0 0
Read Time:1 Minute, 42 Second


DAR ES SALAAM.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimeahidi kushirikiana katika sekta za kimkakati hususani kilimo, pamoja na biashara na uwekezaji kwa lengo la kukuza na kuimarisha diplomasia ya uchumi.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) katika sherehe za maadhimisho ya miaka 44 ya siku ya Taifa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na maadhimisho ya miaka 40 ya uhusiano wa kidiplomasia baina ya Iran na Tanzania zilizofanyika tarehe 10 Februari 2023 Jijini Dar es Salaam.

“Tanzania na Iran tumekuwa tukishirikiana katika maeneo mbalimbali, hadi sasa tumekuwa tukishirikiana katika sekta za elimu, afya, utalii, nishati, madini. Pia kwa sasa Irani imeonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya kilimo hasa ukizingatia kilimo ni kipaumbele cha Serikali,” alisema Dkt. Tax

Waziri Tax ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na Iran katika maeneo mapya ya kimkakati ikiwemo sekta ya kilimo ili kupata uzoefu katika maendeleo na uwekezaji wa kuifanya nchi kuwa na uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha pamoja na kuongeza viwanda.

Akielezea kuhusu biashara na uwekezaji, Dkt. Tax alisema kuwa kupitia kongamano la wafanyabiashara na wawekezaji lililofanyika Mwezi Agosti, 2022 limefungua fursa za biashara na uwekezaji. “Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuwavutia wafanyabiashara na wawekezaji wengi zaidi kuwekeza nchini,” alisema Dkt. Tax

Naye Balozi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini, Mhe. Hossein Alvandi Bahineh alisema kuwa Iran imekuwa na uhusiano wa kidiplomasia na Tanzania kwa miaka 40 hadi sasa na mataifa hayo yamekuwa yakishirikiana kijamii, kisiasa, kiuchumi na utamaduni kwa maslahi ya pande zote mbili.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Tanzania zimekuwa marafiki wa muda mrefu na itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuimarisha sekta za kilimo, elimu, afya pamoja na biashara na uwekezaji kwa maslahi ya mataifa yote mawili.

Balozi Alvandi aliongeza kuwa mazingira ya biashara kati ya Iran na Tanzania yanaridhisha kwani hadi mwaka jana 2022 biashara kati ya Iran na Tanzania iliongezeka kutoka dola milioni 20 hadi dola milioni 70.

Contact us : +39 389 85 83370
Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %