
WU® MediaPRODUCTION LIMITED
AMPA TUZO NA KUWANASIHI WASANII WASIPARURANE WAPULIZANE. MAMBO MA 8 YA TUKIO LA THE DREAM CONCERT KWA VIJANA
Anaaandika PhD Dkt.Ahmad Sovu
“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania-kazi iendelee“
Tarehe 31, Mei, 2022 Rais Samia Suluhu Hassan alifungua tamasha la msanii Joseph Mbilinyi maarufu Mr.Sugu katika ukumbi wa Serena jijini Dar es Salaam.
Mr.Sugu alifanya maadhimisho ya kutimiza miaka 30 ya kazi yake ya uimbaji wa muziki wa kufoka foka, yaani Hiphop hapa nyumbani Tanzania. Hafla hiyo adhimu ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wasanii wakongwe wa muziki huo akiwamo Inspekta Haroon maarufu ‘Babu’, Ambwene Yesaya ‘AY’, Mheshimiwa Mwana FA, Mheshimiwa Nikki wa pili, Joe Makini, Lady Jay D ‘Jide’, Weusi na wasanii wengine lukuki.
Rais Samia Suluhu Hassan ametajwa kuweka historia kwa kuhudhuria kwake katika tukio hilo. Mkongwe wa masuala ya burudani na habari nchini, ndugu Joseph Kusaga alisema “Mama unaunganisha watu wa Taifa lote na unatupa furaha na faraja” anasema Kusaga hakumbuki lini tukio la namna ile limewahi kuhudhuriwa na Rais. anasema masuala haya yalikuwa yanaonekana ni ya kihuni huni lakini mama umetuunganisha, viongozi wa siasa wote tuko hapa.Asante.
Katika tukio lile, kupitia wazungumzaji mbalimbali akiwamo Mheshimiwa Rais Samia na hata Mr.Sugu nimemaizi kuna mambo kadhaa ya kujifunza mahsusi kwa vijana, wasanii wenyewe na jamii kwa jumla kama ifuatavyo:-
Mosi, uthubutu, ujasiri na uvumilivu ni nyenzo muhimu sana kwa mtu yeyote ili aweze kutimiza ndoto. Kila mmoja katika waliopata fursa ya kusema katika tamasha hilo alidhihirisha kuwa Mr.Sugu alikuwa ni mtu mwe Uthubutu na jasiri. Mheshimiwa Rais Samia alimuelezea Sugu bayana kuwa ni mtu jasiri na mvumilivu kwani ukiangalia historia yake na ilivyoelezwa na rafiki zake unamuona hatua alizozipitia. Sugu mwenyewe alithibitisha hayo kwa kusema kuwa alikuwa akitoka Mbagala wakati huo kwa mguu hadi Posta kwenda kurekodi au kushiriki matamasha Kwa hakika hapa pana funzo kubwa sana kwa vijana wetu. Kuwa maisha ni mapambano. Ukiona vyaelea ujue vimeundwa.
Pili, umuhimu wa kutambua kipaji chako
Kulingana na maelezo ya ndugu Nehemiah rafiki wa karibu wa Sugu ambaye walisoma pamoja naye anasema, Sugu alipenda muziki tangu wakiwa nae shuleni. Hata walimu walipomuona mtukutu akahamishwa shule bado hakuacha muziki. Leo tunashuhudia muziki umemfanya Sugu kutoka mtaani hadi Bungeni na kupata mafanikio makubwa sana. Hapa pana mafunzo muhimu sana hasa kuweza kubaini kipaji chako na kusimamia hadi ukafikia mafanikio. Nitumie fursa hii kuikumbusha jamii hususan wazazi na walimu wenzangu tusivize vipaji vya watoto wetu tuwasaidie na tuwaelekeze ipasavyo. Kwa mujibu wa mtaalamu Prof.Howard Gardner katika nadharia yake iitwayo vipaji lukuki (multiple intelligence) anasema binadamu huzaliwa na vipawa mbalimbali moja ya kipawa hicho ni muziki (musical intelligent). Mzazi hata kama unatamani mtoto wako asiimbe muziki wa kidunia muongoze kwenye kutumia sauti yake vizuri katika mambo unayoyaamini ni ya heri. Mathalan, kuimba mashairi, kaswida, nasheed, injili, kwaya n.k lakini usivize na kuuwa kipaji cha mtoto hata kama si hiki cha sauti.
Tatu, kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi Ni ukweli uliodhahiri kuwa Sugu amekuwa mchapakazi wa kazi aipendayo kwa bidii. Haya yanadhihirishwa katika kazi zake. Ubunge alidumu kwa miaka 10 na katika muziki hadi hivi leo bado anafanya vema. Ni muhimu kufanya kazi zaidi ili kufikia kilele cha mafanikio.
Nne, kutumia fursa kadri iwezekanavyo au ipatikanapo Simulizi ya nguli wa muziki ndugu Kitime inadhihirisha hili kwa Mr.Sugu. Mzee Kitime anasema mwaka 1995 walianzisha kampuni ya kupata waimbaji. Anasema kalikuja kabwana mdogo shati refu sana. Bwana mdogo huyo si mwingine alikuwa ni huyu Mr.Sugu Joseph Mbilinyi aliyetukusanya hapa. Mheshimiwa Rais Samia Suluhu anasema Sugu aliponialika siku aliyopanga sikuwa na nafasi nikamwambia nikupe mwakilishi au usogeze mbele. Sugu alisogeza tarehe mbele na hatimaye anaadhimisha miaka yake siasa na muziki mgeni rasmi akiwa ni Mheshimiwa Rais. Huku ndio kutumia fursa tunakojifunza kwa Sugu. Vijana tunapaswa kila mlango wa fursa kwanza tuutafute na tukiupata tusiufanyie mchezo. Tuutumie vilivyo.
Tano, kupenda mafanikio ya wenzako Sugu mbali ya kuwa miongoni mwa waasisi wa muziki huu. Amekuwa akipenda mafanikio ya wenzake. Mwenyewe anasema bado ‘taita’ sana na hajalosti ingawa anafurahia sana maendeleo ya vijana mbalimbali waliowika na kung’ara katika tasnia yao hiyo ya muziki. Hii ni funzo kubwa kwa vijana sisi wa sasa kwani mafanikio ya mwenzio yafurahie na iwe chachu ya kusonga mbele. Asemavyo Rais Samia wasanii msiparurane mpulizane kila mmoja na kipaji chake. Ajitahidi kukionesha ili kufikia mafanikio. Vijana na tuache unaa na kusagiana haisaidii. Tujifunze kwa Sugu.
Sita, kukumbuka ulikotoka Sugu katika maadhimisho yake ya miaka 30 unaona namna alivyowaalika watu mbalimbali ambao kwa namna moja amehangaika nao katika maisha hadi kufikia hatua hiyo. Tumeshuhudia akiwa na rafiki zake aliosoma nao tangu shule. Shukrani zake kwa kina mzee Kitime, Mzee Kinana na kina General Ulimwengu ni ushahidi tosha kuwa anakumbuka alikotoka. Somo la kujifunza hapa ni umuhimu wa vijana kukumbuka ulipo na utokako. Sio kuwa katika mafanikio fulani basi unajongomea na kujiona ulifika uliko mwenyewe. Hili lilikolezwa na Mheshimiwa Rais Samia kuwa hata wao katika siasa anasema wengi huanza na ‘humble beginning’ mwanzo wenye utiifu ila baadaye watu hubadilika na kusahau walikotoka.
Nasaha za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Mheshimiwa Rais Samia Suluhu mbali ya kuzungumzia namna serikali yake ilivyopiga hatua kubwa katika tasnia ya wasanii ikiwamo kutoa Fedha zaidi ya Bilioni 1 katika mfuko wa sanaa, kujenga viwanja vya michezo na sanaa na pia kuandaa tunzo mbalimbali. Pia, alitoa nasaha zifuatazo:
Saba, kuzingatia mila na desturi zetu Mheshimiwa Samia aliwanasihi wasanii kuwa pamoja na kuburudisha ni lazima tutambue kuwa ipo mipaka ambayo hatuwezi kuivuka na tuzingatie maadili ili kufanya muziki wenu uheshimike. Kwa mfano, hapa mmeimba lakini nimesikia neno Kilimanjaro wala huoni udhia kusikiliza.
Nane, msiparurane mpulizane Mheshimiwa Rais Samia amewataka wasanii kupendana, kushirikiana na kusaidiana. Wanasanii mna mchango mkubwa sana acheni kuparurana pulizaneni na kila mmoja aoneshe kipaji chake.
Mwisho alimpongeza Sugu kwa kuandika kitabu kihusucho maisha yake mwenyewe. Ni watu wachache sana ambao wanapenda kujiandikia historia yao wenyewe na wakawa wawazi kama wewe. Alisema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Natoa kongole sana kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuthamini mchango wa muziki wa Hiphop nchini na kwa Bwana Joseph Mbilinyi katika sanaa na kuzalisha ajira kwa vijana na watu wengine.
Vilevile, nampongeza Mheshimiwa Joseph Mbilinyi maarufu Mr.Sugu, kwani wapo madaktari na maprofesa ambao wamefikia viwango hivyo vya juu vya kitaaluma kwa kufanya tafiti kutoka katika nyimbo za Sugu na wasanii mbalimbali.
Pia, twawapongeza Waziri Mchengerwa na watendaji wake wa wizara ya sanaa na utamaduni. Kwa hakika wamekuwa wakijali na kufuatilia maslahi ya wasanii kwa kiasi kikubwa.
Mwandishi ni Mhadhiri na Mshititi kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kigamboni DSM.
0713400079
sovu82@gmail.com








