Na GFAMILY KAGUTTA
WU®MEDIA
Kaimu balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Italia, Bi Jubilata Mgaya siku ya jana tarehe 3/08/2024 aliungana na Watanzania nchini Italy katika zoezi la kuaga mwili wa marehemu Juma Ally Ngunike aliyefariki jijini Napoli siku ya tarehe 17/07/2024.
Marehemu alifariki baada ya kuchukua maamuzi ya kutoa uhai wake mwenyewe kwa kujinyonga kwa mujibu wa mashuhuda na ripoti ya Uchunguzi iliyotolewa na Jaji wa mahakama ya Napoli.
Katika tukio hilo la kusikitisha sana, Marehemu aliacha maandiko yaliyoeleza kisa na sababu za kupata shinikizo la kufanya maamuzi ya kutoa uhai wake.
Shughuli za kuaga mwili wa marehemu zilianza kwa taratibu za imani za Dini, na ziliongozwa na Imam wa Jumuiya ya Watanzania Italia mkoa wa campania, Maalim Rajab Kunga. Baada ya taratibu zote kukamilika na Watanzania wote kupata kutoa heshima zao za mwisho kwa kuzunguka Jeneza la marehemu, Maalim Rajab Kunga alipata nafasi ya kutoa neno. Maalim alieleza na kukumbusha watu kuwa Umauti upo na cha muhimu ni kujiandaa kwa kufanya amali njema. Pamoja na mengi aliyoongea pia alisisitiza na kuasa watu wenye tabia ya kutumia misiba kuchochea chuki,fitna na kuzushiana mambo yasiyofaa ..” inapotokea misiba ni wakati wa kuwa pamoja na kila mmoja kutoa ushirikiano badala ya kuwa kikwazo katika kukamilisha taratibu za kuwastiri marehemu zetu.” Alisema Maalim Rajab Kunga.
Baada ya tukio hilo lililofanyika kwanye viwanja vya Wakala wa Mazishi na misiba, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania Italia mkoa wa Campania ndugu Hussen Jiwe Msawira alielekeza kufuatana na ratiba, wageni na waliohudhuria kuelekea katika ukumbi uliopangwa kwa ajili ya kupata sadaka ya chakula pia kuweza kumsikiliza Kaimu balozi ambae aliongozana na baadhi ya wafanyakazi wa Ubalozi.
Kwa upande wa ndugu wa Marehemu aliongea kwa niaba ya familia mpwa wa marehemu ambae anaishi nchini Uingereza Dada Halima Khalid, aliwashukuru sana Watanzania na kuwaombea Mungu. Ndugu Andrew Mhela ambae ni Katibu wa kamati kuu ya Diaspora alitoa salaam fupi kwa niaba ya Kamati kuu ya Diaspora Italia, na kwa niaba ya Jumuiya ya Watanzania Roma, vilevile alikabidhi michango ya Jumuiya ya Watanzania Roma kiasi cha Euro 880.
Kaimu Balozi aliongea mwisho, kutoa salaam za rambirambi kutoka kwa Ubalozi na serikali kwa ujumla wake. Pia alitoa salamu Maalumu kutoka kwa Mh. Balozi Mahmoud Thabit Kombo ambae wakati unatokea msiba alikuwa bado ni Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Italy. Mh. Balozi Kombo sasa ni Waziri wa mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kaimu Balozi Mh. Jubilata Mgaya alisema Waziri wa mambo ya nje anatoa salaam za rambirambi na pole kwa wafiwa na Diaspora wote kwa ujumla na anaungana nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Pamoja na mengi aliyoongea kaimu Balozi pia amesema kutokana na mazingira ya kifo cha marehemu Juma Ally Ngunike , ubalozi upo tayari kumsikiliza Mtanzania yeyote anaepitia changamoto ambazo anaona zinaathiri afya yake ya ubongo. ameahidi kulifanyia kazi ili kuja na mpango maalumu kwa kuwa ameona hili ni tatizo kubwa linalowakumba Diaspora lakini halijatolewa kauli na kufanyiwa kazi kutokana na kutozungumzwa hadharani. Kaimu balozi amesisitiza tena kuwa kama ilivyokuwa wakati wa Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Ubalozi utaendelea kushirikiana kwa karibu na Jumuiya zote za Watanzania nchini Italy na maeneo yote ya uwakilishi wake, na aliwatoa wasiwasi Watanzania kuwa Balozi Kombo sasa ndie Mkuu wa balozi zote hivyo bado yupo karibu sana na Diaspora.
Uongozi wa Jumuiya ya Watanzania Italia mkoa wa Campania utatoa ratiba ya safari ya mwili wa marehemu siku ya jumatatu 5/08/2024 kuelekea nyumbani Tanzania kwenye nyumba yake ya milele.
“INNALILLAH WAINNA ILLAH RAJ UUN”