0 0
Read Time:1 Minute, 23 Second

WABONGO UGHAIBUNI MEDIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo(Mb.), ametoa rai kwa Jumuiya ya Diaspora wa Tanzania wanaoishi nchini Hungary kuendelea kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwao na kujiepusha na vitendo vyovyote vya uvunjifu wa sheria za nchi hiyo ili kulinda taswira nzuri ya nchi.

Rai hiyo ameitoa alipokutana kwa mazungumzo na Jumuiya hiyo leo Februari 24, 2025 nchini humo ikiwa ni sehemu ya ziara yake.

Katika mazungumzo yake na Jumuiya hiyo, Mhe. Waziri Kombo aliwaeleza masuala mbalimbali yanayoendelea nchini, ikiwemo miradi ya maendeleo pamoja na dhumuni la ziara yake nchini humo kuwa ni pamoja na kuendelea kuzungumza na Serikali ya Hungary ili kupanua wigo wa kozi zinazotolewa katika ufadhili huo ili kujumuisha kozi zinazohitajika zaidi nchini kama udaktari, uuguzi na uhandisi.

Aidha, Mhe. Waziri Kombo alitumia fursa hiyo kueleza jitihada zinazofanywa na Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Sayansi ili kuhakikisha Tanzania inatumia kikamilifu fursa ya Mpango wa Ufadhili wa Masomo unaotolewa na Hungary yaani ’Stipendium Hungaricum Scholarship’ kwa kuhakikisha nafasi 30 zinazotolewa na nchi hiyo kila mwaka zinajazwa ili kuwawezesha Watanzania kunufaika na elimu bora inayotolewa nchini Hungary.

Kwa upande wa Diaspora hao ambao wengi wao ni wanafunzi, waliwasilisha changamoto na mapendekezo kwa ajili ya kufanyiwa kazi na Serikali ya Tanzania ili kuboresha zaidi ushiriki wao katika kujenga Taifa wawapo nchini Hungary na hata watakaporejea nchini ambapo Mhe. Waziri alipokea changamoto na mapendekezo hayo na kuahidi kuwa Wizara itafanyia kazi.

Pia , Mhe. Waziri Kombo alitumia fursa hiyo kutoa vyeti vya pongezi kwa Diaspora wote walioshiriki kuwasaidia Watanzania wenzao waliokuwa Ukraine kipindi cha vita ikiwa ni ishara ya kutambua mchango uliotolewa na Diaspora hao.

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %