WU®
Leo tarehe 03 Desemba 2021 Mhe. Balozi Mohamed Mtonga Kamishna Jenerali wa Banda la Tanzania akiwa na Bi. Getrude Ng’weshemi kutoka TanTrade, Mkurugenzi wa banda hilo katika Maonesho ya Expo 2020 Dubai wamemkaribisha Mhe. Job Ndugai Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiambatana na ujumbe wake.
Mara alipowasilili, Mhe. Job Ndugai alikaa kikao na watumishi wanaowakilisha Taasisi za sekta mbalimbali zinazoshiriki kwenye Maonesho ya Dunia ya Expo 2020 Dubai. Wawakilishi hao wanatoka taasisi za: Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Pamoja na Maafisa wa Ubalozi wa Tanzania Abu Dhabi, UAE.
Katika kikao hicho Mhe. Job Ndugai alipokea taarifa iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Banda la Tanzania Bi. Getrude Ng’weshemi ambapo alieleza hali halisi ya ushiriki wa Tanzania mpaka sasa katika maonyesho hayo. Taarifa iliweka bayana mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizopo na hatua zinazochukuliwa katika kuimarisha ushiriki wa dhati kwa Tanzania ili nchi iwe na manufaa kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Job Ndugai ameonyesha kufurahishwa na hatua ya ushiriki iliyofikiwa tangu maonesho haya yaanze tarehe 01 Oktoba 2021. Amesema, ‘’Nawapongeza wote mliopo hapa kuiwakilisha Tanzania mkiwa mmetoka katika Sekta mbalimbali. Hatua hii ni muhimu kwetu kama nchi na ninawasihi tuendelee kushiriki kwa kujituma na kwa kutekeleza mikakati tuliyojiwekea kama nchi ili ulimwengu uweze kujua ni nini hasa Tanzania imeleta kwenye maonesho haya. Tumebarikiwa na upekee mkubwa katika vitu vingi lakini pia tuna vipaumbele vya kitaifa na hili ni jukumu letu sote kutekeleza tukishirikiana bega kwa bega na wenzetu walioko nyumbani Tanzania.
Napenda pia kuwafikishia salama za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye anatambua ushiriki wa nchi katika maonesho haya ya dunia. Wataalam mjipange na kujifunza kutoka kwa wenzetu ili kufahamu nini kinachosababisha wenzetu waende kwa kasi kimaendeleo na kisha mtoe taarifa yenye mapendekezo kwa serikali ambayo italishauri bunge kuondoa sheria zinazokwamisha au kuongeza sheria zitakazosaidia kupiga hatua kimaendeleo. Mategemeo yetu ni makubwa hivyo tuhakikishe tunanaiwakilisha vema Tanzania hapa Dubai na tuipeperushe bendera yetu ulimwenguni”.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Dubai ‘Diaspora’ ambao walishiriki katika Siku maalum ya Uzinduzi wa Juma la ‘’ Ijue Tanzania’’ katika kusherekea Siku ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika. Wakiwa kama wawakilishi wa kwanza wa Watanzania hapa Dubai, wamejitokeza na kumhakikishia Spika kuunga mkono jitidaha za ushiriki wa Tanzania katika maonesho haya ya Expo 2020 Dubai.
Baada ya kikao hicho Mhe. Job Ndugai pamoja na wajumbe alioambatana nao walipita kwenye banda la Tanzania wakiongozwa na Mkurugenzi wa Banda la Tanzania Bi. Getrude Ng’weshemi ambapo wajumbe waliweza kujionea maudhui ya vipaumbele vinavyoitangaza Tanzania katika maonesho ya Expo 2020 Dubai. Asilimia kubwa ya banda limesheheni maudhui yanayoitangaza Tanzania kupitia Sekta za Utalii, Madini, Kilimo, Nishati, Utamaduni, Viwanda na Uwekezaji.
Vilevile Mhe. Job Ndugai alipata wasaa wa kutembelea mabanda ya nchi za Thailand na Bostwana kwa lengo la kujifunza kutoka nchi hizo na kupata uzoefu wao wa kushiriki kwenye maonesho makubwa ulimweguni kama haya.
Hii ni fursa ya kipekee kwa nchi kujifunza, kupata uzoefu, kujitangaza na kukuza ushirikiano wa kidiplomasia na nchi nyingi za Bara la Arika na dunia kwa ujumla. Ushiriki huu unategemewa kuibua fursa mbalimbali ulimwenguni za kiuwekezaji na maendeleo endelevu kwani katika kuunganisha fikra kuna uhakika wa kutatua changamoto na kukaribisha dunia yenye mafanikio.