2 0
Read Time:3 Minute, 5 Second

George Michael Uledi.
Kyela,Mbeya!
Septemba 31,2021.

Moja ya kitu ambacho lazima tukipe jicho la tatu kwa sasa kama Taifa ni uwepo wa askari wa kila aina mitaani kwetu ambao wamefuzu mafunzo ya ujuzi wa kila aina lakini pia wengi hawana kazi maalum za kufanya za kuwaingizia kipato cha kuendesha maisha.

Kiusalama suala hili halipaswi kupuuzwa hata kwa dakika moja hasa na Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na vyombo vyake vya ulinzi na usalama hasa vyombo vya siri!Hakuna askari mtii hasa anapokuwa na njaa!

Lazima kama Taifa tuanze kufikilia nje ya boksi ya jinsi ya ‘kuwacontain” askari wetu tunawafukuza kwa makosa mbalimbali majeshini na labda makosa mengine yalipaswa kuwa ya kuonywa tu lakini tunaishia kuwafukuza na kuwajaza mitaani!

Kwa mtazamo wa haraka haraka tunaweza kudhani inasaidia kujenga nidhamu ndani ya majeshi yetu lakini inaweza ikawa tunatengeneza mzigo mkubwa kwa Taifa hasa katika nyanja ya ulinzi na Usalama!”vihatarisha amani”.

NINI KINATOKEA MPAKA MAKOMANDO WANAJAZANA MTAANI?

Komando kwa tafsiri isiyo rasmi ni askari aliyepitia mafunzo maalum na ya ziada”special force” ya kuweza kumkabili adui katika mazingira magumu na ana uwezo wa kuingia katika eneo la adui bila kujulikana na kumthibiti.

Uwezo wa komando wa kutekeleza majukumu anayopewa na Kamanda wake ni wa ufanisi na usahihi wa hali ya juu sana na haujawahi kuwa wa kutiliwa shaka.Kwa kifupi komando ni Askari Jeshi aliyefudhu mafunzo ya hatari zaidi kuliko mafunzo yoyote jeshini kwahiyo tunapoongelea komando tunaongelea mtu hatari,makini,sugu na mtu mwenye mbinu za ziada za medani”Initiatives”.

Ni hatari sana kwa Taifa kuwa na utitiri wa watu hawa mitaani bila shughuli maalum za kufanya.Katika miaka ya karibuni nimeshuhudia wimbi kubwa la Askari hasa wa JWTZ wakilanda mitaani kwa sababu mbalimbali moja wapo ikiwa ni kufukuzwa kazini!

Wapo askari wengi waliopita katika mafuzo ya viwango mbalimbali kama (i)Komando (ii)Ofisa kadeti,(iii)mafunzo ya askari wa chini”NCO’s” bila kuwasahau vijana wa (iv)JKT ambao wamezagaa mitaani!Wengine waliondolewa jeshini kwa sababu ambazo zingeweza kuvumilika!

Mfano,unamfukuzaje Askari kwa kosa la kuchelewa kurudi kambini kwa lisaa limoja?Askari ambaye umemweka monduli,Arusha kwa mfano, kwa zaidi ya mwaka mmoja wa mafunzo ya “jasho na damu” na kumpa kila aina ya mafunzo ya juu ya jeshi?Kuna watu nawajua ambayo wapo mtaani kwa sababu tu walichelewa kurudi kambini kwa lisaa limoja,kozi ikaishia hapo na kutelekezwa mtaani!TPDF lazima tubadilike!

Hivyo hivyo timua timua imeendelea katika vyombo vingine vya ulinzi na usalama hivyo kuifanya Nchi kuwa na askari wa kila aina ya mafunzo mitaani!Hii inaweza kuwa fursa kwa makundi ya watu wasiotutakia mema kama ambavyo matukio ya hivi karibuni yamebainika!

NINI TUNAPASWA KUFANYA KWA SASA KAMA TAIFA?

Uwepo wa askari wengi mitaani hasa makomando ambao mimi mwenyewe nawajua unanitia shaka hasa katika kulinda usalama na amani ya Taifa.Ni hatari makomando hawa wakiendelea kuwa mitaani bila”kuwamonitor” na kujua wanafanya nini!Lazima tuchukue hatua sasa!

kuna ulazima na uharaka kwa Serikali yangu ya CCM kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama kufanya sensa ili kujua idadi ya watu wa aina hii haraka!

Matukio ya karibuni ya askari wetu wenye mafunzo ya hali ya juu”komando” kuhusishwa na matukio yenye kuhatarisha usalama wa Taifa iwe kengele ya tahadhari kwetu kama Taifa!Hatupaswi kuona matukio haya kama ya matukio ya kawaida!

Nadhani tunatakiwa tuanze kuwaza pamoja kama Taifa jinsi gani ya kukabili suala ili ambalo mbeleni linaweza kuja kuwa tishio la amani na usalama wa Taifa!

Mwandishi ni kijana wa CCM,Ofisa wa zamani,Idara ya Habari -Maelezo,Ofisa Mwanafunzi wa zamani,Chuo cha Maofisa wa Jeshi Monduli Arusha,Mhadhiri wa zamani Vyuo Vikuu vya Tumaini Iringa & Saut na Mtia nia Ubunge Jimbo la Kyela 2020.

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %