Na Abbas Mwalimu (0719258484).
Ijumaa tarehe 27 Agosti,2021.
Rais mpya wa Zambia, Mheshimiwa Hakainde Hichilema maarufu kama HH ameweka bayana kuwa hatoishi katika makazi ya Nkwazi yaliyopo Ikulu ya Zambia iliyopo Mtaa wa Uhuru, Lusaka bali ataishi katika nyumba yake maarufu kama Nyumba ya Jamii.
Rais HH alibainisha hayo Jumanne tarehe 24 Agosti, 2021 siku aliyokula kiapo, lakini kufuatia sintofahamu ya wazambia, Katibu Mkuu wa chama cha United Party for National Development (UPND) ambacho ni chama kinachoongoza serikali, Bwana Batuke Imenda amefafanua kauli ya Rais HH kuwa alichomaanisha Rais huyo ni kuwa ataendelea kuishi kwenye Nyumba ya Jamii iliyopo mji wa New Kasama na kufanya kazi kutokea Ikulu.
Licha ya ufafanuzi huu wa Katibu Mkuu wa chama tawala UPND lakini bado baadhi ya wazambia wamekuwa na hofu juu ya Rais HH kuishi katika Nyumba ya Jamii wakiamini kuwa Ikulu zimejengwa maalumu kwa viongozi na zina usalama wa kutosha.
Katika kulitazama hilo, binafsi, sitapenda kujikita katika suala la kuhama ama kutohama ikulu, bali nitajikita katika kauli aliyotoa katika hotuba yake kuwa, “Hakuna Mzambia atakayeenda kulala usiku akiwa na njaa” na muhimu zaidi aliposisitiza kuwa hatakuwa na uvumilivu kwa wala rushwa.
Kwa mtazamo wangu, miongoni mwa mambo yaliyomuangusha Rais aliyepita, Edgar Lungu, ni haya mawili ya njaa inayochangiwa na umasikini wa kutupwa wa wananchi na rushwa, hivyo kuyaona haya ndiyo hoja muhimu ya kuhakikisha anaishughulikia kuliko suala la makazi.
Kimsingi zaidi, tatizo hili la njaa na umasikini si la Zambia peke yake, bali ni tatizo la Afrika nzima japo kuna baadhi ya nchi zimeonesha mafanikio katika mapambano yake dhidi ya changamoto hizi.
Nasema ni tatizo la Afrika nzima kwa sababu limeainishwa kama lengo mojawapo la Afrika kulifikia pindi ifikapo mwaka 2025 kuwa na Afrika yenye usalama wa chakula na kutokuwepo kwa njaa Afrika nzima (Rejea ripoti za AU, 2014 na 2015). Lakini pia ni sehemu ya malengo ya Afrika kufikia mwaka 2063 inayojulikana kama Agenda 2063. Je litafikiwa?
Lakini kipekee zaidi, matatizo haya ya rushwa na njaa yaliyobainishwa na Rais HH yanasababishwa na kuyumba kwa utawala (governance) Afrika.
Hili lilipata kuwekwa bayana katika Ripoti ya Benki ya Dunia maarufu Berg Report ya mwaka 1981 Accerelated Development in Sub-Saharan Africa: A Plan for Action, kwamba tatizo kuu la Afrika ni Utawala (Governance).
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Utawala (Governance) ni namna ambavyo mamlaka na madaraka yanatumika katika kusimamia vema uchumi wa nchi na rasilimali zake kwa ajili ya maendeleo ya nchi husika.
Birner (2007) yeye aliongezea kwa kusema kuwa, ‘Governance is the exercise of economic, political, and administrative authority to manage a country’s affairs at all
levels’, kwa tafsiri yangu ni kwamba, utawala ni zoezi la usimamizi wa uchumi, siasa, na mamlaka ya kiutawala katika kusimamia masuala ya nchi katika ngazi zote.
UNDP wao wamebainisha kuwa utawala, na hasa utawala bora unahusisha pia ushiriki wa wananchi na uhusishwaji wa kundi la watu masikini katika kufanya maamuzi ya ugawanyaji wa rasilimali za nchi kwa ajili ya maendeleo (Birner, 2007).
Kwa maana nyingine ni kwamba tatizo kubwa la Afrika ni kukosa usimamizi mzuri wa uchumi na rasilimali na ugawanyaji sahihi wa rasilimali hizo kwa ajili ya kuleta maendeleo ya wananchi wa nchi husika.
Katika hili, Paul Collier katika andiko lake Wars, Guns, and Votes: Democracy in Dangerous places la mwaka 2009 ameweka mkazo kwa kusema, ‘wakati rasilimali zina nafasi kubwa ya kusaidia kuleta maendeleo Afrika, zimekuwa zikisaidia pia kuchochea migogoro.’
Kwa mantiki hiyo basi, Rais HH ana kazi kubwa ya kuondoa umasikini, njaa na rushwa nchini Zambia, kimsingi akifanya haya atakuwa anatakeleza sehemu ya dhana ya Utawala (Governance).
Kwa mujibu wa OECD, kukikosekana Utawala thabiti unaokidhi matakwa ya wananchi husababisha kuwepo kwa mambo manne ambayo ni kukosekana kwa uwajibikaji (lack of accountability), kukosekana kwa uwazi (transparency), kukosekana kwa Utawala wa Sheria (rule of law) na kuongezeka na hatimaye kutamalaki kwa rushwa (Corruption). Rejea Managing Development: The Governance Dimension, Discussion Paper, World Bank, 1991.
Inawezekana kukawa na sababu za kipekee za kimaeneo zinazosababisha njaa na umasikini Afrika lakini bado haziondoi ukweli kuwa sehemu ya umasikini wa Afrika inasababishwa na rushwa na utawala dhaifu (poor governance). Hili lilipata kubainishwa pia na Addae-Korankye katika andiko lake, ‘Causes of Poverty in Afrika: A Review of Literature’, la mwaka 2014.
Hivyo basi, haya yote kwa ujumla wake hupelekea kuwepo kwa njaa na umasikini.
Birner (2007) yeye alisisitiza pia kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya utawala, umasikini na usalama wa chakula.
Kwa msingi huo, njaa ni sehemu ya kukosekana kwa usalama wa chakula. Hivyo Rais HH ana wajibu wa kupambana na hayo katika utawala wake.
Kwa upande mwingine, kukosekana kwa utawala thabiti na hatimaye nchi husika kuwa na utawala dhaifu (poor governance) inaelezwa kuwa ni aina mpya ya kitisho cha kiusalama (contemporary security threat) kinacholikabili bara la Afrika (Rejea andiko la Paul Collier, Security Threats Facing Africa and its Capacity to Respond).
Kwa bahati nzuri nilimsikia Rais HH akisisitiza kuwa Serikali yake haitavumilia rushwa, itahakikisha inapunguza matumizi yasiyo ya lazima, itapunguza deni linaloikabili Zambia (ripoti za IMF na Benki ya Dunia zinaonesha kuwa Zambia ndiyo nchi inayoongoza kwa madeni Afrika) na kupambana kurejesha imani ya jamii na soko.
Kwa maoni yangu, kuna hitajio kubwa kwa Rais HH kuhakikisha watu wasikini wanatazamwa kipekee katika muktadha mzima wa maendeleo Zambia.
Hivyo basi utawala wake unatakiwa uangalie namna ya kuwa na sera zitakazowafanya wananchi masikini washirikishwe moja kwa moja katika uchumi, kwa kuwa kukikosekana usimamizi na mgawanyo mzuri wa rasilimali mara nyingi husababisha kutokea kwa mgawanyiko mkubwa wa kipato kati ya walio nacho na wasio nacho na hivyo kundi la wasio nacho kujikuta limetengwa (marginalized) katika keki ya taifa na maendeleo na hivyo kusababisha umasikini mkubwa kwa kundi hilo. Mondal (2018) Poverty, Politics and the Socially Marginalized-a state level analysis in India alibainisha haya pia.
Hivyo basi, kwa maoni yangu, hoja muhimu si kuhama Ikulu na kuamua kuishi Nyumba ya Jamii pale New Kasama, bali hoja ni namna gani Serikali ya Rais HH itatatua matatizo ya njaa na umasikini yanayoikabili Zambia? Hili ndiyo suala la msingi, ambalo kimsingi linahitaji utawala imara kuhakikisha kunakuwa na usimamizi mzuri wa rasilimali, ugawanyaji mzuri wa keki ya taifa, ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi itakayoweza kuwajumuisha wananchi katika uchumi, kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kuwekeza katika kilimo kitakachoondoa shida ya chakula.
Wenu:
Abbas Mwalimu (Facebook|Instagram|Twitter).
+255 719 258 484
Uwanja wa Diplomasia (Facebook|Instagram).