0 0
Read Time:2 Minute, 16 Second

Na Mkali

Kalamu ya Mkali yamjibu Mwenyekiti wa baraza la wazee wa CDM

Tarehe 01/10/2024, katika maadhimishamo ya Siku ya Wazee Duniani, Ndugu Hashimu Juma Issa, ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chama cha Chadema alitoa matamko yenye upotoshaji mkubwa; tena ni upotoshaji wenye chembechembe za uchochezi unaoweza kuzua janga la udini ambao hatima yake inaweza kuwa ni kuvuruga amani na mshikamano wa taifa letu.

Imekuwa ni vizuri sana kwamba siku iliyofuata, Chama cha Chadema kilimkemea huyu mzee kwa kujiweka mbali na kauli zake.

Pamoja na makanusho mazuri ya Chama chake, naona kuna umuhimu wa kumkumbusha huyu mzee na watu wenye mawazo ya aina yake kweli kadhaa zifuatazo:

(1) Waanzilishi wa Taifa letu walipojenga ustaarabu wa mifumo inayokataza nchi yetu kuwa na dini ya taifa, yaani “state religion” hawakukurupuka kamwe. Walizingatia historia ya ulimwengu iliyojaa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyotokana na mifumo ya kuwa na dini za taifa.
Na hivi sasa hili katazo letu limekwisha kuwa ni tunu ya taifa; kama ilivyo kuwa kwetu taifa huru ni kwa milele, halikadhalika hili katazo ni la kudumu kwani ulinzi na usalama wa taifa letu hauna kikomo, ni endelevu.

(2) Hiki chama kinachoitwa OIC – Organisation of Islamic Countries ni ‘Club’ ya nchi zinazosadiki mambo ya dini za taifa. Sasa Tanzania nchi ambayo siyo muumini wa dini za taifa kujiunga na OIC tutakuwa tunakwenda kutafuta nini huko?

(3) Huyu mzee pia amepotosha umma alipodai kuwa huko nyuma Tanzania haikujiunga na OIC kwa sababu Rais wetu alikuwa ni mkiristo. Hiyo si sahihi. Hatujiungi kwa sababu sheria zetu haziruhusu. Na sheria haziruhusu kwa sababu za usalama wa taifa. Aidha hayupo Kiongozi awe ni mkristo au muislamu ambaye amepewa mamlaka ya kuhatarisha usalama wa Taifa kwa sababu yoyote ile.

(4) Hata kama alivyosema kuwa sasa tuna: Rais wa Muungano, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu, Mawaziri wa Mambo ya Ndani na Nje wote waislamu, lakini hata hivyo hatuwezi kujitumbukiza kwenye OIC kwa sababu hao viongozi wote hawajapewa madaraka kuvuruga amani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hawana. Aidha hao viongozi wanaongoza kwa kuzingatia katiba, sheria, mila, tamaduni, yaani ustaarabu tuliojiwekea.

(5) Kama nilivyogusia hapo juu kuwa kutokuwa kwetu na dini ya taifa (state religion) ni tunu kama ulivyo uhuru wetu. Yaani hizi tunu pamoja na zingine zote zina uhai usio na kikomo. Rais na Baraza la Mawaziri, Wabunge na Majaji hawana mamlaka ya kufuta uhuru wa nchi.

HITIMISHO.

Watanzania karibu wote wana dini au imani zao; na Serikali yetu itaendelea kuheshimu hiyari ya wananchi kukumbatia imani zao. Lakini Tanzania itaendelea kubaki haina dini ya taifa (state religion). Lengo ni kudumusha amani, usalama na umoja wa Taifa letu.

Kwa taarifa yako mzee wetu, mimi mwenye kuleta andiko hili ni muislamu.

mkali@live.co.uk.
05/10/2024.

Happy
Happy
67 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
33 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %