0 0
Read Time:3 Minute, 1 Second

Na, Zain
Diaspora

Washington DC

Elimu ni ufunguo wa maisha!

Tanzania ni nchi yenye raslimali na maliasili nyingi. Nchi nyingi duniani zenye utajiri wa hivyo na sio za kibepari, zinakataa uraia pacha. Ndio maana hakuna uraia pacha Arabuni, hakuna uraia pacha India na nchi nyingi za Asia hasa zile zinazoendelea kwa kasi kama Singapore, Malaysia na Indonesia. Hakuna uraia pacha China na nchi nyingi za mashariki ya mbali. Ulaya pia kuna nchi zinakataa uraia pacha.

Hata wanaodai uraia pacha wanakubali madhara ya kuwapa wageni uraia pacha na Tanzania. Na kwa kauli moja wanaomba uraia pacha kwa wazawa wa Tanzania tu. Ingawaje huwa wanajichanganya na kusema raia wa kigeni watakaotimiza vigezo wapewe uraia pacha.

Zifuatazo ni sababu kuu tatu za kuukataa uraia pacha Tanzania na kutoa Hadhi Maalumu kwa wanadiaspora wa Tanzania;

  1. Si kitu cha kuiga majirani, hasa kama wamefanya makosa.
  2. Uraia pacha hauwezi kuzuia raia wa kigeni watakaotimiza vigezo kupata uraia pacha na Tanzania, hasa kwa watakaoomba uraia pacha kwa kutumia ndoa au nasabu kwa mfano watoto au wazazi.

Sharti la kukaa nchini miaka kumi pia sio gumu kama vile wengi wanavyofikiria. Kuna raia wa kigeni hasa wawekezaji tayari wako nchini zaidi ya miaka kumi, wanaishi kwa vibali na wengine hawana vibali kabisa hasa katika maeneo ya mipaka ya Tanzania. Kuna wakimbizi, na walioingia nchini kimuziki na vishughuli shughuli vingine. Isitoshe miaka kumi sio mingi kwa hesabu za kitaifa hasa kwa wanaojali vizazi vya baadae.

Kenya ilipotoa uraia pacha mwaka 2010, kundi hili ndio lililoanza kuomba uraia pacha kabla hata ya wanadiaspora.

Hawa wawekezaji wakipata uraia pacha na Tanzania watawekeza kama wazawa wa Tanzania, na serikali itapoteza kodi zote na faida zote za uwekezaji kutoka kwao.

  1. Uraia pacha hauwezi kuzuia raia wa Tanzania wenye asili ya kigeni kuchukua uraia pacha na nchi zao za asili, au hata za ugenini. Na wakipata uraia pacha wataweza kuwapa uraia pacha ndugu, familia, jamaa hata na marafiki zao waliopo nje. Kwa sasa kundi hili nchini Tanzania lina wahindi, waarabu, wazungu, hata wachina wachina wameanza kujichomeka.

Kundi hili vilevile lina uwezo mkubwa kiuchumi, na ndio wamiliki wa mali zikiwemo ardhi, viwanda, mabenki na biashara kuu nchini. Kwa hivi sasa wengi wao wana uraia wa nje lakini ni wa siri, wakikamatwa wanaweza kufilisiwa, kufungwa jela au kufukuzwa nchini. Kuwapa uraia pacha wa kihalali ni kuwaruhusu kuchuma Tanzania na kuhamishia mali nje ya nchi bila ya kuficha chochote.

Mwisho wa siku wanadiaspora wa Tanzania wanaodai uraia pacha na Tanzania, watasababisha hasara kwa wanadiaspora wote wa Tanzania, watasababisha hasara kwa wananchi wa Tanzania hasa pale ardhi yao, biashara na nafasi za kazi zitakapochukuliwa na raia wa kigeni, na wataisababishia serikali hasara ya kupoteza baadhi ya wawekezaji wake ambao ni raia wa kigeni pindi watakapotimiza vigezo vya kuchukua uraia pacha na Tanzania.

Yote hayo ni uchumi tu unaogomba!

Ni jana tu nimezungumza na dada mmoja wa kikenya aishie hapa Marekani, akaniambia alitumia milioni nne na nusu hela za Kenya kununua shamba la heka moja kwao. Tena alifanya haraka sana asije kupoteza hiyo bahati. Milioni nne na nusu za Kenya ni milioni 85 na laki tano za Tanzania. Ukiamua kuzitumia kununua shamba kwa bei ya heka moja kwa laki tano, utanunua heka 171 Tanzania wakati mkenya kanununua heka moja kwao.

Bila ya kusahau uraia pacha hautawasaidia chochote wanadiaspora wa Tanzania wenye uraia katika nchi zisizoruhusu uraia pacha kama China, India, Singapore, Japan, Holland, Oman, Yemen, Saudi Arabia, Qatar, Dubai na kadhalika.

HADHI MAALUMU INA FAIDA ZILEZILE ZA URAIA PACHA NA INAEPUKA MADHARA YA URAIA PACHA KWA WANADIASPORA, WANANCHI WA WATANZANIA, SERIKALI NA TAIFA KWA UJUMLA

Ambae hataelewa hii awatafute wale wapiga manyanga wa Harmonize kwenye wimbo wa I am single wampigie manyanga!

Zain
Washington DC

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %