
WU® MediaPRODUCTION LIMITED
KALAMU YA MKALI
mkali@live.co.uk.
HAYA NI MATUMIZI YA KIHUJUMA YA FEDHA ZA UMMA.

Jamani hebu tutazame kiasi gani cha fedha zitafujwa kupitia hii Kamati.
1) Hao wajumbe 200 kila mmoja atalipwa ‘allowance – per diem) ya shilingi 250,000/= kila siku. (200 ×250,000 = 50,000,000).
2) Shilingi milioni hamsini zitakuwa zinatumika kila siku ya uhai wa hiyo Kamati.
3) Hii Kamati itadumu kwa muhula wa miezi minne. Tuzidishe hiyo milioni hamsini mara siku 120, (50,000,000 × 120 = 6,000,000,000/=). Hapo hatujaweka gharama za hivyo vitendea kazi: magari na Laptops. Kuharibu kiasi hiki cha fedha kuchunguza suala ambalo lilitakiwa kufutwa bila uchunguzi ni uhujumu uchumi.
4) Ni dhahiri kuwa Mh.Mwigulu amepwaya kwenye wadhifa wake. Dalili zote zinaonyesha kuwa kazi imemshinda. Upeo huu wa wananchi kuchukia uamuzi wa Serikali yao (inavyojiri katika suala hili la tozo) haujapata kutokea tangu uhuru. Ni sawa kabisa huyu Mheshimiwa aidha apumzishwe au ajipumzishe kwa kujiuzuru.
5) Ni kweli kuwa huo uamuzi ulipitia Bungeni, lakini Rais hawezi kuwatumbua wabunge wote waliopitisha bili iliyozaa hii tozo. Lakini Kiongozi wa juu muhusika kuwajibika au kuwajibishwa ni sawa.
6) Katika muda wa miaka mitano, hayupo Rais, tangu uhuru, ambaye alileta huduma na kujenga miradi mikubwa kwa nchi yetu kama alivyofanya Hayati Magufuli. Lakini alitekeleza hayo bila tozo yoyote.
7) Aidha, hayati Mwalimu Julius Nyerere alituachia mashirika ya umma hai 450, alitoa bure huduma za afya na elimu pamoja na ruzuku kwa wakulima. Fauka ya hayo alisaidia kimatendo ukombozi wa bara la Afrika kuliko Rais mwingine yoyote; na upeo wa utumiaji (exploitation of our natural resources) wa raslimali zetu wakati ule ulikuwa ni mdogo kuliko leo.
Na yeye pia hakutumia tozo. Huu umuhimu wa tozo leo, unaletwa na nini?
8) Kadhalika, hii tozo ni sawa kabisa na “Poll tax’ ya zama za kikoloni; ambayo Mwalimu Nyerere aliifuta mwaka 1968 kwa sababu ilikuwa ni ya kisheria lakini si ya haki.
9) Tuwe tunajikumbusha kuwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Margaret Thatcher, alilazimishwa na Chama chake ajiuzuru baada ya kuleta tozo au “Poll tax”; tozo ambayo ingalikifanya Chama cha Conservative kisishinde uchaguzi uliokuwa unakuja. Aliyechukuwa nafasi yake John Major, alifutilia mbali hiyo tozo kabla ya uchaguzi.
USHAURU.
Hii tozo ifutwe bila kuundwa Kamati ya aina yoyote. Tozo hii inajenga chuki kali kati ya wananchi na Viongozi wa nchi yetu. Haileti maana Taifa kutumia Shilingi bilioni sita, kuchunguza kama wananchi waendelee kunyanyaswa na hii tozo ambayo si ya haki.
Tanzania tusikubali kuvuruga amani yetu ili kuhifadhi uso au nyuso za watu wachache waliobuni tozo kandamizi, tozo isiyo ya haki.
mkali@live.co.uk.
13/09/2022.








