WU®Media PRODUCTION LIMITED
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema itaendelea kuwainua watoto wa kike ili kujikita zaidi katika masomo ya sayansi.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Riziki Pembe Juma aliyasema hayo katika ufungaji wa uzinduzi wa program ya kuwawezesha wasichana kusoma na kushiriki katika masuala ya teknologia na kidijital hafla ambayo ilifanyika katika ukumbi wa Hyatt Regency jijini Dar es salam.
Amesema serikali imekuwa ikichukua jitihada katika kuwainua watoto hao kwa kuandaa program mbalimbali ndani ya skuli na maeneo mengine ili kumfanya mtoto wa kike anasoma masomo ya sayansi.
Waziri Riziki anabainisha kwamba mtoto wa kike ana umuhimu mkubwa katika taifa la Tanzania kwani ana upeo mkubwa katika mambo mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Amesema Zanzibar ina wataalamu wanawake waliobobea katika fani mbalimbali hatua ambayo inaonesha kwamba ukimuwezesha mtoto wa kike ni kuongeza wataalamu wengine nchini.
Amebainisha kwamba mashirikiano ya tasisi za serikali na binafsi ikiwemo tasisi ya Zanzibar milele Foundation, FAWE, SUZA, Chuo cha Teknologia Karume, vyuo vya mafunzo ya amali na wadau wengine imewezesha wasichana zaidi ya 400 katika Kambi za mafunzo Maalum ya sayansi.
Hivyo ameahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania zitaendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa huku akisisitiza kuunda timu maalum ya wataalamu kuona jambo hilo linafikiwa kwa pande zote mbili za Tanzania.
Naye Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima akizundua program hiyo amesema serikali kwa kushirikiana na UN Women pamoja na wadau wengine wa maendeleo wanatarajia kuanzisha vituo 35 vitakavyotoa mafunzo ya kidijitali kwa wasichana kupitia mradi uliojikita kuongeza ushiriki kwa watoto wa kike katika masuala ya Tehama.
Amesema awamu ya pili ya mradi huo ndio itakayoleta mpango wa kuandaa wanafunzi waliopo maskulini na wengine wote wanaopenda maendeleo ya kidijitali waweze kuendelea na mafunzo.
Aidha amesema awamu hiyo ya pili imegundulika kwamba katika maendeleo ambayo dunia inakwenda nayo imeonekana wanawake wameachwa nyuma hivyo katika masuala ya kizazi cha usawa wa kijinsia kitamfanya mwanamke asiachwe nyuma na kuhakikisha anapewa kipaumbele katika nyanja zote hasa katika maendeleo ya sayansi ya kidijitali.
Jumla ya Nchi 11 zitafaidika na program hiyo Tanzania ikiwa ni nchi moja wapo.
Imeandaliwa na kitengo cha Habari Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto.