Na Mwandishi Wetu ZAIN
ACCRA GHANA
NINI CHA KUJIFUNZA KWA WENZETU KATIKA KUTUMIA KUMBUKUMBU ZA MASHUJAA WA TAIFA
Waghana wanamkumbuka, wanamsheherekea na wanajifunza kuhusu Kwame Nkurumah kila siku, na wanaingiza pesa nyingi pia kwa kutumia ukumbusho huo wa rais wao wa kwanza.
Wametenga eneo kubwa kama la uwanja wa mpira katikati ya jiji la Accra pembeni kidogo na eneo la kitaifa la kusheherekea uhuru wao (Independence square)
Kuna kiingilio, wenyeji wanalipa Ghana cedes 25, wageni wanalipa cedes 100. Watoto wa shule ni wengi kwa makundi hutembelea makumbusho haya.
Ndani ya uwanja kuna bwawa lenye sanamu za makumbusho, kuna viduka vidogo vidogo, kuna ukumbi wa mikutano, vyakula na muziki. Kuna jumba ambalo linahifadhi kaburi la Kwame Nkurumah na kuna majengo mawili ambayo yamerasimishwa kuonyesha historia na maisha ya Kwame Nkurumah.
Ndani ya majengo ya makumbusho hairuhusiwi kupiga picha. Yaliyomo ni historia kamili ya Kwame Nkurumah, tokea kuzaliwa kwake, kusoma kwake, kazi zake, kujiunga na siasa, urais wake, mafanikio yake, kila kazi au mradi alioufanya umeelezwa hasa kuhusu elimu, afya na matibabu, maji, umeme, usafiri, nk. Ndoa zake zote mbili zimetajwa, watoto wake, kupinduliwa kwake, kuishi kwake uhamishoni, kifo chake, na utata wa kurudisha mwili wake Ghana.
Harakati zake za ukombozi wa Afrika na kauli zake za ukombozi ikiwemo ukombozi wa Ghana haujakamilika kama Afrika haijakombolewa.
Mapicha ni mengi na pia kuna baadhi ya vitu ambavyo alivitumia wakati wa uhai na uongozi wake. Vitu hivyo ni pamoja vitu vya ofisini, nyumbani, zawadi alizopewa nk. Kwenye mlango mkuu kuna gari aina ya Cadillac 1961 ambalo rais Nkurumah alipewa zawadi na rais Kennedy wa Marekani.
Ukitoka kwenye makumbusho haya utatoka tofauti na ulivyoingia, utakuwa na elimu tele kuhusu huyu mwamba Nkurumah, ukombozi wa Ghana na Afrika kwa ujumla.
Ni kumbukumbu ambayo inaweza kufananishwa na ile ya Mao Tse Tung kule Beijing China.
Tanzania tuna nafasi ya kulifanya hili kwa kutumia historia ya mwalimu Nyerere. Biashara ya makumbusho ni pamoja na ubunifu kama kuwepo karibu na vivutio vingine au kuwa katikati ya jiji.