0 0
Read Time:5 Minute, 32 Second

WU® MEDIA

Rome.

Mzee Rukhsa: Kutoka kusaka ushekhe mpaka kupata urais

“Leo nina miaka karibu 94, sina siku nyingi za kuiacha dunia. Sitaki niende huko napoenda na aibu nyuma yangu.

Maisha ya mwanadamu ni hadithi tu hapa ulimwenguni, basi ewe ndugu yangu kuwa hadithi nzuri kwa hao watakaosimuliwa…” hii ni moja ya nukuu maarufu zaidi ya hayati Ali Hassan Mwinyi katika miaka ya hivi karibuni.

Hadithi ya maisha ya Rais mstaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi maarufu Mzee Rukhsa aliyehudumu madarakani kwa miaka 10 kutoka mwaka 1985 mpaka 1995 imetamatika Alhamis ya tarehe 29, Februari 2024.

Ni hadithi ndefu ya miaka 98. Hadithi ya maisha yake ilianza kuandikwa Mei 8 mwaka 1925, alipozaliwa katika kijiji cha Kivule katika eneo la kisiju Pwani, Wilaya ya Mkuranga katika Mkoa wa Pwani wa Tanzania.

Mzee Mwinyi utotoni alipewa na wazazi wake jina la Sihaba, likiwa na maana ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwajaalia mtoto wa kiume, wazazi wake mpaka anazaliwa yeye walikuwa na watoto wa kike tu.

Alipotimu miaka 4 safari ya maisha ya Mzee Mwinyi iliingia katika hatua muhimu ambayo ilibadili mustakabali mzima wa maisha yake yote ya baadaye. Baba yake, Mzee Hassan Mwinyi aliamua kumpeleka kijana huyo visiwani Zanzibar ili akapate malezi na mafunzo ya kidini.

Katika kitabu cha maisha yake kilichochapishwa mwaka 2020, Mzee Mwinyi anaeleza kuwa baba yake alitamani awe mchamungu na mwanazuoni mkubwa.

Na ili kufikia azma hiyo, Baba yake alitamani asome dini mpaka kufikia katika chuo maarufu cha enzi hizo visiwani Zanzibar cha Ukutani.

“Kuhusu elimu ya dini, zama zile wasomi wakubwa walipatikana miongoni mwa watu waliosoma Chuo cha Ukutani, Unguja. Enzi zile, kwa watu wa Zanzibar na Afrika ya Mashariki, umashuhuri wa chuo hicho kwa elimu ya dini ulifanana na ule wa Vyuo Vikuu vya Oxford na Cambridge vya Uingereza kwa elimu ya dunia.

Ndio maana nilipotimia umri wa miaka minne baba alinifungia safari ya Unguja ili nikaanze kusoma katika vyuo vya chini kwanza ili mwishowe nami nifike Ukutani,” ameandika Mzee Mwinyi katika kitabu chake.

Safari ya elimu ya Mzee Mwinyi
Alipowasili Unguja Mzee alikabidhiwa kwa malezi katika familia ya rafiki wa baba yake katika kijiji cha Mangapwani. Na kama ilivyopangwa, alipelekwa mwanzo katika chuo cha kufunza watoto Kurani.

Akiwa anaendelea na masomo ya Kurani katika kijiji cha Mangapwani, fursa ya elimu ya shule msingi ikajitokeza, alijiunga darasa la kwanza mwaka 1933 akiwa na umri wa miaka minane na nusu katika shule ya msingi Mangapwani .

Baada ya kusoma kwa miaka minne katika shule hiyo Mzee Mwinyi alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wawili tu waliochaguliwa kuendelea na masomo katika Shule ya Kati ya Dole ambayo ilikuwa ni ya bweni na kusoma hapo mpaka darasa la nane.

Mzee Mwinyi anaeleza katika kitabu cha maisha yake kuwa mpaka anamaliza masomo yake ya elimu ya msingi alikuwa hakosi katika orodha ya wanafunzi watatu bora.

Baada ya kumaliza masomo ya msingi aliendelea na masomo ya sekondari na baaadaye mafunzo ya awali ya ualimu hapo hapo Dole mwaka 1944.

Mzee Mwinyi alianza rasmi kazi ya ualimu mara tu baada ya kuhitimu masomo. Baada ya kufanya kazi kwa miaka 10 Mzee Mwinyi alipelekwa masomoni nchini Uingereza katika Chuo Kikuu cha Durham kuendelea na masomo ya ualimu kati ya mwaka 1954 na 1956.

Kati ya mwaka wa 1961 na 1962 Mzee Mwinyi alirejea nchini Uingereza kwa mafunzo zaidi katika Chuo Kikuu cha Hull, na aliporejea Zanzibar aliteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Ualimu , kazi aliyoifanya mpaka mwaka 1964 yalipotokea Mapinduzi ya Zanzibar.

