
NIDHAMU NA UTII KWA AMIRI JESHI MKUU SIO SUALA LA MJADALA.
George Michael Uledi.
Kyela, Mbeya.
April 13, 2021.
Siri kubwa ya kupiga hatua za kimaendeleo katika Taifa ni uwepo wa utii na nidhamu ya kusikiliza, kufuata na kuteleleza maelekezo ya viongozi wa kitaifa. Hii ndio sheria na kanuni ya kwanza ya kiashiria “Indicator” cha wapi Taifa linataka kwenda na lini Taifa litafika linapotaka kwenda.
Taifa lenye viongozi waadilifu, wazalendo na wenye mapenzi mema kwa nchi yao wakifungamanishwa na wananchi wenye utii na nidhamu kwa hakika maendeleo katika Taifa hilo hayataepukika! Sheria ya pili ya kufikia nchi ya asali na maziwa ni lazima dhana hizo kuu mbili zisimame pamoja.
Faida ya kuwa na Watanzania wenye nidhamu na utii kwa Taifa lao sio tu hujenga umoja bali pia hujenga uhuru na uwezo wa Taifa kupambana na maadui wa ndani na wa nje ya taifa lao.
Maendeleo ya leo ya Nchi ya China katika kila sekta ni matokeo ya kuwa na Taifa la watu wenye nidhamu na utii kwa uongozi wa XI Jinping, Rais wa China wa sasa ambaye ameweza kuaminiwa na Wachina baada ya kupewa nafasi ya kutekeleza maono yake tangu mwaka 2013. Hivyo, baadae Wachina kuamua kubadilisha katiba na kuondoa ukomo wa vipindi vya Urais kwa XI Jinping.
China leo ndio Nchi ya pili duniani kwa kuwa na uchumi mkubwa baada ya Marekani huku ripoti zikiitaja China kuwa Nchi yenye uchumi mkubwa duniani kufikia mwaka 2028 tofauti na makadirio ya China yenyewe ya kuwa na uchumi mkubwa duniani kufikia mwaka 2035.