Lazima Uishinde Hofu Ya Kushindwa
Na Paul R.K Mashauri
Hofu ya kushindwa ni hisia halisi ambayo watu wengi huangaika nayo hata unaodhani wanajiamini. Unahitaji kuwa na mtazamo chanya kama wa rafiki yangu Mandonga ili uishinde hofu ya kushindwa. Kwa sababu inaweza kukuzuia kujaribu kitu kipya au ukachukua tahadhari ambayo haipo. Nakumbuka katika mtihani wangu wa kidato cha sita nilipata homa ya ghafla kwa kuogopa kushindwa hesabu. Cha ajabu matokeo yalipokuja nilifaulu.
Hii ina maana 80% ya hofu nyingi tulizonazo hazitotokea. Unakumbuka tuliambiwa mwaka 2000 ni mwisho wa dunia? Na kwamba kompyuta zote zitazima? Mbona tupo tunadunda?Tunaumiza nafsi zetu bure. Na hata idadi kubwa ya hofu ulizonazo hivi sasa juu ya kipato chako au watoto wako au chochote kile hazitotokea.
Kimsingi, chanzo kikuu cha hofu ya kushindwa ni hisia za aibu, hasara, hofu ya kupoteza muda, fedha, heshima nk. Lakini ukichunguza kwa kina, hofu nyingi zinatokana na jamii iliyotuzunguka. Jamii ambayo ukishindwa unaonekana kama una mkosi au laana au umerogwa au mbumbumb au Mungu anakuadhibu. Tena unajadiliwa kwenye makundi ya WhatsApp na familia inasema umeitia aibu.
Hizi zote ni hofu za kweli na zinazoeleweka, lakini ni muhimu kukumbuka kuwa kushindwa iwe ni mtihani, ndoa, biashara, kazi na hata maisha kunaweza kukakubadilisha ukawa bora zaidi. Kumbuka CocaCola iligunduliwa kimakosa. Mgunduzi alishindwa kupata alichokuwa anatafuta lakini katika kushindwa kwake akagundua CocaCola. Leo tunaangalia kombe la dunia kwa nguvu ya Cocacola.
Ndani ya kushindwa na kukosea kuna nguvu ya kujifunza. Mwandishi John Maxwell anaita hiyo kushindwa kwa kwenda mbele “Failing Foward”. Inaweza kuwa kichocheo cha kukusaidia kukua na kukuza ujuzi wako na kujiamini. Unapokabiliwa na kushindwa, ni muhimu kuwa na mtazamo chanya na kuutumia kama fursa ya kujifunza na kukua.
Kwa nchi kama Tanzania hii ni muhimu sana kuzingatia. Kwa sababu hapa kwetu wanaoshindwa wanapewa majina; kilaza, aliyefulia, kiazi, mgaagaa nk.
Lakini ukiendekeza mawazo hasi ya jamii hutofika popote katika maisha. Zingatia kile unachoweza kuchukua kutoka katika kushindwa na utumie kwa faida yako. Mengine weka pamba masikioni. Kwa sababu haohao wanaokusimanga, ukifanikiwa wanakuwa wa kwanza kulalamika hupokei simu zao.
Wosia wangu kwako ni huu; Kushindwa kunaweza kuwa jambo gumu kupitia, lakini pia kunaweza kuwa somo la nguvu katika uthabiti na ustahimilivu. Huwezi kuwa na uthubutu au roho ngumu kama hujawahi kushindwa. Na usiruhusu hofu ya kushindwa ikuzuie kujaribu tena na tena na tena kama George Washington aliyeshindwa mara nyingi sana kabla hajawa Rais wa Marekani.
Oooh nimekumbuka kitu. Katika mzunguko wa kwanza wa kombe la dunia mwaka 2022, Argentina walipoteza mechi dhidi ya Saudi Arabia. Wengi waliwacheka na kuwasimanga. Lakini hebu angalia mtazamo wao chanya. Wakachukua kushindwa kwao kama funzo. Leo Argentina wameingia nusu fainali ya kombe la dunia Hii inatufundisha nini? Somo ni hilohilo, kwamba hakuna aliyefanikiwa ambaye hajawahi kushindwa.
Paul R.K Mashauri
mfanyabiashara na mwandishi
WhatsApp: +255 754 557037
info@paulmashauri.com
www.paulmashauri.com