Mzee Mwinyi aliupenda ualimu na alikipenda Kiswahili, haikuwa ajabu mara kwa mara kumsikia katika uhai wake akikemea matumiza mabovu ya lugha.

Mapinduzi na kuingia serikalini

Baada ya kutokea kwa mapinduzi ya Januari 12, 1964 visiwani Zanzibar ambapo utawala wa Kisultani uliangushwa, watumishi wengi wa umma hasa raia wa Uingereza waliondoka visiwani humo na kuacha ombwe la uongozi serikalini.

Mzee Mwinyi akateuliwa na aliyekuwa rais wa kwanza wa Zanzibar Abedi Amani Karume kuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Elimu.

Mwezi Aprili 1964, serikali za Zanzibar chini ya hayati Karume na ya Tanganyika chini ya Mwalimu Julius Nyerere zikaungana kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Miaka sita baadaye, Disemba 1970 akateuliwa kuwa Waziri katika serikali ya muungano na kuhudumu katika wizara mbali mbali, akianzia katika Ofisi ya Rais, kisha Afya kutoka 1972 mpaka 1975.

Mwaka 1975 Mwalimu Nyerere alimteua Mzee Mwinyi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi mpaka alipojiuzulu mwaka 1977 akiwajibika kufuatia ukiukwaji wa haki za binadamu wa vyombo vya dola katika operesheni maalumu ya kudhibiti mauaji ya watu wakongwe katika mikoa ya kanda ya ziwa nchini .

Baada ya kujiuzulu, Mwinyi aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri kutoka mwaka 1978 mpaka 1981.

Urais wa Zanzibar…Tanzania

Aliporejea kutoka Misri Mzee Mwinyi alirudi kwenye Baraza la Mawaziri la Nyerere mpaka mwaka 1984.

Januari 1984 kulitokea kile ambacho huitwa katika historia ya siasa za Tanzania kama ‘kuchafuka kwa hali ya hewa Zanzibar ambapo aliyekuwa Rais wa Zanzibar Aboud Jumbe alilazimika kujiuzulu nyadhfa zote kwenye chama na serikali.

Baada ya kujiuzulu kwa Mzee Jumbe, Mzee Mwinyi aliteuliwa na uongozi wa chama chini ya Mwalimu Nyerere kuwa Rais wa Zanzibar mpaka kufikia uchaguzi mkuu wa 1985.

Mwaka 1985, ulikuwa mwaka muhimu katika historia ya siasa za Tanzania, Mwalimu Nyerere alikuwa anang’atuka madarakani.

Katika kitabu chake Mzee Mwinyi anaeleza kuwa wengi, akiwemo yeye mwenyewe, waliamini aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo na mwanadiplomasia mbobevu Dkt Salim Ahmed Salim alikuwa anaenda kumrithi Mwalimu.

Haikuwa hivyo, kwa mujibu wa Mzee Mwinyi baadhi ya Wazee wenye msimamo mkali wa kihafidhina ndani ya CCM walimkataa Dkt Salim na Mwalimu Nyerere alilazimika kukubali ili kulinda umoja wa chama hicho. Bahati kwa mara nyingine tena ikamwangukia Mzee Mwinyi.

Mzee Mwinyi aliingia madarakani wakati ambapo Tanzania ilikuwa ikipitia wakati mgumu kiuchumi. Alilazimika kufanya mabadiliko ya kisera na kisiasa ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Mabadiliko hayo hayakuwa rahisi kutokea kwa kuwa bado ndani ya serikali na chama cha CCM kulikuwepo na wale walioamini na kutaka kuendelea kwa mfumo wa Ujamaa.

Hata hivyo, Mzee Mwinyi alishikilia hatamu za uongozi barabara na kutekeleza alichokiamini, hali iliyofanya utawala wake ujitanabaishe zaidi na mabadiliko kuanzia ya kisera, kisiasa na kiuchumi.

Ni wakati wa utawala wake ndipo serikali ilipoanza kuchukua hatua za kurudi nyuma katika kuendesha uchumi moja kwa moja na kuruhusu sekta binafsi kuingia, mfumo wa vyama vingi kurejea pamoja na kuruhusiwa kwa vyombo vya habari binafsi.

Hayo na mengineyo yakampatia jina ambalo litaendelea kuwa kielelezo cha uongozi wake: Mzee Rukhsa.

Si wote waliofurahia mabadiliko yake, hususan wahafidhina wa Ujamaa. Pia katika vitu ambavyo anakosolewa navyo ni kuwa mabadiliko aliyoyaleta yalichochea kushamiri kwa rushwa nchini Tanzania.

Katika kitabu chake, anataja mambo kadhaa kuwa ni changamoto alizokutana nazo akiwa uongozini,
na wafanyakazi.

Diaspora Italy
Contact us: +39 389 8583370

Email: info@ tzabroad.com

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %