0 0
Read Time:4 Minute, 45 Second

Na Abbas Mwalimu (0719258484).

Ijumaa tarehe 27 Agosti, 2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Alhamisi tarehe 26 Agosti, 2021 alipokea Hati za Utambulisho wa Mabalozi watano walioteuliwa kuziwakilisha Nchi zao hapa nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Ndugu Jaffar Haniu ni kwamba Mabalozi hao ni Mhe. Martin Klepetko wa Jamhuri ya Czech, Mhe. Maria Alejandra wa Jamhuri ya Chile, Mhe. Pavel Vziatkin wa Jamhuri ya Belarus, Mhe. Luke Joseph Williams wa Australia na Mhe. Monica Greiff Lindo wa Jamhuri ya Colombia.

Mabalozi hawa wote wanawakilisha nchi zao hapa nchini lakini makazi yao ni jijini Nairobi nchini Kenya.

Wadau wengi wamekuwa wakiuliza, kwa nini mabalozi hawa wawakilishe nchi zao katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini wawe na makazi yao nchi ya Kenya? Je hili ni sahihi?

Jibu ni kuwa hakuna tatizo lolote kwa mabalozi kuwakilisha nchi zao hapa nchini wakiwa na makazi yao jijini Nairobi nchini Kenya.

Ni sahihi na hakuna tatizo lolote kwa sababu ni suala la kimkataba. Labda suala la muhimu hapa ni kufahamu usahihi wake upoje kwa mujibu wa Mkataba?

Kimsingi usahihi wake unatokana na Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 unaohusu Mahusiano ya Kidiplomasia kwa Kingereza Vienna Convention on Diplomatic Relations of 1961 (VCDR1961).

Mkataba huu, kwanza umeainisha wazi kuwa mahusiano ya kidiplomasia yataanzishwa kwa ridhaa baina ya nchi husika ama nchi na taasisi ama mashirika ya Kimataifa.

Ibara ya 2 ya VCDR 1961 inasomeka kama ifuatavyo:

‘The establishment of diplomatic relations between States, and of permanent diplomatic missions, takes place by mutual consent.’

Kwa mantiki hiyo Tanzania ina mahusiano ya kidiplomasia na nchi hizo yaliyoanzishwa miaka mingi mno isipokuwa nchi hizo hazina vituo vya kudumu vya balozi zao hapa nchini.

Labda jambo muhimu kujua hapa ni kwa nini makazi ya Mabalozi hao yawe Jijini Nairobi na si Dar es Salaam?

Kwa kawaida Balozi ama Vituo (Post) hufunguliwa katika Miji Mikuu isipokuwa labda kuwe na sababu maalumu kwa mfano kama ilivyokuwa miaka kadhaa kwa nchi yetu ambapo Balozi nyingi zipo Dar es Salaam mji ambao ni wa Kibiashara licha ya kuwa Mji Mkuu na Mji wa Serikali ni Dodoma. Nadhani hili lilitokana na kwamba Wizara na Ikulu vilikuwa Dar es Salaam. Ndiyo maana mara baada ya kuhamiana Dodoma ,Serikali imegawa viwanja 63 kwa Balozi na Mashirika ya Kimataifa.

Kwa msingi huo, makazi ya Balozi huwa pale ambapo Kituo cha Balozi (Post) kimewekwa. Kwa muktadha huu vituo vya mabalozi hao vipo jijini Nairobi na huko ndiko makazi yao yalipo kwa kuwa huko ndiko kuliko siti zao za kudumu.

Lakini pia kuna sababu za nchi kuamua kuwa na balozi au vituo nchi fulani na kutokuwa na vituo vya moja kwa moja nchi fulani limefafanuliwa pia katika VCDR 1961.

Kwa maana nyingine ni kwamba nchi kuwa na Balozi anayeiwakilisha nchi yake katika nchi nyingi ama zaidi ya moja ni suala la kimkataba.

Hili katika lugha ya kidiplomasia tunaita multiple accreditation, na limeelezwa kwenye ibara ya 5 na ya 6 za Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961. Kwa muktadha huu Tanzania na Kenya nitaielezea ibara ya 5 pekee.

Ibara ya 5 ibara ndogo ya kwanza na ya pili za VCDR 1961 zimefafanua haya.

1.The sending State may, after it has given due notification to the receiving States concerned, accredit a head of mission or assign any member of the diplomatic staff, as the case may be, to more than one State, unless there is express objection by any of the receiving States.

Ibara hii ya 5 (1) ndiyo inajenga msingi wa Tanzania kupokea hati za mabalozi hao. Kwa nini?

Kwa sababu, wakati ule mawasiliano ya siri baina ya Kenya na nchi hizo ambazo tumeona mabalozi wao wakiwasilisha Hati za Utambulisho yanafanyika (Tukumbuke kuwa uteuzi wa mabalozi hufanyika kwa njia ya siri kwa mawasiliano baina ya wakuu wa nchi au nchi na taasisi ama shirika la Kimataifa), baadae kuna kitendo cha nchi iliyowapokea mabalozi hao kukubali [huitwa agrement kwenye ibara ya 4 (1)] baada ya kujiridhisha, kwa muktadha huu nchi ya Kenya hapo pia hufuata nchi husika zilizotuma mabalozi hao Kenya kutuma majina hayo kwenye nchi husika ambazo wataenda kuziwakilisha kupitia kituo cha Kenya, hapa ndipo Tanzania ilipoingia.

Lakini pia kwa mujibu wa VCDR 1961 nchi hizo nyingine, yaani ukiacha nchi ya Kenya iliyowapokea mabalozi hao, nchi kama Tanzania ingeweza kuwakataa pia mabalozi hao endapo ingekuwa haijaridhishwa nao. Hivyo kitendo cha Mabalozi hao kuwasilisha Hati kinathibitisha kuwa Tanzania pia imefanya kitendo cha agrement kilichopo katika ibara ya 4 ibara ndogo ya 1 na endapo ingekataa ingekuwa imetumia ibara ndogo ya 2 ya ibara ya 4 ya VCDR 1961.

Je Balozi hizo ambazo zina vituo na makazi yao jijini Nairobi haziwezi kuweka vituo hapa Tanzania?

Kimsingi nchi hizo zinaweza kuweka vituo Tanzania na vikaongozwa na maafisa ambao huitwa charge d affaires. Hili limefafanuliwa katika ibara ya 5 ibara ya 2 ya VCDR 1961 ambayo imeeleza kama ifuatavyo:

‘If the sending State accredits a head of mission to one or more other States it may establish a
diplomatic mission headed by a chargé d’affaires ad interim in each State where the head of mission has
not his permanent seat.’

Kimsingi kuna sababu kadhaa za nchi kutokuwa na uwakilishi wa moja kwa moja na badala yake kutumia multiple accreditation, sababu hizi zinaweza kuwa, sababu za kiuchumi, kibajeti, usalama na historia.

Ifahamike pia kuwa asilimia kubwa ya mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje wanaiwakilisha nchi yetu katika nchi zaidi ya moja na taasisi zaidi ya moja kwa maana ya multiple accreditation.

Kwa hiyo hakuna shida yoyote kwa Mabalozi hao kuwasilisha Hati zao za Utambulisho Tanzania huku vituo vyao vya kudumu vikiwa jijini Nairobi, Kenya.

Asanteni.

Wenu:

Abbas Mwalimu (Facebook|Instagram|Twitter).

+255 719 258 484

Uwanja wa Diplomasia (Facebook|WhatsApp).

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %