo si ya haki kwa miaka mingine 99.
Sasa tuwe na Uraia Pacha na Kenya au Jumuiya/Shirikisho lenye kipengere cha “land sharing” hawa Wakenya milioni 42.9 ambao ni jumla ya wasio na aridhi kabisa na wenye pungufu ya hekta moja – kweli
wataacha kuhamia kwetu ambako (kwa sasa kuna aridhi ya kutosha?)
Hiyo ni Kenya tu. Kuna Rwanda, Burundi na Uganda ambako aridhi ni matatizo makubwa sana.
Je, watu wa nchi zote zinazotuzunguka wakiwa na haki ya kuja kuishi Tanzania kwa kutumia tiketi ya uraia pacha, kweli tutakuwa na amani?








