0 0
Read Time:4 Minute, 15 Second

MAREKANI WAMEKOSEA WAPI?

Na Abbas Mwalimu

Jumatatu 30 Januari 2023.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax alikutana na Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi na Mashirika ya Kimataifa yaliyopo nchini Tanzania, jijini Dodoma.

Katika Mkutano huo Waziri Tax alieleza sababu kuu nne za kukutana na Mabalozi hao.

Kimsingi sababu hizo zinatokana na taarifa ya tahadhari ya hatari iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani Jumatano tarehe 25 Januari 2023. Taarifa hiyo ilifuatiwa na taarifa iliyokuja kutolewa na Shirika la Ndege la Uholanzi-KLM Ijumaa tarehe 27 Januari 2023.

Katika hotuba yake Waziri Tax alitumia lugha ya kidiplomasia kuonesha makosa yaliyofanywa na ubalozi wa Marekani licha ya kutoutaja ubalozi huo kwa kuzingatia taratibu za Diplomasia zinavyoongoza.

Hivyo, makala hii inalenga kubainisha makosa yalilofanywa na Ubalozi wa Marekani ambayo Waziri alitumia lugha ya kidiplomasia kuyaeleza.

Tukumbuke kuwa Balozi zinaendeshwa kwa mujibu wa Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 unaohusu Uhusiano wa Kidiplomasia.

Katika mkataba huo kuna Ibara ambazo zinafafanua namna gani Balozi zitafanya shughuli zao.

Makala hii itaangazia ibara mbili za Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 na moja ya Mkataba wa Montevideo wa mwaka 1933 ili kubainisha makosa yaliyofanywa na Ubalozi wa Marekani.

Ibara ya Tatu Ibara ndogo ya Kwanza kifungu ‘d’ cha Mkataba wa mwaka 1961 kinasomeka hivi:

3 (1, d) Ascertaining by all lawful means conditions and developments in the receiving State, and reporting thereon to the Government of the sending State;

Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi ni kwamba mkataba unaelekeza mambo mawili:

Mosi kuenenda na mazingira yote yaliyomo katika nchi ambayo ubalozi upo. Katika muktadha huu ni kuenenda na mazingira yote yaliyopo nchini Tanzania.

Pili, kutoa taarifa kwa nchi iliyoutuma ubalozi huo. Hapa ni kwamba Ubalozi wa Marekani una wajibu wa kutoa taarifa ya yanayojiri Tanzania kwa nchi ya Marekani. Lakini je ni kwa utaratibu upi? Tutakuja kuona hapo baadae.

Kosa la kwanza lipo hapa, kwamba kuenenda na mazingira ni pamoja na kuheshimu sheria za nchi ambapo ubalozi wa nchi hiyo upo. Kwa maana hiyo walitakiwa kuheshimu sheria za Tanzania.

Hii ikiwa na maana kwamba licha ya wao kuwa na wajibu wa kutoa taarifa ya yanayajiri lakini pia wanapaswa kuzingatia sheria za Tanzania.

Je sheria za Tanzania zinasemaje? Kwa Sheria za Tanzania Jeshi la Polisi ndilo lenye wajibu wa kulinda usalama wa raia na mali zao kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama. Hili ni kosa la pili la Ubalozi wa Marekani.

Kosa hili linakujaje? Labda hapo tujiulize. Kosa hili linatokana na Marekani ama kushindwa kutambua Sheria za Kimataifa ama kwa makusudi.

Tukitazama Mkataba wa Montevideo wa mwaka 1933 unaohusu Haki na Wajibu wa Nchi tunaweza kuona kosa la pili la Marekani.

Ibara ya 9 ya Mkataba wa Montevideo inaeleza kama ifuatavyo:

The jurisdiction of states within the limits of national territory applies to all the inhabitants. Nationals and foreigners are under the same protection of the law and the national authorities and the foreigners may not claim rights other or more extensive than those of the nationals.

Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi ni kwamba:

Wajibu wa nchi ndani ya mipaka yake huwahusu watu wote, wageni na raia wa nchi hiyo.

Raia wa nchi husika (katika muktadha huu wa Tanzania) na wa kigeni (wa Marekani na wa nchi nyingine waliopo Tanzania) wanalindwa na sheria moja za Tanzania na Mamlaka za nchi (Tanzania).

Na kwamba raia wa kigeni (Marekani) hawawezi kudai haki zaidi ya zile wanazopata raia wa nchi husika (Tanzania).

Kwa mujibu wa Ibara hii ya 9 tunaona kuwa raia wa Marekani waliopo Tanzania wanalindwa na Sheria za Tanzania na chombo kinachowalinda ni Jeshi la Polisi. Hapa ndipo lilipokuwapo kosa la pili.

Kosa la tatu la Ubalozi wa Marekani ni kutofuata njia sahihi za Mawasiliano.

Ibara ya 27 ya Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 inaelekeza balozi kufanya nawasiliano na nchi zilizowatuma.

Lakini ibara hiyo inasisitiza kwa kuweka mkazo “by all appropriate means.” kwa maana ya kufuata njia zote sahihi.

Katika hili kosa la Marekani linakuja hivi, Balozi zina njia zake za mawasiliano kama ilivyoainishwa kwenye ibara ya 27 ya Mkataba wa Vienna.

Katika muktadha huu ni kwamba Marekani ina wajibu wa moja kwa moja wa kuwasiliana na Serikali ya Marekani kwa njia za siri.

Pili ina wajibu wa kuwasiliana na raia wa Marekani waishio Tanzania pasina kuhusisha raia wa nchi nyingine kwa sababu jukumu la Ubalozi wa Marekani linawahusu raia wa Marekani tu na si raia wa nchi nyingine.

Hivyo ilitarajiwa kwamba Ubalozi huo ungewasiliana na raia wake kwa ‘appropriate means’ ikiwamo kutumia Jumuiya za Wamarekani waishio Tanzania au kuwatumia taarifa katika anwani pepe za wamarekani waishio Tanzania (Sitaki kuamini kuwa hawana e-mail zao).

Zaidi Ubalozi wa Marekani ulipaswa kuwasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania na hapo Wizara ya Mambo ya Nje ingewasiliana na Wizara ya Mambi ya Ndani ya Nchi nayo Wizara ya Mambo ya Ndani kulitaarifu Jeshi la Polisi.

Hivyo kimsingi hayo ndiyo makosa yaliyofanywa na Marekani na kuzua taharuki.

Abbas Mwalimu
(Facebook|Instagram|Twitter| Clubhouse)

+255 719 258 484

Uwanja wa Diplomasia
(Facebook|WhatsApp)

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %