Na
mkali@live.co.uk.
24/07/2021.
Jamani, Hawa mabeberu wanataka kutuzamisha kwenye dimbwi la madeni yasiyolipika kwa lengo la kutunyang’anya uhuru tulionao kama Wachina wanavyofanya hivi sasa au hao mabeberu wenywe walitufanyia kuputia kitu kilichoitwa “Structural Adjustment Programmes” SAPs za miaka ya 1980s.
SAPs zilitulazimisha sisi kufuta ruzuku kwa wakulima wetu; wakati zaidi ya asilimia 50 ya bajeti ya Umoja wa Ulaya ni ruzuku kwa wakulima wao. Yaani fedha ambazo zinatolewa bure si mkopo kwa wakulima hao.
Iwapo kuwanyima ruzuku wakulima ni azizi kwa nini hao wenyewe hawafanyi?
Marekani (USA) nayo inatoa ruzuku lukuki kwa wakulima wake.
Aidha hawa mabeberu walitulazimisha kufuta mifumo ya elimu bure, afya bure nk nk.
Na walitulazimisha haya yote ili tuweze kulipa mikopo ambayo wao wenyewe walitushawishi kuchukuwa kama wanavyofanya hivi sasa.
Mikopo ya nyuma mataifa yetu haikuihitaji, tena ni mikopo ambayo ilinufaisha viongozi waliokuwa madarakani wakati huo. Na mikopo ya leo inaelekea kuchukua sura hiyo hiyo.
Wakati hawa mabeberu wanaingilia ‘internal affairs’ zetu kupitia taasisi yao ya (IMF) International Monetary Fund; Mwalimu Julius Nyerere wakati anakataa haya masharti yao ya kishenzi aliwahi kuuliza: tangu lini IMF imasimama ‘ for
International Ministry of Finance?
Tukirudi kwenye hii inayoitwa mikopo ya kutusaidia kumudu korona.
Tanzania inataka kuchukua “mkopo” wa dola zaidi ya milioni 500 kwa ajili ya kukusanya takwimu za korona. Ni takwimu gani hizo zitahitaji mkopo wa upeo huu? Na huo ni mwanzo tu. Nini itakuwa hatima ya haya madeni? Serikali yetu inajua inachofanya hapa? Huku ni kutojua au ni makusudi?
USHAURI
Msimamo wa hayati Magufuli wa kukataa kuchukua mkopo wowote wa kushughulikia korona, ulikuwa siyo tu ni sahihi bali ni msimamo wa kizalendo.
Kinachoendelea hivi sasa nchini kinaweza kuwa ni kutuuza sisi na vizazi vyetu vijavyo. Napenda kurudia kuwa ninasema kinawezekana kuwa, sisemi ndicho.
Taifa kamwe lisiruhusu wachache wetu wauze Taifa letu kwa manufaa yao. Muda wa kurekebisha haya makosa tunao.
mkali@live.co.uk.
24/07/2021.